Walioiba gari Dar wakamatwa Mwanza

Muktasari:

Gari liliibwa mwezi uliopita maeneo ya Kimara na baadaye ili bainika kwamba walioliiba wamekimbilia Mwanza


Mwanza. Jeshi la Polisi mkoani Mwanza limewakamata watu wawili  kwa kosa la kuiba gari aina ya Hino mali ya kampuni ya Sonu Esat Africa Ltd ya jijini Dar es Salaam.

Taarifa iliyotolewa leo na Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza, Jonathan Shanna imeeleza kuwa majambazi hao, mmoja mkazi wa Kimara jijini Dar es Salam na mwingine mkazi wa Kishiri jijini Mwanza walikamatwa Oktoba 11 saa 11:00 jioni katika mtaa wa Kishiri –Igoma jijini Mwanza.

“Watuhumiwa hao walikamatwa jana baada ya kupatikana kwa taarifa za kiintelejensia kwamba wameingia mkoani hapa wakiwa na gari ambalo wameliiba  Dar es Salaam, baada ya taarifa hizo polisi walianza kufuatilia na kufanikiwa kukamata wezi hao wakiwa na gari hilo,” amesema Shanna.

Amesema gari hilo liliibwa mwezi uliopita katika maeneo ya Kimara jijini Dar es Salaam na Septemba 25 kulifunguliwa jalada katika Kituo cha Polisi Kimara na kuanza kufanyika ufuatiliaji wa haraka ambapo baadaye ilibainika wezi hao wamekimbilia jijini Mwanza.

Amesema watuhumiwa hao baada ya kufika Mwanza walifuta majina ya ruti ya gari hiyo ambayo ilikuwa imeandikwa Mbezi – Makumbusho.

“Walilipeleka kwenye gereji mbili mjini Mwanza kwa ajili ya kulikata vipande vipande ili baadaye waliuze, lakini wamiliki wa gereji walikataa na kuwaeleza kuwa wanamuogopa RPC wa Mwanza. Vilevile walikuwa wakibeba abiria nyakati za usiku kwa ajili ya kujipatia fedha,” amesema.

Amesema polisi wanaendelea na mahojiano na watuhumiwa wote wawilina  uchunguzi utakapokamilika watafikishwa mahakamani.