Sumaye aunguruma Ukonga

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Frederick Sumaye, amesema serikali itatumia zaidi ya Sh 1bilioni hadi Sh 2 bilioni kwa ajili ya uchaguzi huu fedha ambazo ni kodi zetu.

 

BY Mwandishi Wetu, Mwananchi. mwananchipapers@mwananchi.co.tz

IN SUMMARY

Sumaye yupo kwenye kampeni za ubunge jimbo la Ukonga ambako anamnadi mgombea, Asia Msangi.  Uchaguzi utafanyika Septemba 16 mwaka huu.

Advertisement

Dar es Salaam. Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Frederick Sumaye, amesema serikali itatumia zaidi ya Sh 1bilioni hadi Sh 2 bilioni kwa ajili ya uchaguzi huu fedha ambazo ni kodi zetu.

 Uchaguzi mdogo wa majimbo mawili na kata 21 za udiwani unatarajia kufanyika Septemba 16 mwaka huu.

Akizungumza leo Septemba 12 katika kampeni za udiwani jimbo la Ukonga, Sumaye amesema kitendo cha Mwita(Mwita Waitara) kuja kuomba kura ni wazi amewadharau sana watu wa Ukonga

“Kuna wana CCM wako ndani ya chama zaidi ya miaka 10 na wangependa kugombea hiyo nafasi lakini amepewa Mwita. Huu ni ukandamizaji wa Demokrasia, yaani wameufanya nje sasa hivi umeingia ndani ya CCM,” amesema

Sumaye ambaye alikuwa akimnadi Asia Msangi anayewania ubunge jimbo la Ukonga, kupitia Chadema amesema ilidhaniwa wanaopata shida ni wapinzani lakini kwa sasa kila mtu anakiona cha moto.

“Nimekuwa Waziri Mkuu kwa miaka 10 hakuna aliyekaa muda wote huo, na inafahamika nilipokuwa kwenye nafasi hiyo maisha yalikuwaje. Tulisimamia kila kitu na maisha yakawa rahisi,” amesema.

Sumaye ambaye alikuwa Waziri Mkuu wakati wa serikali ya awamu ya tatu iliyoongozwa na Benjamin Mkapa amesema CCM sasa haitaki kuweka mambo sawa, haitaki ushindani na inatumia vyombo vya dola.

“Tunafahamu hiyo jumapili kuna mambo yatatokea hatutakubali. Tunataka wana CCM waelewe kuwa hizi kelele tunazopiga ni kwa ajili ya watanzania wote,” amesema na kuongeza:

“Unadhani mimi nilipungukiwa na akili nilivyotoka CCM kuja huku, niliona moto unaokuja mbele ya taifa hili ni lazima tuwe na vyama vya upinzani vyenye nguvu.”

Kadhalika Sumaye amesema kuna tetesi za watu kujaribu kumteka mgombea ubunge jimbo hilo kwa tiketi ya Chadema, (Asia Msangi)

“Kama kuna watu wana ujinga wa kutaka kumteka Asia Msangi nawaambia wakome, wakome, wakome na hawataweza,” amesema

Sumaye pia amesema iwapo  Chadema kitaingia madarakani kwa kipindi cha  miaka mitano au kumi na kikashindwa kubadilisha maisha ya watanzania, atakuwa wa kwanza kuwaambia wenzake wakae kando kupisha chama kingine.

More From Mwananchi
This page might use cookies if your analytics vendor requires them. Accept