UCHOKOZI WA EDO: Wafanyabiashara wamesawazisha dakika za majeruhi

Tuesday June 11 2019Edo  Kumwembe

Edo  Kumwembe 

Jinsi maisha yanavyokwenda kasi. Yana ajabu yake. Hii nchi kutesa kwa zamu. Rafiki zangu wakusanya ushuru nadhani wamerudi kuishi maisha ya Biblia. Hawa jamaa tunaambiwa walikuwa na matatizo na jamii tangu enzi hizo za zamani. Wanapitia mkondo wa tabu.

Namba Moja amewageuka. Tangu utawala huu uingie walikuwa wanaishi maisha ya raha sana. Walikuwa wanatembea salama katika kivuli kinachoitwa mtazamo chanya dhidi yao kutoka kwa Namba Moja. Tumeishia darasa la saba lakini wanaojua kiingereza wakipita maskani kwetu wanasema ‘Good perception’.

Dakika za mwanzo za kipindi cha kwanza lilikuwa bao la kisigino kutoka kwa watoza ushuru kwenda kwa wafanyabiashara. Vifua vilivyojazwa hofu ni rahisi kuvitengenezea mazingira ya ‘kufanya maongezi pembeni’. Wakati Namba Moja akiwakingia kifua ndugu zetu watoza ushuru, wao walikuwa wananufaika kwa namna moja au nyingine.

Hili ni jambo lililosumbua Wafanyabiashara wengi. Namba Moja alikuwa hajui tu kwamba mtazamo wake chanya uliopitiliza kwa watoza ushuru ulikuwa umefungua mianya mingi ya rushwa. Mtu unaambiwa tu “usipolipa tutaona”. Mfanyabiashara anakuwa mdogo kwa sababu mbele ya macho ya Namba Moja, siku zote yeye ni mwizi na mkwepa kodi.

Siku za karibuni, hasa Ijumaa iliyopita, hatimaye wafanyabiashara wakafunga bao la kusawazisha pale Magogoni. Mtazamo chanya wa Namba Moja umehama. Kutoka kwa watoza ushuru kwenda kwa wafanyabiashara. Hili ndio bao la kusawazisha kwao.

Bao la wafanyabiashara linakuja na maneno mengi ya chinichini. Wengine wanasema “mambo hayaendi”. Wengine wanasema “uchaguzi umekaribia”. Ilimradi tu kila mtu ni mchambuzi ndani ya daladala au maskani za kucheza drafti.

Mwishowe tunataka kuona nani atafunga bao la pili. Kwa sasa kuelekea kukamilika kwa kipindi cha kwanza cha Namba Moja ngoma ni droo. Wale walitesa dakika za mwanzo, hawa wanatesa dakika za mwisho. Mtoza ushuru mkuu mwingine, Zakayo, amebadilishwa.

Kama akifanya mambo mazuri basi wafanyabiashara wanaweza kupiga bao la pili huku wakisema “Si unaona! Umeleta mtu mwafaka”. Kama na yeye akifeli ghafla, basi watoza ushuru wanaweza kushinda na kusema “tatizo sio sisi, ni mfumo na wafanyabiashara”.

Advertisement