TRA yagawa makontena ya RC Makonda kimyakimya

Muktasari:

Kamishna Mkuu wa TRA, Charles Kichere amesema tayari makontena 20 ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda yamekwishagawiwa, licha ya kueleza awali kwamba ingetangaza taasisi ambazo zingegawiwa.

Dar es Salaam. Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeyagawa ‘kimya kimya’ makontena 20 ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda yaliyokuwa yakishikiliwa na mamlaka hiyo.

Septemba 5, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa mamlaka hiyo, Richard Kayombo alieleza kuwa iwapo uamuzi wa kuyagawa makontena hayo utafanyika, taasisi zitakazogawiwa zitajulikana.

Hata hivyo, wakati ikisubiriwa kujulikana kwa taasisi hizo, Kamishna Mkuu wa TRA, Charles Kichere amesema tayari makontena yamekwishagawiwa.

Makontena hayo ambayo yalikosa wanunuzi katika minada yote mitatu iliyoendeshwa na kampuni ya udalali ya Yono yalikuwa na samani za viti, meza na mbao za kuandikia yakidaiwa kodi inayokadiriwa kufikia Sh1.2 bilioni.

Kamishna Mkuu wa TRA, Charles Kichere aliliambia Mwananchi jana kwamba makontena hayo tayari yamegawiwa.

Ingawa hakutaja ni watu gani au taasisi zipi zilizonufaika na mgawo huo, alisisitiza kuwa yalishagawiwa na angetoa taarifa zaidi baada ya kupokea orodha kutoka kwa wasaidizi wake.

“Siwezi kusema lini yaligawiwa wala ni kina nani waliopata mpaka nipate orodha kutoka kwa wasaidizi wangu wa forodha, maana hata sasa ninavyozungumza na wewe sipo ofisini... nadhani tukizungumza kesho (leo) nitaweza kukupatia orodha kamili ya wale waliogawiwa,” alisema.

Hivi karibuni kamishna huyo aliliambia Mwananchi kuwa TRA ilikuwa inakamilisha mchakato wa kuanza kuyagawa makontena hayo baada ya kukosekana wanunuzi.

Alisema sheria ya kodi ya forodha ya Afrika Mashariki inaelekeza kuwa mali zinazokosa mnunuzi zinawekewa utaratibu maalumu ikiwamo ule wa kugawiwa bure.

“Inapojitokeza minada yote hakuna mnunuzi aliyepatikana, kuna utaratibu ulioelekezwa kisheria wa kuziondoa mali hizo sehemu ya mnada na moja ya utaratibu huo ni kugawa bure,” alisema.

Hata hivyo, hakuwa tayari kutaja tarehe ya kuondolewa kwa makontena hayo mbali ya kusisitiza kuwa ofisi yake imeanza kutekeleza taratibu zinazotakiwa.

Alipoulizwa kwa nini makontena hayo yamekosa wateja katika minada yote, kamishna huyo hakuwa na jibu la moja kwa moja na badala yake alihoji, “Mimi sijui kwa nini, labda nikuulize wewe maana mnazunguka huku na kule unaweza kujua.”

Baadaye alipoambiwa huenda hali hiyo inatokana na kiwango kikubwa cha bei kilichowekwa ambacho kiliwahi kulalamikiwa na wanunuzi, Kichere alijibu, “Gharama au bei zinawekwa kisheria. Hizi bei hatuzipangi tu kienyeji, kuna vitu vingi vinaangaliwa kabla ya kuwekwa, mfano kuna gharama ya ardhi, gharama ya kuhifadhi mzigo na mengineyo. Hizi bei zipo kwa mujibu wa sheria.”

‘Sinema’ ya makontena hayo

Kwa mara ya kwanza makontena hayo yalianza kupigwa mnada Agosti 25, lakini yalikosa wanunuzi kutokana na wateja wengi kushindwa kufikia bei iliyotakiwa, baadhi yao wakitaja Sh10 milioni kwa kontena badala ya Sh60 milioni iliyotakiwa.

Baada ya makontena hayo kutouzika, Agosti 26, Makonda alitoa onyo akiwa mkoani Kagera kuwa mtu atakayeyanunua atalaaniwa yeye (mnunuzi) na uzao wake.

Agosti 27, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Phillip Mpango alikwenda bandarini kuyakagua na kuwataka viongozi wenzake serikalini kutathmini kauli zao akiwataka watu wanaotaka kununua samani hizo wasiogope.

Akizungumza na madiwani, viongozi na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato mkoani Geita Agosti 30, Rais John Magufuli alipigilia msumari sakata hilo akiwataka viongozi kuwatumikia wananchi bila kujali kuwa wako kwenye nafasi gani.

“Umesikia hili sakata la Dar es Salaam, eti mkuu wa mkoa ameleta makontena, ameambiwa alipe kodi, kwa nini asilipe kodi?” alihoji Rais Magufuli.

“...Sasa ukichukua makontena kule umezungumza na watu wengine labda na wafanyabiashara, unasema ni makontena yako halafu ukasema tena labda ni ya walimu, wala hata shule hazitajwi maana yake nini,” alihoji Rais.

Septemba Mosi ulifanyika mnada mwingine, lakini kwa mara nyingine makontena hayo hayakuuzika kutokana na wateja kushindwa kufikia bei iliyotajwa. Kadhalika Septemba 8 ulifanyika mnada mwingine bila mafanikio.