Wakazi waingiwa hofu mauaji ya kupiga nondo

Muktasari:

Wanane wauawa Desemba hadi Januari; polisi, uongozi wa mitaa ‘waingia kazini’

 Hofu ya kiusalama imewakumba wakazi wa kata za Nyegezi na Mkolani jijini Mwanza baada ya kuibuka kwa matukio ya watu kuvamiwa njiani na majumbani, kushambuliwa kwa kupigwa nondo au kukatwa na vitu vyenye ncha kali, kuporwa na wengine kuuawa.

Kati ya Desemba 2017 hadi Januari 2018, matukio manane ya watu kuvamiwa, kushambuliwa na kuuawa yameripotiwa katika kata hizo mbili zinazounda kata 18 za Jiji la Mwanza.

Bila kutaja idadi ya vifo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi anasema tayari wameyadhibiti makundi anayoitwa ya vibaka yanayohusishwa na matukio ya uhalifu si kwenye kata za Nyegezi na Mkolani pekee, bali maeneo mengine jijini humo hasa kipindi cha mwishoni na mwanzoni mwa mwaka.

“Ni matukio ya kawaida tu ya kihalifu ya vibaka, wananchi wasiwe na hofu kwa sababu tumechukua hatua kuvidhibiti (vikundi),” anasema Kamanda Msangi.

Kiongozi huyo wa polisi mkoa anakiri kupokea taarifa ya mfanyabiashara wa miamala ya fedha kwa njia ya mitandao ya simu eneo la Nyegezi ambaye hakumtaja jina kuuawa kwa kupigwa nondo na kukatwa na kitu chenye ncha kali.

Tukio hilo ni miongoni mwa matukio manane yanayotajwa na Mtendaji wa Kata ya Mkolani, Godfrey Mwegomba na wenyeviti wa mitaa katika kata hiyo na ile ya jirani ya Nyegezi.

Akizungumza wakati wa mahojiano maalumu ofisini kwake mwishoni mwa wiki, Mwegomba ambaye ndiye mlinzi wa amani Kata ya Mkolani anasema wananchi wameingiwa na hofu baada ya watu wawili kuuawa kwa kupigwa nondo huku wengine saba wakijeruhiwa ndani ya miezi miwili ya Desemba hadi Januari.

“Tumeanzisha ulinzi shirikishi na tayari tumefanikiwa kuwatia mbaroni watu 10 na kuwakabidhi polisi kwa mahojiano kuhusiana na matukio ya uhalifu mitaani,” anasema Mwegomba.

Anaitaja mitaa ya Kasese, Mkolani na Ibanda kuwa ndio imeshuhudia idadi kubwa ya matukio ya uhalifu kwa kipindi hicho. Kata ya Mkolani yenye wakazi zaidi ya 32,199 kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012, ina jumla ya mitaa 10.

Wenyeviti wa mitaa

Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika maeneo yao, wenyeviti wa mitaa ya Majengo Mapaya katika kata hiyo na wenzao wa Nchenga na Nyabulogoya, Kata ya Nyegezi wamesema wanashirikiana na polisi kuimarisha doria mitaani nyakati za usiku ili kukabiliana na makundi ya vijana wanaowavamia wananchi na kuwashambulia kwa kuwapiga nondo na kuwakata mapanga.

Mitaa Majengo Mapya, Nchenga na Nyabulogoya inapakana na Stendi Kuu ya Mabasi ya Nyegezi.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Majengo Mapya, Hezron Shiganza anasema kati ya Desemba hadi Januari, waendesha pikipiki wawili mtaani kwake wameuawa kwa kupigwa nondo na watu waliowakodisha ambao pia walitokomea na pikipiki zao.

“Baadhi ya matukio yametokea mapema saa moja jioni jambo linalozua hofu miongoni mwa wananchi,” anasema Shiganza.

Kauli hiyo inaungwa mkono na Mwenyekiti wa Mtaa wa Nchenga, Paschal Joseph ambaye eneo lake limeshuhudia vifo vitatu, kimoja cha mfanyabiashara wa miamala ya fedha kwa njia ya mtandao kuuawa kwa kukatwa mapanga na viwili vya wanaotuhumiwa kuwa vibaka kupigwa, kuuawa na kuchomwa moto na watu wenye hasira.

“Mauaji ya mfanyabiashara huyo yaliyotokea umbali wa mita 200 tu kutoka nyumbani kwake yana dalili za kisasi kwa sababu wauaji hawakuchukua chochote,” anasema Joseph.

Anasema tukio la wananchi kumchoma moto mtu aliyetuhumiwa kupora simu ya kiganjani na mkoba wa mpitanjia lilitokea Januari 15. Mwenyekiti wa Mtaa wa Nyabulogoya, Stephen Ntilibiza anasema katika mtaa jirani wa Califonia, kulitokea kifo cha mtu mmoja ambaye mwili wake uliokotwa ukiwa na majeraha yaliyotokana na kitu chenye ncha kali.

“Uchunguzi wa awali unaonyesha wahusika wa matukio haya ni vijana waliokuwa wakipiga debe katika Stendi Kuu ya Nyegezi ambao wameondolewa katika operesheni inayoendelea ya kudhibiti wezi na wanaobughudhi abiria,” anasema Ntilibiza.

Uongozi wa stendi kuu

Akizungumzia ongezeko la vitendo vya uhalifu kuhusishwa na kuondolewa kwa wapiga debe, Mwenyekiti wa Kituo cha Mabasi Nyegezi, Peter Maroro anasema uwezekano huo upo kwa sababu miongoni mwa walioondolewa, wamo waliokubuhu kwa unywaji wa pombe ambao walikuwa wakituhumiwa kuwaibia na kudokoa mali na fedha za abiria.

“Baada ya kuwaondoa, malalamiko ya abiria na wafanyabiashara kuibiwa eneo la stendi yamepungua, hii inadhihirisha miongoni mwao walikuwemo wahalifu.