Vodacom yaendelea kupambana ajira ya bosi wake mpya

Mkuu wa Mawasiliano na Uhusiano wa Vodacom, Jacquiline Materu


Muktasari:

Akifafanua zaidi kuhusu utaratibu wa kutoa vibali vya wageni kufanya kazi nchini, Mavunde alisema waombaji wakishakamilisha utaratibu wote hupata ndani ya siku 14.

Dar es Salaam. Wakati kampuni ya Mawasiliano ya Vodacom ikimteua Hisham Hendi kukaimu nafasi ya mkurugenzi mtendaji, imesema inaendelea kufuatilia ajira ya bosi wake mpya, Sylvia Mulinge ambaye mpaka sasa hajapata kibali cha ajira kutoka serikalini.

Hendi mwenye uzoefu wa miaka 15 ya biashara za mawasiliano, alijiunga na Vodacom mwaka 2016 akishika nafasi za juu katika kampuni za Vodafone na Vodacom.

Kwa sasa anashika nafasi hiyo ikiwa imepita miezi minne tangu aliyekuwa mkurugenzi mtendaji wa kampuni hiyo, Ian Ferrao kustaafu, huku kampuni hiyo ikimteua Mulinge kurithi nafasi hiyo.

Hata hivyo, uliibuka utata katika taratibu za Uhamiaji na Idara ya Kazi nchini, jambo lililosababisha Mulinge aliyetakiwa kukabidhiwa ofisi Agosti 31 kushindikana.

Akizungumza na Mwananchi jana, mkuu wa Mawasiliano na Uhusiano wa Vodacom, Jacquiline Materu alisema bado wanafuatilia ajira ya Mulinge ndiyo maana Hendi anakaimu nafasi hiyo. “Bado tunafuatilia ajira ya Mulinge, ndiyo maana Hendi anakaimu. Ungewauliza Serikali wenyewe wamefikia wapi,” alisema Materu.

Hivi karibuni, naibu waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi na Ajira), Anthony Mavunde alizungumzia kuchelewa kwa ajira ya mkurugenzi huyo tangu alipoteuliwa Aprili, akisema Serikali inalifanyia kazi suala hilo.

Akizungumza katika mahojiano na Mwananchi alipotembelea ofisi za gazeti hili zilizopo Tabata Relini jijini Dar es Salaam, alisema suala hilo wameiambia hata kampuni ya Vodacom kinachoendelea.

“Katika taratibu hizo niweke wazi kwamba uzuri ni hata wahusika wenyewe walihusishwa yaani Vodacom,” alisema Mavunde.

Akifafanua zaidi kuhusu utaratibu wa kutoa vibali vya wageni kufanya kazi nchini, Mavunde alisema waombaji wakishakamilisha utaratibu wote hupata ndani ya siku 14.

“Katika mfumo wa utoaji wa vibali vya kazi, kwa sasa tumeweka utaratibu mzuri kabisa ambao mtu yeyote akikidhi mahitaji ya kinachopaswa kuwasilishwa, kibali hakiwezi kuchelewa kwa siku 14, kupata majibu kama umekubaliwa au umekataliwa,” alisema Mavunde.