Ripoti yaeleza haki ya kufanya siasa inavyominywa nchini

Katiba ya Jamhuri ya Muungano inatambua haki ya watu kushiriki siasa na inautambua mfumo wa siasa wa demokrasia ya vyama vingi.

Mbali na Katiba, haki za kiraia na kisiasa zinalindwa na mikataba ya kimataifa ambayo Tanzania imesaini ikiwa pamoja na Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa (ICCPR) wa mwaka 1966, Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu (ACHPR).

Mikataba mingine ni ule wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu juu ya Haki za Wanawake barani Afrika (Maputo Protocol) na Mkataba wa Afrika wa Haki na Ustawi wa Mtoto (ACRWC).

Hata hivyo, utekelezaji wa haki hizo umebaki kuwa kitendawili kutokana na kutungwa kwa sheria kinzani na matukio yanayokwenda kinyume na haki hiyo.

Hivi karibuni Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimezindua ripoti ya haki za binadamu kwa mwaka 2018 ikionyesha kuminywa kwa haki za kufanya siasa kwa mwaka 2018 ikilinganishwa na mwaka 2017.

“Hii ilichangiwa kwa kiasi kikubwa na uminywaji wa haki za uhuru wa kujieleza; ukiukwaji wa haki ya kuwa huru na salama na uhuru dhidi ya utesaji; na uminywaji wa uhuru wa kujumuika na haki ya kushiriki katika utawala,” inasema ripoti hiyo.

Hata hivyo, Msajili wa Vyama vya siasa, Jaji Francis Mutungi anakanusha kuvunjwa kwa haki ya kufanya siasa, akisema hayo ni maoni binafsi ya LHRC.

“Hayo ni mawazo yao na ni haki yao kuwa na maoni. Ni mawazo yao tu,” anasema Jaji Mutungi.

Ripoti hiyo pia imeangazia katika matukio ya kujichukulia sheria mkononi, vifo vinavyotokea mikononi mwa vyombo vya dola, ukatili dhidi ya maofisa wa vyombo vya dola, mauaji yanayotokana na imani za kishirikina, ukatili dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi, adhabu ya kifo na ajali za barabarani kama masuala makuu yaliyoathiri haki ya kuishi kwa mwaka 2018.

Haki ya kuishi

Hii ndiyo haki inayatazamwa kama haki ya msingi kuliko zote na ukiukwaji wa haki nyingine za msingi za binadamu pia uliathiri haki hii. Haki hiyo inatajwa kuimarika kwa mwaka 2018 kuliko mwaka 2017.

Haki nyingine zinazozungumziwa na ripoti hiyo ni pamoja na uhuru wa kukusanyika, uhuru wa kujumuika, haki ya kushiriki katika utawala au Serikali.

“Uhuru wa kukusanyika uliendelea kuathiriwa na katazo la kutofanya mikutano ya hadhara nje ya jimbo ya mwanasiasa husika.

“Wanasiasa kadhaa wa vyama vya upinzani walikamatwa kwa kutotii katazo hili, japo halina uhalali wa kisheria na kulikuwa na malalamiko ya maombi ya kukusanyika kukataliwa mara kwa mara na Jeshi la Polisi,” inasema ripoti hiyo.

Uhuru wa kukusanyika

Ripoti inasema ukiukwaji wa uhuru wa kukusanyika mwaka 2018 uliathiri kwa kiasi kikubwa utekelezaji na ufurahiaji wa uhuru wa kujumuika.

“Mwaka 2018 vyama vya upinzani vililalamika kuhusu kutotendewa haki katika utekelezaji wa shughuli za kisiasa, ikiwamo kubughudhiwa, kunyimwa au kucheleweshewa dhamana katika kesi mbalimbali na adhabu za vifungo.

Inataja pia mapendekezo ya marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa ya mwaka 1992 yaliyotolewa mwaka 2018 kuwa yalitishia zaidi uhuru wa kujumuika wa vyama vya siasa.

Vifungu kadhaa vya sheria hiyo, vinatajwa na ripoti hiyo kuwa tishio kwa uhuru wa kujumuika wa vyama vya siasa na vingine vikitajwa kuwa na maelezo yenye utata na hivyo kuacha mianya ya kuwa na tafsiri pana na kutumiwa vibaya.

