Upelelezi kesi ya vigogo wa Six Telecoms, Dk Ringo Tenga wakamilika

Wednesday April 17 2019

 

By Pamela Chilongola, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Serikali imeiambia Mahakama ya Hakimu Kazi Kisutu kuwa upelelezi wa kesi inayowakabili vigogo wa Six Telecoms akiwamo wakili Dk Ringo Tenga umekamilika, hivyo wanaandaa taarifa kwenda Mahakama Kuu.

Mbali na Dk Tenga wengine ni Hafidhi Shamte au Rashid Shamte ambaye ni mkurugenzi mkuu wa kampuni hiyo; Peter Noni, Noel Chacha na Kampuni ya Six Telecoms.

Wakili wa Serikali, Simon Wankyo alidai leo Jumatano Aprili 17, 2019 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu,Thomas Simba, kuwa shauri hilo limekuja kwa ajili ya kutajwa na upelelezi umekamilika.

"Upelelezi umekamilika tunaandaa taarifa kwenda Mahakama Kuu hivyo tarehe inayokuja nitaieleza mahakama hii tumefikia wapi, naomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa,” alidai Wankyo.

Hakimu Simba alisema shauri hilo ni la muda mrefu hivyo aliutaka upande wa mashtaka ujitahidi kesi iweze kuendelea.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Aprili 30, 2019 itakapotajwa na washtakiwa wamerudishwa rumande.

Advertisement

Katika kesi ya msingi, Dk Tenga ambaye ni mkurugenzi na mwanasheria wa kampuni hiyo na wenzake wanadai  kati ya Januari mosi 2014 na Januari 14, 2016 maeneo ya Dar es Salaam, walitoza malipo ya mawasiliano ya simu za kimataifa chini ya kiwango cha Dola 0.25 za Marekani kwa dakika kwa lengo la kujipatia faida.

Pia, kipindi hicho wanadaiwa kuhujumu miundombinu ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa kutoza gharama chini ya kiwango na kushindwa kulipa Dola 3,282,741.12 kwa TCRA kama malipo ya mapato.

Washtakiwa hao wanadaiwa katika kipindi hicho walishindwa kulipa ada za udhibiti za Dola 466,010.07 kwa TCRA.

Katika shtaka la utakatishaji wa fedha; Hafidhi, Noni,Tenga na Chacha, wanadaiwa walitumia au walisimamia Dola 3,282,741.12 wakijua fedha hizo ni zao la makosa ya udanganyifu linalotokana na mashtaka yaliyotangulia.

Vilevile, washtakiwa hao wanadaiwa kuwa waliisababishia TCRA hasara ya Dola 3,748,751.22 (Sh8 bilioni).

Advertisement