Tanzania katika ushiriki wa mtandao wa usambazaji umeme SADC

Wednesday August 14 2019

 

By Kelvin Matandiko, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imeweka wazi namna inavyoshiriki katika hatua za ufanikishaji wa malengo ya makubaliano ya kukuza uzalishaji, kujenga miundombinu na usambazaji wa nishati ya umeme katika nchi 15 za Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) wa ‘SADC Power Pool’.

Makubaliano hayo ni sehemu ya sekta tano zilizopo katika Idara ya Miundombinu inayotekeleza Mpango Kabambe wa Maendeleo ya Miundombinu katika mtangamano(RIDMP), utakaokoma 2027.   Sekta nyingine ni usafirishaji, Teknolojia ya habari na Mawasiliano(Tehama), vyanzo vya maji na hali ya hewa. 

Mpango huo unalenga kuanzisha mtandao wa upatikaji umeme wa uhakika, unaotabirika na unaopatikana kwa gharama nafuu ili kuchochea ukuaji wa sekta ya viwanda ndani ya jumuiya hiyo.

Akizungumza na wanahabari leo Agosti 14, 2019, Waziri wa Nishati, Dk Merdard Kalemani ametaja miradi miwili inayounganisha Tanzania na Nchi kadhaa za Jumuiya, ambayo iko katika utekelezaji.

“Tunayo miradi mikubwa miwili ya kushirikiana, kuna unao safirisha umeme 400KV kutoka Iringa, Mbeya hadi Malawi na Zambia, ujenzi umeshaanza hatua za juu kabisa na fedha zimepatikana kutoka Benki ya Dunia, makubaliano ya baadaye ni kuuziana umeme kulingana na mahitaji,” amesema Dk Kalemani.

“Mradi mwingine ni ule wa ZTK (Zambia, Tanzania na Kenya), unaosafirisha umeme wa 400KV kutoka Singida hadi Zambia upande wa kusini, na kwa upande wa kaskazini unasafirisha kutoka  Singida, Namanga, Arusha, hadi Kenya, hiyo ni miradi miwili mikubwa kwa SADC.

Advertisement

Aidha, mbali na miradi hiyo, Dk Kalemani amesema kukamilika kwa mradi wa uzalishaji umeme wa Julius Nyerere(JNHPP), katika Mto Rufuji utawezesha kuuza umeme nchi za Malawi, Malawi na DRC kongo.

Mipango ya kuzalisha

Kuhusu eneo la uzalishaji umeme kwa kutazama soko la Jumuiya hiyo, Dk Kalemani amesema Tanzania imeweka mikakati ya kutumia vyanzo vyake ili kuzalisha umeme  kwa lengo la kuchangia SADC.

Amesema Tanzania inatekeleza mkakati wa kufikia megawati 10,000 ifikapo mwaka 2025.

Amesema mpango huo uko katika malengo la Mpango wa SADC power pool, ikitumia umeme mchanganyiko kama vile nishati ya gesi asilia.

“Tuna megawati 884 zinazotokana na gesi ambayo kwa sasa imefikia futi za ujazo 57 trilioni , serikali imetenga futi za ujazo 8trilioni kuzalishia umeme. Tumeanza na mradi wa umeme wa JNHPP, kule mto Rufiji, utasaidia kupata umeme wa kutosha, unaotabirika, uhakika na gharama nafuu kwa SADC,” amesema.

Mipango ya kusambaza

Kuhusu usambazaji, tayari serikali ya Tanzania imeshaanza utekelezaji wa miradi ya kujenga miundombinu ya kusafirisha.

“kwa sasa tunajenga katika kona nne. Kuna kona ya kutoka Dar es Salaam hadi Kaskazini kupitia Segera, Tanga hadi Namanga. Kona ya pili ni kusafirisha umeme kutoka Iringa, Mbeya, Sumbawanga, Kigoma hadi Nyakanazi. Pia kuna kona nyingine ni kutoka Kigoma unapita Singida hadi Namanga.”

Advertisement