Vilevile sheria hiyo inaelezwa kuwa vifungu visivyozingatia kanuni za haki asilia na vifungu vinavyotoa mamlaka makubwa kupita kiasi kwa msajili wa vyama vya siasa.

Ripoti hiyo inagusia utafiti uliofanywa na Shirika la Twaweza mwaka 2018 ulioonyesha kwamba uelewa wa wananchi kuhusu vyama vidogo vya siasa ni mdogo.

“Kwa mujibu wa utafiti huo, wananchi wengi wanavifahamu zaidi vyama vikubwa vitatu vya siasa, ambavyo ni CCM (asilimia 100), Chadema (asilimia 97) na CUF (asilimia 83).

“Uelewa mdogo kuhusu vyama vingine unaonyesha haja na umuhimu wa kutoingilia uhuru wa kujumuika na kukusanyika wa vyama vya siasa...,” imesema ripoti hiyo.

Kushiriki uchaguzi

Kuhusu haki ya kushiriki katika utawala au Serikali, ripoti hiyo inasema ni pamoja na haki ya kupiga na kupigiwa kura na haki ya kushiriki katika masuala ya siasa.

“Kwa mwaka 2018, LHRC ilifuatilia matukio kadhaa yaliyopelekea ukiukwaji wa haki ya kupiga na kupigiwa kura wakati wa chaguzi ndogo zilizofanyika katika maeneo mbalimbali Tanzania Bara.

“Wakati wa zoezi hili, vyama vya upinzani vililalamika kuhusiana na ukiukwaji kwa taratibu za uchaguzi, ikiwemo mawakala wao kunyimwa/kucheleweshewa vibali vya kuingia katika vituo vya kupigia kura,” inasema ripoti.

Ikitolea mfano Dar es Salaam, ripoti inasema malalamiko ya wapinzani yalisababisha polisi wafuasi wa Chadema kukabiliana na kusababisha kuuawa kwa mwanafunzi wa chuo cha usafirishaji.

Uhuru wa kujieleza

Kuhusu uhuru wa kukusanyika na uhuru wa kujumuika, ripoti hiyo inasema kukosekana kwake uliathiri kwa kiasi kikubwa haki ya kushiriki katika masuala ya siasa na kuchangia kwa kiasi kikubwa kupungua kwa nafasi ya ushiriki Tanzania Bara.

Hali hiyo pia inaelezwa kuchangia kupungua kwa nafasi ya ushiriki wa siasa.

“Kwa mujibu wa utafiti huo, ni asilimia 44 tu ya wananchi wanaridhia na utendaji kazi wa wabunge wao, huku asilimia 45 wakiridhika na utendaji wa madiwani wao,” inasema ripoti.

Mbali na ripoti, Wakili kutoka Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), Patience Mlowe anataja marekebisho ya Sheria ya Vyama vya siasa ya mwaka 2018 kukwaza ushiriki wa wananchi katika siasa.

“Ushiriki wa siasa ni haki ya kikatiba kwa vyama vya siasa, taasisi, vikundi na watu. Lakini kuna mtu amefanywa kuwa mwamuzi wa siasa na kufanya siasa sasa kumekuwa kama kosa la jinai.

“Msajili wa vyama vya siasa anaweza kufuta chama bila hata kufuata utaratibu wa mahakama. Yeye ni mteule wa Rais ambaye naye ni mwenyekiti wa chama cha siasa,” anasema Mlowe.

Maoni ya Mlowe yanaungwa mkono na Mkurugenzi wa Habari na Uhusiano wa nje wa Chadema, John Mrema akisema Sheria ya sasa ya vyama vya siasa imeweka mazingira magumu kwa vyama vya upinzani kufanya siasa, licha ya kuwa ni haki ya kikatiba.

“Msajili amekuwa mratibu hata wa itikadi ya chama, hata ukitaka kufanya mafunzo inabidi upate kibali kwake. Makatazo yamekuwa mengi kiasi kwamba imekuwa vigumu kufanya siasa,” anasema Mrema.