Tani 1.2 za samaki zakamatwa Kagera, zagawanywa kwa taasisi za Serikali, shule

Muktasari:

  • Operesheni ya kukamata wavuvi haramu imefanikiwa kukamata tani 1.2 za samaki mkoani Kagera ambazo zimegawanywa kwa taasisi za Serikali zikiwamo shule za sekondari

Bukoba. Idara ya uvuvi mkoani Kagera imekamata samaki aina ya sangara kiasi cha tani 1.2 wenye thamani ya Sh10.3 milioni ambao walipatikana kwa njia za  uvuvi haramu na walikuwa wakitoroshwa kwenda nchini Uganda.

Ofisa mwandamizi wa ulinzi wa rasilimali za uvuvi Kanda ya Ziwa, Didasi Magembe ametoa taarifa hiyo leo Ijumaa Novemba 9,2018 kwa waandishi wa habari katika viwanja vya ofisi za idara hiyo katika manispaa ya Bukoba mkoani humo.

Magembe amesema kati ya samaki hao wapo ambao wako chini ya sentimita 50 na wengine zaidi ya sentimita 85 wanaoruhusiwa kwa mujibu wa sheria na kwamba kiwango hicho kimegawiwa kwa taasisi mbalimbali zikiwemo baadhi ya shule za sekondari.

Amesema samaki hao wanavuliwa kwa kutumia zana za uvuvi haramu kama makokoro, timba, ndoano na mitumbwi au boti huku wanaohusika wakitumika usiku kuingia ndani ya Ziwa Victoria

"Tumejipanga kuhakikisha tunalinda rasilimali ndani ya ziwa kwa kufanya doria za mara kwa mara huku wanaotuhumiwa wakifikishwa mahakamani au kutozwa faini kwa mujibu wa sheria," amesema Magembe.

Aidha ofisa mwandamizi wa uvuvi mkoani Kagera, West Mbembati amesema katika kipindi cha kuanzia Oktoba 20 hadi jana Novemba 8, 2018 wamekamatwa wavuvi haramu 41 kati yao wanne wamefikishwa mahakamani na 37 wametozwa faini na kunyang’anywa zana zao.

Amesema vitendo vya uvuvi haramu vimeshamiri zaidi katika wilaya ya Muleba kata ya Nyakabango ambapo mkakati uliowekwa ni kuunda vikosi kazi katika mwambao wa ziwa na visiwani na kuzitaka kamati za ulinzi na usalama kusimamia kazi ya kutokomeza uvuvi haramu mkoani humo.