Upepo wa Sugu wazidi kuitikisa CCM Mbeya

Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi

Muktasari:

Mbali na mbunge, pia halmashauri ya Jiji la Mbeya iko chini ya Chadema.


Mjini ni moja ya majimbo sita ya uchaguzi yaliyopo mkoani Mbeya. Ndio jimbo pekee kati ya saba linaloongozwa na mbunge wa upinzani Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ kutoka Chadema kwa vipindi viwili mfululizo na halmashauri yake kwa kipindi kimoja.

Majimbo mengine ni Kyela, Rungwe, Busokelo, Mbeya Vijijini, Mbarali na Chunya ambayo wabunge wake wanatokana na CCM.

Mbali na mbunge, pia halmashauri ya Jiji la Mbeya iko chini ya Chadema.

Hata hivyo, pamoja na CCM kushikilia majimbo mengi na halmashauri zake, bado inalimezea mate kwa kuwa ufalme wa mkoa huo umejikita katika jiji hilo, wakati yenyewe inashika majimbo ya pembezoni.

Hali hiyo inaonekana kuikwaza zaidi CCM na vigogo wake kukosa usingizi na sasa imeamua kulivaia njuga kupambana kwa udi na uvumba kuhakikisha inafanya mapinduzi makubwa ya kisiasa katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2020 ili iweze kuiweka Mbeya Mjini chini ya himaya yake.

Hali hiyo inabainishwa na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa CCM (NEC) , Dk Steven Mwakajumilo akianza na sababu za chama chake kupoteza jimbo hilo mara mbili mfululizo.

Mwakajumilo anayeuwakilisha mkoa wa Mbeya katika NEC, anasema mchawi mkubwa ni ubinafsi, tamaa, njaa na undumila wa baadhi ya viongozi ambao wamekuwa wakienda na majina ya wagombea wanaowahitaji kwenye vikao vya uteuzi badala ya kuwasilisha majina ya watu ambao ni chaguo la wanachama.

Anabainisha hayo wakati akifungua mafunzo ya ujasiriamali kwa jumuiya za CCM, za Vijana (UVCCM) na wanawake (UWT), ikiwa ni sehemu ya harakati za chama hicho kulikomboa jimbo la Mbeya Mjini.

“Ilifika mahala tukakubali kuingiliwa na wanasiasa uchwara wakaivuruga Mbeya na sisi tukakubali kuvurugwa…. Sasa kupitia safu hii ya uongozi wa sasa Mbeya Mjini itakuwa historia kwa kiongozi kubeba jina la mgombea.

“Na mimi nikiwa mjumbe wa kamati ya maadili ya CCM Mkoa na mjumbe wa halmashauri kuu ya Taifa, moja ya maazimio ya vikao vya chama ni kuwa kiongozi ambaye amechaguliwa na CCM atakuwa ametoka mikononi mwenu (wapiga kura),” anasema.

Anaongeza, “Nyinyi ndio mtakaosema tunamtaka fulani kwa mustakabali wa mkoa wa Mbeya na nchi yetu, lakini huyo mtu atokane na sifa zinazojitosheleza na si kwa kupita usiku kuwashawishi, si kwa kuja kujiuza bali hekima na busara zake kwa taifa zitamwongoza,” alisema Mwakajumilo.

Anasema kutokana na tabia za viongozi, baadhi ya wanasiasa uchwara walikuwa wakitoka maeneo mbalimbali nje ya jimbo la Mbeya Mjini na kuja kuwavuruga, hali ambayo ilisababisha jimbo hilo kuonekana kama jehanam ya kisiasa.

Mjumbe huyo wa NEC anasema katika kukabiliana na changamoto hiyo, CCM kupitia kwa mwenyekiti wake wa Taifa, Dk John Magufuli imefanya mabadiliko makubwa ya uongozi ndani ya chama sambamba na kubadilisha baadhi ya mifumo, hali ambayo anaamini itaondoa kabisa siasa za majitaka za wanasiasa uchwara wa Mbeya Mjini.

Mikakati

Alisema kuwa kutokana na mifumo ambayo imeasisiwa na Dk Magufuli, hivi sasa chama kimejipanga kuhakikisha wananchi wa Mbeya Mjini wanapata mgombea ambaye ni chaguo lao kwenye uchaguzi mkuu ujao ili kuhakikisha jimbo hilo linarejea CCM.

Anasema mikakati hiyo inapaswa kuanza mwakani kwenye chaguzi za Serikali za mitaa na anawataka viongozi wa CCM ngazi ya matawi kuhakikisha hawawapuuzi uchaguzi huio kwa kuwa ndio utakaotoa dira ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 kwa CCM kushinda, huku akisisitiza kuwa wananchi ndio wawe na sauti ya kumpata mgombea wanayemtaka.

Mapema Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Iringa ambaye alikuwa mkufunzi wa mafunzo hayo, Kenani Kihongosi anashindilia msumari kwenye ubionafsi.

Anasema upinzani wa Mbeya Mjini upo kutokana na ubinafsi, ukabila uliopo miongoni mwa wana CCM.

“Niwahakikishie CCM Mbeya Mjini, mkiachana na ukabila, ubinafsi, tamaa, hapa hakuna upinzani hapa,” anasema.

Ili kuondokana na hali hiyo, Katibu wa CCM, Mbeya Mjini, Gerald Mwadalu anasema ili kuhakikisha jimbo hilo linarudi mikononi mwake, wameanza kuendesha siasa ngazi ya shina ili kuwafikia wanachama.

Anasema “Siasa zetu tunaendesha kwa balozi, balozi tukiamini ana watu 50, tuna mabalozi 1,006 katika Jiji la Mbeya. hivyo tukisema watu 1006 mara 50 hizo ni kura za CCM, sasa hivi tukisema uchaguzi ufanyike, hatujarudisha jimbo la Mbeya mjini?” anahoji.

0756 059107