Viwanda vilivyobinafsishwa kufanyiwa tathmini

Friday July 28 2017
VIWANDA PICHA

Dar es Salaam. Msajili wa Hazina, Dk Oswald Mashindano amesema ofisi hiyo imeunda kamati ya watalaam 24 ambao  watazunguka nchi nzima kufanya tathmini ya kina kwa viwanda vilivyobinafsishwa na kutoa mapendekezo kwa Serikali.

Amesema tayari mpango kazi umekamilika na kamati hiyo itaanza kazi baada ya mkutano wa kesho na makatibu wakuu wa wizara.

Kauli hiyo ameitoa jana Alhamisi Julai 27 saa 4:00 usiku kupitia kipindi cha Tunatekeleza, kinachorushwa na Shirika la Utangazaji la Taifa(TBC1).

Amesema leo wajumbe hao watakuwa katika mkutano wa mafunzo maalumu na makatibu wakuu na wadau mbalimbali ili kufahamu mambo ya msingi yanayohitajika na matatajio ya Serikali kutoka kwao.

"Watagawanywa makundi sita, si wote waende kama kundi moja, watajigawa maeneo mbalimbali na watakamilisha kazi hiyo ndani ya miezi miwili tu," amesema Dk Mashindano.

Dk Mashindano amesema wajumbe wa kamati hiyo wametoka sekta mbalimbali wakiwamo sita kutoka Hazina. Wengine

Advertisement

wametoka ofisi za Waziri Mkuu, Mwanasheria Mkuu wa Serikali(AG) na Wizara ya Fedha na Mipango.

Dk Mashindano amesema hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa agizo la Rais John Magufuli alipoagiza viwanda vyote vilivyobinafsishwa lazima vianze kufanya kazi.

"Tunafanya hivyo kwa sababu; kwanza ni makubaliano ya kimkataba na Serikali lazima ifanye kazi, pili ni utekelezaji wa safari ya kuelekea uchumi wa viwanda,"amesema.

Advertisement