Tanzania kuanzisha idara ya kuimarisha fukwe

Muktasari:

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali inatarajia kuanzisha idara itakayoratibu na kuimarisha fukwe za bahari na maziwa ili kukuza utalii

Dar es Salaam. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali inatarajia kuanzisha idara itakayoratibu na kuimarisha fukwe za bahari na maziwa ili kukuza utalii.

Ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Oktoba 12, 2018 wakati akifungua maonyesho ya utalii ya ‘Swahili International Tourism Expo (SITE)’ yanaratibiwa na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB).

Majaliwa amesema  watalii wengi wanavutiwa na fukwe hizo na kwamba zinaweza kukuza uchumi wa nchi ikiwa zitakuwa na mamlaka inayozisimamia.

“Tunahitaji kuwa na ujenzi wa hoteli, vyakula na bidhaa nyingine za kuvutia utalii ili kukuza uchumi wetu,” amesema Majaliwa.

Awali, mtendaji mkuu wa TTB, Devotha Mdachi amesema zaidi ya kampuni 170 na mawakala wa utalii 300 kutoka nchi mbalimbali duniani wameshiriki kwenye maonyesho hayo.

“Hii ni fursa yetu katika kutangaza utalii wa ndani na washiriki wataweza kutengeneza mtandao mkubwa zaidi duniani kupitia maonyesho haya,” amesema.