VIDEO: Wachimbaji wadogo walalamikia zuio kuingia ukuta wa Tanzanite

Baadhi ya wachimbaji wa madini ya Tanzanite wa Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, wakiwa nje ya lango baada ya kuzuiwa kuingia ndani ya ukuta unaozunguka migodi hiyo. Picha na Joseph Lyimo

Muktasari:

  • Ukuta kuzunguka mgodi wa Tanzanite ulijengwa kwa ajili ya kuimarisha ulinzi wa madini hayo yanayopatikana Tanzania pekee.

Mirerani. Wachimbaji wadogo wa madini ya Tanzanite (WanaApolo) wa Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, wamezuiwa kuingia ndani ya ukuta unaozunguka migodi ya madini ya Tanzanite hadi waonyeshe mikataba ya kazi baina yao na wamiliki wa migodi yao.

Kutokana na hali hiyo wamemuomba Rais John Magufuli kuingilia kati suala la wao kuzuiwa kuingia ndani ya ukuta unaozunguka migodi ya madini hayo hadi wawe na vitambulisho vitatu ambavyo hawana.

Wakizungumza na Mwananchi Digital Septemba 12 wachimbaji hao wamedai kuwa hali ya maisha yao na mji huo kwa ujumla yamekuwa magumu kwani eneo hilo halina shamba zaidi ya kutegemea madini hayo.

Mmoja kati ya wachimbaji wadogo wa eneo hilo, Jabir Ramadhan amesema wamezuiwa kuingia ndani ya ukuta huo baada ya kutakiwa kuonyesha mikataba baina yao na wamiliki wa migodi wanayofanyia kazi ambayo hawana.

Ramadhan amesema baada ya kufika kwenye lango la kuingia ndani ya ukuta unaozunguka migodi hiyo, askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ambaye ana nyota tatu mabegani aliwazuia kwa kuwataka waonyeshe vitambulisho vitatu ili waingie.

Amesema wanatakiwa uwe na kitambulisho cha uraia(Nida), kitambulisho cha eneo tengefu la Mirerani (Mirerani Controlled Area) na mkataba wa kufanya kazi wa mchimbaji na mmiliki wa mgodi ndiyo unaweza kuruhusiwa kuingia ndani.

"Tunamuomba Rais Magufuli aingilie hili kwani hivi sasa kuna ukuta madini hayaibiwi tena, tunataka kufanya kazi hali yetu ni ngumu hatuna mashamba watoto wanatutegemea maisha ni magumu Mirerani," amesema Ramadhan.

Amesema suala la wamiliki wa migodi ya madini ya Tanzanite kuwalipa mishahara wachimbaji wadogo halitawezekana zaidi ya makubaliano ya kulipana asilimia 10 pindi uzalishaji utakapofanyika.

Mwenyekiti wa chama cha wachimbaji madini mkoa wa Manyara, Sadiki Mneney amesema anaomba Rais Magufuli aingilie kati tatizo hilo kwani wakati anazindua rasmi ukuta huo April 6 mwaka huu alisema utakuwa na manufaa makubwa kwa wachimbaji na serikali lakini imekuwa tofauti.

Mneney amesema wananchi wadogo na wamiliki wa migodi wameshaingia mkataba wa kulipana asilimia 10 pindi uzalishaji unapofanyika lakini bado wanakatazwa kuingia.

"Mtu ambaye ataweza kutatua tatizo hilo kwa sasa ni Rais Magufuli kwani awali suala la mitobozano na mipaka kwa wachimbaji wadogo ni yeye alilimaliza na hili tunaomba alimalize," amesema Mneney.

Hata hivyo, Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro mhandisi Zephania Chaula akizungumza kwa njia ya simu amesema serikali inatekeleza maagizo iliyotoa kwa wachimbaji hao hivyo wafuate hilo.

Mhandisi Chaula amesema kwenye ukuta huo kuna tangazo linawaonyesha wataruhusiwa kuingia hadi wadi wawe na mikataba ya kazi tangu Septemba 8 lakini zoezi rasmi limeanza leo jumatano ya Septemba 12 hivyo watekeleze hilo.