VIDEO-Sugu aelezea alivyokuwa akilala mzungu wa nne gerezani-1

Muktasari:

  • Fununu za kuachiwa kwa mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ zimeenea kila mahali. Polisi wamejipanga maeneo yote ya gerezani kulinda usalama.

Mbeya. Nje ya Gereza Kuu la Ruanda, kuna umati mkubwa wa watu. Viongozi wa Chadema wakiongozwa na mwenyekiti wao, Freeman Mbowe wanasubiri kwa hamu kubwa.

Fununu za kuachiwa kwa mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ zimeenea kila mahali. Polisi wamejipanga maeneo yote ya gerezani kulinda usalama.

Viongozi wa Chadema wanaonekana wakizungumza kwa simu, wengine wakiwa katika vikundi vikundi wakijitahidi kuvuta muda kusubiri jambo moja tu, kuachiwa kwa Sugu.

Hata hivyo, umati huo pamoja na Mbowe wanapigwa chenga ya mwili wanapoambiwa kuwa Sugu na mwenzake Katibu wa Chadema Kanda ya Nyasa, Emmanuel Masonga wameshaondoka gerezani hapo tangu saa moja na nusu asubuhi na tayari wamefika nyumbani.

Hizo zote ni mbwembwe, lakini ukweli unabaki kuwa Mei 10, mwaka huu, itabaki kuwa kumbukumbu Sugu aliyeachiwa huru kutoka gerezani alikokuwa akitumikia kifungo cha miezi mitano alichohukumiwa baada ya kukutwa na kosa la kutumia lugha ya fedheha dhidi ya Rais John Magufuli.

Sugu alitolewa gerezani kwa msamaha wa Rais alioutoa Aprili 26, mwaka huu baada ya kukidhi vigezo vya msamaha huo sawa na wafungwa wengine zaidi ya 3,000 waliopunguziwa robo ya vifungo vyao.

Mpaka wakati anatolewa gerezani, Sugu alikuwa tayari ameishi siku 73 katika Gereza Kuu la Ruanda ambako alifungwa tangu Februari 26.

Katika mahojiano maalumu na Mwananchi, Sugu anasema maisha aliyoishi ndani ya gereza hilo si mazuri hata kidogo.

Sugu anasema gereza hilo lilijengwa tangu enzi za ukoloni likiwa na uwezo wa kuhudumia wafungwa kati ya 400 na 450 kwa wakati mmoja.

Sugu ambaye pia ni msanii wa muziki anasema kwa sasa gereza hilo lina wafungwa na mahabusu zaidi ya 1,400 ambao wanahudumiwa na gereza hilo kwa wakati mmoja.

Anasema kutokana na idadi kubwa ya wafungwa na mahabusu waliopo ndani ya gereza hilo, maisha ya wafungwa na askari wa gereza hilo ni magumu kuliko watu wengi wanavyofikiria wakiwa nje ya gereza.

Azungumzia malazi

Sugu anasema katika gereza hilo, kila chumba kimekusudiwa kulala wafungwa kati ya 21 hadi 26, lakini chumba hicho hicho kwa sasa wanalala wafungwa kati ya 80 hadi 100 hali ambayo inasababisha walale wakiwa wamerundikana kiasi kwamba hakuna hata njia ya kupita wakati mfungwa anapohitaji kwenda chooni kujisaidia.

Anasema gereza hilo pia lina uhaba mkubwa wa magodoro, hali ambayo inasababisha godoro moja dogo lenye upana wa futi mbili na nusu kulaliwa na watu wanne.

“Katika godoro la futi mbili na nusu tulikuwa tunalala watu wanne, tulikuwa tunalazimika kulala mtindo wa mchongoma yaani wawili wanalala wakiwa wameelekeza vichwa upande mmoja na wengine wawili wanaelekeza vichwa upande mwingine.

Mtindo huu wa kulala baadhi ya watu wanauita ‘mzungu wanne’ na mimi kwa kipindi chote cha miezi mitatu nilichokaa gerezani nilikuwa nalala mzungu wanne kama wengine,” anasimulia Sugu.

Anasema kutokana na hali duni ya malazi ya wafungwa ni rahisi kuambukizana maradhi hasa yanayoambukiza kupitia mfumo wa hewa kama kikohozi na kifua kikuu.

Chakula cha ubabe

Sugu anasema hali ya chakula kwa wafungwa ndani ya gereza hilo pia si nzuri, kwani wafungwa wanakula mlo mmoja tu kwa siku licha ya Serikali kusema inawatengea fedha za kutosha watu walio gerezani.

Anasema kulingana na tabia za gerezani, watu wengi hawawezi kula na kushiba kwani chakula kinagawiwa na kuliwa kwa ubabe mwingi ambapo wenye nguvu au madaraka ndani ya gereza ndio wenye uhakika wa kula chakula na kushiba.

“Wafungwa waliopewa cheo cha unyampala ndio wanaoweza kupata chakula cha kutosheleza matumbo yao, wengine huishia kula kwa kunyang’anyana na mwenye nguvu ndiye anayekula, kwa kifupi mle ndani utemi tu bila utemi mzee hupati chakula,” anasema Sugu.

Mavazi kwa wafungwa

Kwa mujibu wa Sugu, hali ya mavazi kwa wafungwa gerezani hapo si ya kuridhisha kwani licha ya Serikali kuamua wafungwa wote wavae sare zenye rangi ya njano, upatikanaji wake umekuwa ni mgumu hivyo kushindwa kukidhi mahitaji ya wafungwa.

Sugu anasema katika kundi la wafungwa wanaokadiriwa 800 ni wafungwa kama 200 tu ambao wanapata mavazi rasmi ya wafungwa kwa maana ya sare za rangi ya njano na wanaosalia takribani 600 wanalazimika kuvaa nguo zao za nyumbani.

Anasema ikitokea nguo za mfungwa zimechakaa, atalazimika kuzitumia hizo hizo na kuteseka kwa baridi kali hadi mwisho wa kifungo chake au labda itokee mfungwa mwenye mavazi rasmi amemaliza kifungo na kuvua nguo zake ndipo mwingine hupewa.

Akataa sare zilizotumika

Sugu anasema wakati yeye na mwenzake Katibu wa Chadema Kanda ya Nyasa, Emmanuel Masonga wanaingia gerezani hapo walikaa takribani wiki moja bila kuwa na sare, lakini aliambiwa kwamba kuna agizo kutoka ‘juu’ kwamba lazima wavae sare.

“Nilishangaa pale nilipopata taarifa kwamba kuna agizo kutoka juu likidai Sugu lazima avae sare. Lakini ukiangalia mle ndani kuna wafungwa wana zaidi ya miaka 10 hawana sare kwa sababu Serikali haijawashonea.

“Kwa sababu ya Sugu na Masonga tu zilitafutwa sare za zamani ambazo zilitumika wakatuletea ili tuvae….. tulizikataa na walipoona vile mzee unaambiwa walihaha kututafutia nyingine… wakatushonea mpya.

“Na nilishangaa kusikia hilo ni agizo toka juu… maana sikuona ajabu mfungwa Sugu kuvaa sare. Eti walitaka kumfedhehesha Sugu kisaikolojia. Kwangu niliona poa tu kwanza walinipunguzia kuvaa nguo za nyumbani na kuanza kufuafua mara kwa mara,” anasema Sugu.

Usikose kusoma mfululizo wa maisha ya Sugu gerezani kesho