Sheria mpya ya asasi za kiraia kisu kikali cha uhuru wa kujumuika

Historia ya vyama vya kiraia inatembea kwa kasi kurudi nyuma kabla hata ya uhuru. Hiki ni kipindi ambacho makundi ya wananchi yaliungana katika harakati za kudai Tanganyika huru.

Miongoni mwa makundi hayo ni chama Tanganyika African Association (TAA) kilichoanzishwa mwaka 1929 na ambacho baadaye kilijibadili na kuwa Tanganyika African Nation Union (Tanu), chama kilichopigania uhuru. Hata hivyo, wafanyakazi wa TAA hawakuwa huru kujitanua watakavyo kwa kuwa chama kilichokuwa rasmi kilikuwa cha Wafanyakazi wa Kiafrika wa Tanganyika (TAGSA).

Miongoni mwa viongozi wa TAGSA alikuwa Rashid Kawawa, ambaye alitumia nafasi hiyo kupinga ubaguzi wa rangi uliokuwapo wakati huo, na pia kudai masilahi kwa wafanyakazi.

Kawawa alikuwa pia mwanzilishi wa Shirikisho la Wafanyakazi la Tanganyika (TFL) mwaka 1955. Baadaye alijiunga na Tanu na kuwa kiongozi wa juu serikalini hadi uwaziri mkuu.

Baada ya Tanganyika kupata uhuru, baadhi ya vyama vya wafanyakazi na kiraia vilikufa na viongozi wake wakachukuliwa kuwa watendaji serikalini.

Mwaka 1964, TFL ilibadilishwa na kuwa National Union of Tanganyika Workers (Nuta), baadaye ikawa Jumuiya ya Wafanyakazi (Juwata), kisha Ottu na sasa Tucta.

Kwa kadiri mabadiliko hayo yalivyokuwa yakifanyika, nguvu ya vyama vya wafanyakazi iliendelea kupungua dhidi ya Serikali ndipo likatokea ombwe lililokuja lililojazwa na asasi mbalimbali za kiraia.

Sheria ya asasi za kiraia

Nje ya historia hiyo, mwaka 1990 zilianzishwa asasi za kiraia (Azaki) zikiwemo rasmi na zisizo rasmi. Hapa zipo za kiserikali, zisizozalisha faida, za kijamii, za kidini; vyama mbalimbali vikiwamo vya wafanyakazi, kitaaluma na vyombo vya habari. Ni kipindi hicho pia uliporejeshwa mfumo wa vyama vingi vya siasa.

Asasi zote hizo zimekuwa kama ilivyokuwa kwa vyama vya wafanyakazi, zimekuwa zikitoa mchango muhimu katika utetezi wa haki za kijamii, utoaji wa huduma na maendeleo ya nchi.

Pamoja na majukumu yote hayo, hivi karibuni Bunge limepitisha mabadiliko ya sheria ambayo wanaharakati wanayaona yanakwenda kuathiri shughuli hizo kwa kiwango kikubwa.

Sheria hizo ni ile ya makampuni, Sheria ya asasi za kiraia, Sheria ya takwimu, Sheria ya vyama vya Kijamii, Sheria ya filamu na michezo ya kuigiza, Sheria ya wakala wa usafirishaji majini, Sheria ya hatimiliki na ile ya miunganiko ya wadhamini.

Mabadiliko hayo yameibua mjadala mpana yakitajwa kuwa sehemu ya ukandamizaji wa demokrasia na yanakwenda kinyume na Katiba ya nchi.

Marekebisho hayo ya sheria yamekuja wakati pia kukiwa na malalamiko ya ukandamizwaji wa mfumo wa vyama vingi kupitia marekebisho ya Sheria ya vyama vya siasa ya mwaka 1992 ambayo yanapingwa mahakamani.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dk Adelardus Kilangi alipoulizwa juzi jioni alisema hakuwa kwenye nafasi nzuri kuzungumzia suala hilo, lakini akadokeza kuwa sheria hiyo imeshasainiwa na Rais.

Mapema, akiwasilisha muswada huo, Dk Kilangi alisema “lengo la marekebisho haya ni kutofautisha usajili wa kampuni na mashirika yasiyo ya kiserikali na kampuni. “Kifungu kipya cha 4A kinampa msajili mamlaka ya kufanya uchunguzi wa mwenendo wa shirika lolote lililo chini yake na ...Kifungu cha 8A kinaongezwa kwa kuweka masharti ya kufuta usajili wa shirika lisilo la kiserikali ambalo halikidhi masharti ya usajili.”

Kutokana na maudhui ya sheria hiyo, Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kimefanya kongamano jijini Dar es Salaam kuijadili na kutafakari jinsi ya kupambana nayo.

Rais wa TLS, Dk Rugemeleza Nshala anasema mabadiliko hayo yanakwenda kinyume na Katiba inayotoa uhuru wa wananchi kujiunga na vyama vya kiraia.

