Siku sita za mbanano Kamati ya Bajeti, Serikali

Tuesday June 11 2019

Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini akizungumza na

Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini akizungumza na watu wenye ualbino kutoka taasisi ya Hope Delivery Foundation walipotembelea Bunge, jijini Dodoma jana. Picha na Edwin Mjwahuzi 

By Fidelis Butahe, Mwananchi [email protected]

Dodoma. Siku moja kabla ya kusomwa Bajeti ya Serikali ya mwaka 2019/2020, Mwananchi limebaini mambo matano yanayotikisa vikao vya pamoja kati ya Serikali na Kamati ya Bunge ya Bajeti.

Vikao hivyo vilivyoanza Ijumaa iliyopita na kutarajiwa kumalizika kesho vinajadili hoja zilizoibuliwa na wabunge katika mijadala mbalimbali wakati wizara 19 zilipokuwa zikiwasilisha bajeti zake kuanzia Aprili 2.

Mambo hayo ni mapato ya vitambulisho vya wajasiriamali kutoonekana vitabu vya mapato, malimbikizo ya watumishi wa umma, malimbikizo ya kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ambayo hayajarejeshwa kwa wahusika, Serikali kutotoa fedha za ahadi yake ya kumalizia ujenzi wa maboma ya shule na hospitali na fedha za kumalizia miradi ya maji.

Vitambulisho

Katika mmoja wa mijadala bungeni, mbunge wa Momba (Chadema), David Silinde aliibana Serikali kuhusu kutoonekana kwa fedha za vitambulisho vya wafanyabiashara wadogo katika kitabu cha mapato.

Hoja hiyo ya Silinde ilijibiwa na Waziri wa Fedha, Dk Philip Mpango lakini mbunge huyo ambaye pia ni mjumbe wa kamati ya Bunge ya Bajeti hakuridhika na kabla ya kushika shilingi ili wabunge wengine wamuunge mkono kujadili hoja yake, Spika Job Ndugai aliingilia kati na kuagiza suala hilo likajadiliwe kamati ya Bajeti na kwamba angelifuatilia kwa kina.

Advertisement

Desemba 10, mwaka jana Rais Magufuli alitoa vitambulisho 670,000 kuwatambua wafanyabiashara wadogo nchini kuhakikisha wanafanya shughuli zao bila kusumbuliwa.

Siku hiyo kila mkuu wa mkoa alipewa vitambulisho 25,000 ambavyo kila mjasiriamali analipia Sh20,000 na fedha hizo kupelekwa Mamlaka ya Mapato (TRA). Baadaye jumla ya vitambulisho 1.1 milioni viliongezwa.

Silinde alisema mapato hayo hayaonekani katika ofisi za sekretarieti ya mikoa, Tamisemi wala ofisi ya Waziri Mkuu.

Hata hivyo, Dk Mpango alijibu, “ni suala la msingi. Sio kila mapato ya Serikali yanakuwa yanaonyesha item kwa item ( kipengele kwa kipengele) kwenye volume one (kitabu namba moja cha mapato). Viko vyanzo ambavyo tunaviingiza kwenye mfuko mkuu….. Fedha hizi zipo tumezibajeti kama sehemu ya mapato ya mfuko mkuu.”

Malimbikizo watumishi

Suala jingine lililotikisa Bunge ni Serikali kutolipa malimbikizo ya watumishi wa umma ikiwa ni pamoja na likizo, uhamisho na kupandishwa madaraja.

Aprili 15, bungeni jijini Dodoma naibu waziri wa Tamisemi, Mwita Waitara alisema hadi siku hiyo walimu 86,000 walikuwa wanaidai Serikali zaidi ya Sh43 bilioni yakiwamo malimbikizo ya mishahara na likizo.

Waitara alifafanua kuwa Serikali ilisitisha kupandisha walimu na watumishi wengine madaraja mwaka wa fedha 2015/16 na 2016/17 kutokana na uhakiki wa watumishi uliohusisha uhalali, elimu na ngazi za mishahara.

Alisema lengo la uhakiki lilikuwa kuhakikisha kuwa Serikali inabaki na watumishi wenye sifa na wanaostahili kulipwa.

VAT

Mbunge wa viti maalumu (CUF), Zainab Mndolwa alihoji malimbikizo ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwenda katika viwanda, kwamba kwa miaka minne Serikali wamerejesha Sh6 bilioni tu huku kukiwa na malimbikizo ya Sh45 bilioni.

“Tusimdanganye Rais (John Magufuli), anataka Tanzania ifikie katika uchumi wa viwanda. Wafanyabiashara wameandika barua lakini kilichorudishwa ni Sh6 bilioni, sasa Serikali inawakwamisha wawalipe kwa wakati kwa sababu ni fedha zao,” alisema.

Fedha za ujenzi wa maboma

Hoja nyingine inayotikisa kikao hicho ni ahadi ya Serikali mwaka 2017/2018 kutoa kiasi cha fedha kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa maboma ya shule na hospitali yaliyojengwa na wananchi.

Mmoja wa wabunge ambaye hakuwa tayari kutajwa jina lake amesema katika ahadi ya Serikali ya Sh251bilioni, kiasi kilichotolewa ni Sh67 bilioni.

Fedha miradi ya maji

Suala la kutopelekwa kwa fedha za maji lilitikisa hadi Kamati ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kubainisha kuwa fedha zilizotengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya maji katika mwaka wa fedha 2019/2020 zimepungua kwa asilimia tisa ya fedha zilizoidhinishwa mwaka 2018/19.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mahmoud Mgimwa alisema tatizo la upungufu wa maji safi na salama nchini ni kubwa, ambapo upatikanaji wa maji safi ni asilimia 64.8 vijijini na asilimia 85 mjini.

Alisema makadirio ya matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2019/2020 hayakidhi mahitaji makubwa ya maji kama yalivyoelezwa katika mpango wa taifa wa maendeleo wa miaka mitano ambao umebainisha maji kama kipaumbele kimojawapo cha kukuza uchumi.

Advertisement