Viwanda vya sukari hatarini kufungwa Tanzania

Meneja uendeshaji wa viwanda vya Kagera na Mtibwa, Abel Magese alipozungumza na Mwananchi wiki hii alisema soko limekuwa gumu kutokana na sukari kutoka nje ya nchi kuingizwa kwa njia za panya.

 

BY Waandishi Wetu, Mwananchi mwananchipapers@mwananchi.co.tz

IN SUMMARY

Meneja uendeshaji wa viwanda vya Kagera na Mtibwa, Abel Magese alipozungumza na Mwananchi wiki hii alisema soko limekuwa gumu kutokana na sukari kutoka nje ya nchi kuingizwa kwa njia za panya.


Advertisement

Dar/mikoani. Endapo Serikali haitadhibiti biashara ya magendo ya sukari, viwanda vya Kagera na Mtibwa vimesema vitalazimika kusitisha uzalishaji.

Hatua hiyo inatokana na viwanda hivyo kuwa na shehena kubwa ya sukari iliyozalishwa ambayo inakosa soko, jambo linalohatarisha operesheni zao na kutishia ajira za maelfu ya wafanyakazi iwapo vitafungwa.

Meneja uendeshaji wa viwanda vya Kagera na Mtibwa, Abel Magese alipozungumza na Mwananchi wiki hii alisema soko limekuwa gumu kutokana na sukari kutoka nje ya nchi kuingizwa kwa njia za panya.

“Tatizo ni kubwa, sukari inayoingizwa nchini isivyo halali kuendelea kuzagaa mitaani bila udhibiti ndiyo sababu (ya kuathiri soko letu),” alisema Magese.

Novemba 2017, Rais John Magufuli alibatilisha utaratibu wa utoaji wa vibali vya kuagiza sukari kutoka nje akitaka kulinda viwanda vya ndani.

Rais alimwagiza Waziri wa Kilimo kuivunja menejimenti ya Bodi ya Sukari na kuwapangia watendaji wake kazi nyingine.

Alichukua uamuzi huo ukiwa ni mwaka mmoja tangu alipozuia uagizaji wa sukari isipokuwa kwa kibali maalumu. Kwenye mabadiliko hayo, Rais aliagiza wazalishaji wapewe vibali vya kuagiza bidhaa hiyo kutoka nje.

Baada ya njia hizo halali kubanwa, baadhi ya wafanyabiashara wanaendelea kuagiza bidhaa hiyo bila kufuata utaratibu uliopo, hivyo kuviumiza viwanda vya ndani.

Mwezi Julai, Waziri wa Kilimo, Dk Charles Tizeba alifanya ziara katika maduka makubwa ya kuuzia sukari na mchele na kubaini uingizaji wa bidhaa hiyo kinyume cha utaratibu kisha akaagiza kuchukuliwa hatua kwa waliohusika.

Hata hivyo, Magesse anasema hadi wiki iliyopita Kiwanda cha Sukari Kagera kilikuwa na tani 13,000 iliyozalishwa, hivyo kuyaelemea maghala yaliyopo kwasababu kila siku uzalishaji unaongezeka na sasa inahifadhiwa hadi nje.

“Mtibwa nako hali ni hiyo hiyo. Kama itaendelea hivi, itahatarisha uzalishaji na tunaweza kuusimamisha.”

Bei elekezi ya Serikali

Wakati shehena hiyo ikikwama kwenye viwanda hivyo kwa kukosa wateja, bei elekezi iliyotangazwa na Bodi ya Sukari Tanzania mwaka 2016 ya kilo moja kuuzwa Sh1,800, imeshindwa kutekelezwa.

Uchunguzi wa Mwananchi uliofanywa katika mikoa mbalimbali umebaini kilo hiyo inauzwa kati ya Sh2,500 hadi Sh3,000.

Jijini Arusha kilo moja inauzwa kati ya Sh2,500 hadi Sh2,700 wakati Kigoma na Kagera ikiuzwa kati ya Sh2,800 hadi Sh3,000 na Dar es Salaam Sh2,500.

Meneja huyo alisema kusimamishwa kwa uzalishaji katika viwanda hivyo kunahatarisha ajira kwa zaidi ya wafanyakazi 10,000 kwasababu Kagera wapo takriban 6,000 na Mtibwa 4,000.

Kukabiliana na changamoto iliyopo, alisema wamewasiliana na Bodi ya Sukari, Wizara ya Kilimo na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kuishughulikia, lakini mpaka hakuna suluhu iliyopatikana.

Licha ya changamoto hiyo, Magesse alisema, “mikakati yetu ni kutosheleza soko la ndani, wanaoingiza kwa njia zao ndiyo wanaharibu soko letu kwa sababu wao wanauza kwa bei ya chini.”

Alisema ingawa Serikali imefanya juhudi kubwa kudhibiti vibali vya uingizaji wa bidhaa hiyo kwa matumizi ya viwandani na majumbani, kuna wachache wanatumia mianya isiyojulikana kuiingiza.

“Hatujui nani anaingiza ila ukienda sokoni unaikuta hiyo sukari,” alisema.

Waziri Mwijage

Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage alipotafutwa kuzungumzia suala hilo alisema amesikia kuna barua ofisini kwake Dodoma na kwamba, akifika na kuiona ataifanyia kazi.

“Nipo Dar es Salaam, nikifika Dodoma nitaona malalamiko yao na kuyashughulikia kama kuna mtu wanamtuhumu nitashughulika naye,” alisema waziri huyo.

Kilio cha viwanda hivyo kinakuja siku chache baada ya viwanda vinavyotumia sukari kwenye uzalishaji kukabiliwa na uhaba wa malighafi hiyo.

Mshauri wa Sera wa Shirikisho la wenye Viwanda Tanzania (CTI), Akida Mnyenyelwa alisema zamani Serikali ilikuwa inaamini wanaoingiza sukari ya viwandani wanaiingiza sokoni na kuiuza kwa ajili ya matumizi ya nyumbani.

“Tukio la juzi la waziri kukamata sukari ya magendo ni ushahidi kwamba kuna mianya ya kukiuka sheria. Limedhihirisha ujanja unaofanywa, uingizaji wa sukari ya viwandani hivi sasa umedhibitiwa sana,” alisema Mnyenyelwa.


More From Mwananchi
This page might use cookies if your analytics vendor requires them. Accept