Wanafunzi bora Kisarawe kuzawadiwa vifaa vya umeme

Tuesday February 25 2020

 

By Mwandishi wetu

Kampuni ya kuzalisha vifaa vya umeme wa jua ya ZOLA Electric Tanzania,  imetangaza kuwazawadia vifaa vya nishati ya umeme wa jua wanafunzi wa kidato cha nne watakaofanya vizuri kwenye mtihani wa taifa katika wilaya ya Kisarawe.
Wilaya hiyo inayoongozwa na mkuu wake Jokate Mwegelo inaendesha  kampeni inayojulikana kama ‘Bukua na Ushinde’.
Akitangaza ofa hiyo ,Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya ZOLA Tanzania, Yusuph Nassoro,amesema  ‘Bukua na Ushinde’Imelenga kuchochea motisha kwa wanafunzi waliopo mashuleni kusoma kwa bidii ili waweze kufaulu mitihani yao vizuri hususani katika maeneo yenye changamoto ya nishati ya umeme kutoka gridi ya taifa.
“Tunaamini kuwa elimu ni ufunguo wa maisha na jamii ikielimika, inaweza kupiga hatua ya maendeleo kwa haraka,ndio maana tumekuja na mpango huu wa kutoa motisha kwa wanafunzi mashuleni, hususani maeneo yenye changamoto ya nishati ya umeme,” alisema Bw Nassoro.
Alisema wanafunzi watakaofanikiwa kuingia katika 10 bora katika mithani ya taifa ya majaribio watapatiwa zawadi ya vifaa vya kusomea na wanafunzi watatu watakaofanikiwa kuingia katika  3 bora watafungiwa mitambo ya umeme wa sola kwenye familia zao sambamba na kupatiwa vifaa vya kisasa vinavyotumia nishati hiyo.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo, ameipongeza kampuni ya Zola, kwa kubuni mpango huu wenye lengo la kuinua sekta ya elimu kupitia kutoa motisha kwa wanafunzi.
 “Nawapongeza Zola kwa kuja na ubunifu huu ambao utachangia kuinua sekta ya elimu katika maeneo ya vijijini vilevile kwa kuikumbuka wilaya  ya Kisarawe”alisema.
 Aliwataka wanafunzi kuendelea kuchangamkia fursa mbalimbali zinazojitokeza ili ziwasaidie kupata mafanikio na kukamilisha ndoto zao na watambue kuwa kusoma kwa bidii na kupata maarifa ni moja ya njia itakayowapeleka katika kupata mafanikio katika Maisha yao sambamba na kutoa mchango wa kuendeleza Taifa.
Alimalizia kutoa wito kwa makampuni mengine ya biashara kusaidia huduma za kijamii zenye mwelekeo wa kuleta mabadiliko sambamba na kubuni biashara zinazochochea kuongeza fursa za ajira na kujiajiri kama ilivyo kampuni ya Zola.

Advertisement