Viongozi wa dini watia neno utendaji wa Magufuli

Muktasari:

Hayo yalielezwa jana katika maombi maalum yaliyofanyika katika kongamano la Roho Mtakatifu linaloendelea katika kituo cha Sala cha Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam.


Viongozi wa dini na waumini wa Kanisa Katoliki wamesema kuwa kasi ya utendaji aliyonayo Rais John Magufuli itasaidia ukuaji wa uchumi wa viwanda.

Hayo yalielezwa jana katika maombi maalum yaliyofanyika katika kongamano la Roho Mtakatifu linaloendelea katika kituo cha Sala cha Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam.

Mwongozaji wa maombi hayo  Epimack Mbeteni alisema ipo imani kwa Mungu kuwa Tanzania itakuwa kwa kasi kiuchumi.

Kituo hicho kinasimamiwa na Parokia ya Manzese na kuendeshwa na mkondo wa Karismatiki Katoliki, Jimbo Kuu la Dar es Salaam.

Mbeteni alisema kasi ya utendaji kazi aliyoanza nayo Rais Magufuli, inadhihirisha wazi kuwa malengo ya kuifikisha Tanzania katika uchumi mkubwa wa viwanda yatafikiwa ikiwa Mungu atapewa nafasi ya kwanza katika kuwezesha hilo.

"Tangu Rais wa awamu hii ameingia madarakani tunaona kasi ya ajabu aliyoanza nayo. Hii inadhihirisha kuwa viwanda vilivyokufa na kugeuka magofu vinakwenda kufufuliwa na vijana wanaotembea na vyeti bila ajira, wanakwenda kupata ajira," alisema Mbeteni wakati akiongoza maombi hayo.

Mgeni rasmi katika maombi hayo, Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Annastazia Wambura, alisema maombi pekee ndiyo yanayoweza kuendelea kuiweka nchi salama na kuepusha vurugu zozote.