Sita wadaiwa kuiba nyaya za TTCL, Tanesco

Muktasari:

  • Watuhumiwa wadaiwa kuuza nyaya hizo kama vyuma chakavu
  • Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Mohammed Mpinga alisema jana kuwa katika msako wa kutafuta mtandao wa uhujumu uchumi huo waliwakamata vijana hao wakazi wa jijini hapa.

Watu sita mkoani hapa wamekamatwa kwa tuhuma za kuiba nyaya za mitandao ya simu mali za Kampuni ya Mawasiliano ya Tanzania (TTCL), Shirika la Umeme (Tanesco) na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira jijini Mbeya (Mbeya-UWSA).

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Mohammed Mpinga alisema jana kuwa katika msako wa kutafuta mtandao wa uhujumu uchumi huo waliwakamata vijana hao wakazi wa jijini hapa.

Alidai kuwa watuhumiwa walikutwa na miundombinu hiyo waliyoiiba kwa kukata nyaya kwenye nguzo na nyingine kuzichimbua ardhini.

“Baada ya kupata taarifa za uhujumu uchumi katika miundombinu hii, tulifanya msako na kuwakamata vijana sita ambao walipekuliwa katika karakana lao za kuuzia vyuma chakavu na kukuta nyaya za TTCL, Tanesco na mita za kusomea maji, mali ya Mamlaka ya Majisafi Jiji la Mbeya,”alisema Kamanda Mpinga.

Alisema watuhumiwa wote baada ya kuhojiwa walikiri kushiriki katika wizi na kuhujumu miundombinu ya TTCL, Tanesco na Mbeya-UWSA.

Kamanda Mpinga alisema kuwa watuhumiwa hao wamekuwa wakiuza nyaya hizo kama vyuma chakavu na kwamba muda wowote watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani.

Mkuu wa Biashara wa TTCL, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Juvenal Utafu alisema kuanzia Julai hadi Desemba mwaka jana TTCL mikoa ya Mbeya na Songwe iliibiwa mita 4,230 za nyaya ambazo ni mikonga yenye shaba ndani yake.

Alisema kutokana na matukio hayo wateja 335 waliathirika kihuduma.

Utafu alisema nyaya zilizoibwa katika kipindi hicho zinagharimu Sh164.26 milioni huku akibainisha kwamba kwa sasa kuna tatizo kubwa la wizi wa miundombinu ya TTCL.

Alisema pamoja na TTCL na polisi kuendelea kufanya msako kubaini mitandao inayohusika na uhujumu uchumi pia aliwaomba wananchi kutoa ushirikiano katika kulinda rasilimali za umma kwa kutoa taarifa za watu wanaowahisi wanajihusisha na uhalifu huo.

Msimamizi wa Kitengo cha Ujenzi-Tanesco Mkoa wa Mbeya, Nyamagwila Maagi alisema kwa sasa Tanesco imekuwa ikiathiriwa zaidi kwenye utoaji huduma kwa wananchi kutokana na wizi unaofanywa na watu kwa kukata nyaya na kwenda kuziuza.

“Sasa hivi imefikia mahala wezi wanaingia kwenye nyumba za watu binafsi na kukata baadhi ya vifaa katika mitaa zetu na kuondoka navyo, na athari yake mteja kukosa umeme, lakini na shirika kuanza kuingia hasara nyingine ya kumrudishia mteja huduma ya umeme,” alisema Maagi.