TCRA yavionya vyombo vya habari vya mitandaoni

Muktasari:

TCRA imesema baadhi ya wamiliki wa mitandao hiyo wamekaidi kutiia agizo la kusajili mitandao hiyo na kuendelea kuchapisha habari mitandaoni.

Dodoma. Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imesema ipo mbioni kuwachukulia hatua za kisheria wamiliki wa mitandao ya kijamii ya 'blogs', tovuti, TV online ambao wanaendelea kuweka habari kwenye mitandao yao ilhali hawajasajiliwa kufanya kazi hiyo.

Akizungumza leo Septemba 11, 2018 jijini hapa wakati wa semina kwa wadau mbalimbali wa mawasiliano iliyoandaliwa na mamlaka hiyo, mhandisi wa TCRA Makao Makuu, Francis Mihayo amesema wapo baadhi ya wamiliki wa mitandao hiyo waliokaidi kutii agizo hilo watawakamata na kuwachukulia hatua za kisheria.

Amesema kuwa tangu muda wa kujisajili uliotolewa na mamlaka hiyo uishe baadhi ya wamiliki wameonekana kukaidi agizo hilo na kuendelea kuweka habari hizo kwa matakwa yao wenyewe bila kujali ni kinyume cha sheria.

“Wapo ambao bado wanaendelea kuweka habari, video na vitu vingine, ilihali hawajajisajili lakini niwaambie kuwa kufanya hivyo ni kinyume cha sheria, hivyo wakati ukifika tutawakamata kwa sasa tunawaangalia tu maana tunawaona wote na kile wanachokifanya,” amesema Mihayo.

Aprili mwaka huu TCRA iliwapa muda wa wiki mbili wamiliki wa mitandao ya kijamii ya 'blogs', tovuti na aina nyingine ya vyombo vya habari vinavyochapisha habari kwenye mtandao bila kujisajili.