Wachumi washauri uboreshaji mazingira ya biashara kuongeza vyanzo vya mapato

Muktasari:

  • Ushauri huo umetolewa baada ya takwimu kuonyesha makusanyo ya Serikali yamepungua kwa asilimia 10.78 kwa miezi 10 ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka huu wa fedha 2017/18.

Dar es Salaam. Wataalamu wa uchumi wamependekeza kuimarishwa kwa vyanzo vya mapato ya Serikali ili kufanikisha utekelezaji wa bajeti.

Ushauri huo umetolewa baada ya takwimu kuonyesha makusanyo ya Serikali yamepungua kwa asilimia 10.78 kwa miezi 10 ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka huu wa fedha 2017/18.

Kuondoa nakisi hiyo ya mapato, wataalamu hao wamependekeza kuboreshwa kwa mazingira ya ufanyaji biashara ili kuongeza vyanzo vya mapato hayo kwa mwaka ujao wa fedha 2018/19, unaotarajiwa kuanza kutekelezwa Julai Mosi.

Bajeti mpya ikitarajiwa kusoma Alhamisi hii umuhimu wa kuchukua hatua mapema umependekezwa ili kupunguza mzigo kwa walipaji kodi wachache waliopo sasa.

Mkurugenzi wa mipango na utafiti wa Taasisi ya Repoa, Dk Abel Kinyondo alisema Serikali inapaswa kuboresha mazingira ya biashara kwa kupunguza ukubwa na wingi wa kodi zinazotozwa kwa wawekezaji na wafanyabiashara waliopo ili kuwashawishi wengi zaidi kuwekeza nchini.

“Kuendelea kuwatoza kodi wajasiriamali wachache waliosajili biashara zao, mwisho wa siku kunaweza kuwatisha wawekezaji wanaotaka kuwekeza. Tunapaswa kuachana na mfumo wa kuwa na kodi zinazoongezeka, sasa zianze kushuka,” alisema.

Kufanikisha hilo, alisema mazingira rafiki yanahitajika ili kujenga imani kwa wawekezaji watakaochangia ongezeko la ajira, uwekezaji hivyo kuongeza vyanzo vya mapato. Kwa mazingira yaliyopo, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imekuwa ikitekeleza mikakati kadhaa kuhakikisha inaongeza wigo wa makusanyo ya mapato.

Miongoni mwa mengi yanayofanywa ni usajili wa wafanyabiashara walio nje ya mfumo rasmi wakiwamo wamachinga, wachimbaji wadogo wa madini na mama lishe.

Mkurugenzi wa Elimu ya Mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo amewahi kukaririwa akisema mpango uliopo ni kuwasajili walau wafanyabiashara wadogo milioni moja mpaka mwishoni mwa mwezi huu.

Takwimu zilizopo zinaonyesha kuna walipakodi milioni 2.615 ambao wanachangia bajeti ya Serikali suala linalosisitizwa kuwa ipo haja ya kuongeza idadi hiyo.

Akiwasilisha bajeti ya Wizara ya Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alisema TRA ilikusanya Sh4.9 trilioni kutoka kwa walipaji kodi wakubwa nchini ikilinganishwa na Sh5.4 trilioni zilizokadiriwa.

Makusanyo hayo yalikuwa sawa na ongezeko la asilimia 7.09 yakilinganishwa na Sh4.5 trilioni za mwaka wa fedha uliopita. Ongezeko hilo lilitokana na ufanisi wa TRA na ushawishi wa viongozi mbalimbali wa Serikali na utii wa walipakodi.

Hata hivyo, makusanyo ya mamlaka hiyo kwa miezi 10 ya mwaka huu wa bajeti haukufikia malengo jambo ambalo wadau wanaamini linahitaji kufanyiwa tathmini na kuboresha mipango iliyopo ili kuongeza uwekezaji na kuzilinda biashara zilizopo.

Mhadhiri mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Delphin Rwegasira alisema mipango zaidi inahitajika kuvutia uwekezaji ili kupunguza mzigo walionao wafanyabiashara na wafanyakazi wachache waliopo. “Kila Mtanzania anapaswa kujumuishwa kwenye kodi. Utayari wa kisiasa ni muhimu pia katika mkakati wa kukuza mapato. Kwenye mapato ya ndani, wafanyakazi wa sekta rasmi pekee wamekuwa wakihusika kulipa kodi,” alisema Profesa Rwegasira.

Alisema zipo kampuni nyingi na watu wengi ambao hawafikiwi na TRA hivyo kutolipa kodi kama inavyotakiwa jambo linalohitaji kufanyiwa kazi.

Kwenye bajeti ya mwaka 2017/18, TRA ilitakiwa kukusanya Sh17.1 trilioni kufanikisha utekelezaji wa Sh31.7 trilioni zilizopangwa kukusanywa na kutumika mwaka huo.

Lakini, kwa miezi 10 ya utekelezaji wake, mamlaka hiyo haikufanikiwa kukusanya kiasi kilichotarajiwa kwa asilimia 11.2. Katika kipindi hicho, TRA ilitakiwa kukusanya Sh14.2 trilioni.

Kwa miezi hiyo 10, TRA ilikusanya Sh12.6 trilioni ambazo ni sawa na ongezeko la asilimia 8.3 zikilinganishwa na zilizokusanywa mwaka uliopita. Hii inamaanisha TRA ilikusanya wastani wa Sh1.26 trilioni kila mwezi.

Kufikia lengo la makusanyo ya Sh17.1 trilioni kwa mwaka huu wa fedha, mamlaka hiyo itapaswa kukusanya Sh4.5 trilioni kwa miezi miwili iliyobaki ya Mei na Juni jambo ambalo ni gumu likilinganishwa na mwenendo uliokuwapo.