Breaking News

Ruto amwambia Rais Kenyatta: ‘Tumetoka mbali’

Wednesday July 10 2019

 

Nairobi. Naibu Rais wa Kenya, William Ruto ameendelea kumkumbusha bosi wake Rais Uhuru Kenyatta kuwa wametoka mbali tangu 2013.

Vilevile, ameeleza matumaini yake kuwa chama cha Jubilee hakitasambaratika kutokana na mzozo baina yao, kwani walikianzisha kama mbinu ya kuwanganisha Wakenya.

Ruto aliwakosoa viongozi wa Jubilee ambao wamekuwa wakilalamika kuhusu mambo ya chama hicho waziwazi, akiwataka waache kujiaibisha, badala yake wasuluhishe tofauti zao ndani ya chama, linaripoti Gazeti la Taifa Leo

Akizungumza katika eneo la Eldama Ravine, Kaunti ya Baringo, Dk Ruto aliwahakikishia wakazi kuwa chama hicho kiko imara, licha ya malumbano ambayo yamekuwa yakishuhudiwa kwa miezi sasa, na madai ya majuzi kuwa kuna mpango wa kumuua.

Ruto alisema hayo wakati wafuasi wake wakiendelea kumshinikiza Rais Kenyatta avunje Baraza la Mawaziri, kwa madai kuwa limegawanyika.

“Tuliamua na Rais kuunda chama baada ya kugundua kuwa siasa za Kenya zilikuwa zimezingirwa na chuki, ubinafsi na ukabila. Kulingana nami, hilo bado halijabadilika na sijafurahia,” alisema Dk Ruto ambaye mbio zake za kuwania urais 2022 zimeshika kasi.

Advertisement

“Tulipounda chama hiki, tulilenga kubadili siasa za nchi hii. Tulitaka kumaliza siasa za migawanyiko, chuki na fujo, ili tuwaunganishe Wakenya bila kujali makabila yao ama mirengo ya kisiasa wanakotoka,” akaongeza Naibu Rais.

“Jubilee haiko kwa ajili ya uchaguzi ambao umepita ama ambao unakuja. Ina kazi bora zaidi ya siasa na chaguzi. Kupeleka malalamishi na propaganda kwa vyombo vya habari badala ya chama ni usaliti,” akasema.

Aidha, aliendelea kujitetea kuhusu michango anayotoa makanisani ambayo imekuwa ikikosolewa, akisema anawekeza mbinguni.

“Tuna jukumu la kujenga kanisa kulingana na Biblia. Mungu anasema tuwekeze mali zetu mbinguni na hivyo ndivyo tunafanya. Wengine wanaoamua kuwekeza katika mambo mengine huo ni uamuzi wao,” akasema Dk Ruto.

Wakati Naibu Rais aliyekuwa ameandamana na Waziri wa Maji, Simon Chelugui, wabunge na viongozi wengine kadhaa akisema hayo, wandani wake walikuwa wakimtia presha Rais avunje baraza la mawaziri, na kuzungumza kuhusu madai ya njama ya kumuua Ruto.

“Wakenya walitarajia Rais angewatimua mawaziri waliotajwa katika madai ya njama hiyo huku uchunguzi ukiendelea,” Gavana wa Nandi Stephen Sang akasema.

Wakati huo huo, wabunge Oscar Sudi (Kapseret) na Didmus Barasa (Kiminini) walitishia kuanika kanda ya video ya mkutano ambapo mpango wa kumuua Ruto uliandaliwa, ikiwa Idara ya Upelelezi (DCI) haitakamilisha uchunguzi huo na kusema kilichoendelea.

“Kukamatwa kwa Dennis Itumbi (Mkurugenzi wa mawasiliano ya kidijitali Ikulu) ilikuwa hatua ya kuwahadaa Wakenya tu. Tunataka kuarifiwa kilichofanyika katika hiyo mikutano,” akasema Sudi.

Advertisement