“Ibara 20 inasema, “Kila mtu anastahili kuwa huru kukutana na watu wengine .... na kuanzisha au kujiunga na vyama au mashirika yaliyoanzishwa kwa madhumuni ya kuhifadhi au kuendeleza imani au maslahi yake au maslahi mengineyo.”

Dk Nshala anasema mabadiliko ya sheria hiyo yamekuja kulenga baadhi ya mashirika yanayopaza sauti kinyume na misimamo ya Serikali.

“Mabadiliko haya yanawalenga wachache. Hizo ripoti nyingi zinazotakiwa kuwasilishwa watawakamata wachache wale wanaopiga kelele. Mwizi ni yule aliyekamatwa,” alisema Dk Nshala.

Anasema sheria hiyo inalenga kuziua asasi za kiraia zilizoajiri mamia ya wafanyakazi wanaotegemewa na jamii ya Watanzania.

Miongoni mwa mambo yanayolalamikiwa katika mabadiliko ya sheria hiyo ni usajili wa asasi hizo kwa kuzikataza kusajiliwa kama kampuni isiyozaa faida kwenye Wakala wa Usajili wa kampuni (Brela).

Dk Nshala ambaye pia ni mkurugenzi wa Chama cha Wanasheria wa Mazingira (Leat), anasema awali chama chao kilisajiliwa kwa msajili wa asasi za kiraia, lakini wakalazimika kukisajili kama kampuni baada ya kutishiwa kufutwa mwaka 2002.

“...Sasa wamekuja na sheria ya kukataa asasi kujisajili kama kampuni,” alisema.

Akifafanua zaidi kuhusu usajili, Wakili John Seka anasema mashirika yaliyosajiliwa kama asasi za kiraia yanatakiwa kupewa cheti cha usajili na yale yaliyosajiliwa kama kampuni yanatakiwa kuchukua kibali kinachofuta sifa ya kuwa kampuni.

Anasema asasi nyingi zilikuwa zikijisajili kupitia Brela kama kampuni kwa sababu ya urahisi, kwani kujisajili asasi ya kiraia kuna mchakato mrefu ikiwa pamoja na kutambuliwa na vikao vya kata, tarafa na wilaya kabla ya kwenda kwa msajili ukiwa na Katiba inayofuata mwongozo wake.

“Lazima msajili ajiridhishe kiasi gani umekubaliana na matakwa ya NGO. Kuna watu wengi watapoteza kazi,” anasema Seka.

Anasema kutokana na sheria hiyo, asasi hizo zina muda mfupi (miezi miwili) wa kufanya marekebisho ikiwa pamoja na kuwajulisha wafadhili wao marekebisho hayo, jambo linaloweza kuathiri ufadhili na utendaji wake na ajira za wafanyakazi wa asasi hizo.

“Unapokuwa na mchakato wa mabadiliko, inabidi umwambie mfadhili mapema kwa kuwa hauna uhakika wa kukubaliwa. Inabidi uwaambie wafanyakazi wako mapema. Hizi ndiyo athari za sheria hii,” anasema Seka.

Suala jingine lililoibua mjadala ni uharaka wa Serikali kupeleka marekebisho hayo bungeni kwa hati ya dharura.

Licha ya sheria hiyo kuandaliwa mapema, wanasheria hao wanadai kupewa siku moja ya kutoa maoni kabla ya muswada haujapelekwa bungeni, jambo wanalosema liliwanyima muda wa kusha kutoa mapendekezo yao.

Suala lingine lililoibuka ni sheria hiyo kutambua hata vikundi vya mitaani kama Vicoba kutambuliwa na sheria hiyo kama asasi za kiraia na hivyo kuzua hofu ya uwezekano wa ofisi ya msajili kuweza kuvihudumia vyote.

“Unapozungumzia NGO unaangalia zaidi ya taasisi 30,000 ngazi ya wilaya, kata mpaka ngazi ya chini. Kwa sheria ya sasa, hata mashirika ya kijamii huko mitaani yanatambuliwa kama asasi za kiraia. Kwa hiyo msajili atajikuta na taasisi za 100,000, ataelemewa,” anasema Seka.

Kwa upande wake Annagrace Rwehumbuza kutoka taasisi ya Tamasha, anasema sheria hiyo imelenga kuzifuta asasi za kiraia zinazoikosoa Serikali, huku pia akisema utekelezaji wa sheria hiyo utaongeza mwanya wa kutoa na kupokea rushwa.

“Wanataka kutufunga mdomo. Kwa mfano sisi tulipokuwa tukipiga kelele kwa suala la ‘teleza’ kule Kigoma tulitafuta msaada wa waziri lakini hatukufanikiwa.

“Tulitafuta msaada wa vyombo vya habari, tukapiga kelele. Kwa hali hiyo msajili anaweza asikupe tena usajili,” alisema Rwehumbiza.