Wanahabari wapata ajali msafara wa JPM

Muktasari:

  • Ajali hiyo imetokea baada ya gari walilokuwa wamepanda kugongwa na gari jingine, wapelekwa hospitali ya Wilaya ya Meatu kwa matibabu

Simiyu. Waandishi wa habari akiwemo wa gazeti la Mwananchi waliokuwa katika msafara wa ziara ya Rais John Magufuli wilayani Meatu mkoani Simiyu wamepata ajali baada ya gari walilokuwa wamepanda kugongwa na gari jingine.

Waandishi hao waliopelekwa Hospitali ya Wilaya ya Meatu kupatiwa matibabu ni Berensi China na Masunga Samson wa ITV, Aidan Mhando (Channel Ten) na Faustin Fabian wa Mwananchi.

Akizungumza na MCL Digital leo Jumapili Septemba 9, 2018 kaimu mganga mfawidhi wa hospitali hiyo,  Dk Charles Enock amesema wamepokea watu wanne na wanaendelea kuwapatia matibabu.

“Mpaka sasa tumepokea watu wanne na wanaendelea kupatiwa matibabu na hali zao ni njema. Bado tunaendelea kuwaangalia ila hali si mbaya,” amesema.

Taarifa kutoka eneo la tukio zinaeleza kuwa gari hilo lililowabeba wanahabari liligongwa kwa nyuma na  gari jingine wakati likiingia stendi ya mabasi ya Meatu, kwamba wanahabari hao wanalalamika kusikia maumivu sehemu mbalimbali mwilini.

Takribani siku tano zilizopita waandishi wa habari wanane walipata ajali ya gari katika msafara wa Rais Magufuli, uongozi mkoa wa Mwanza ukajitwisha  gharama za matibabu za waandishi hao.

Mkuu wa mkoa wa Mwanza, John Mongella pamoja na kuwapa pole kwa matatizo waliyoyapata, pia amewapongeza kwa kazi kubwa na nzuri waliyoifanya kwenye ziara hiyo.

“Nimeagizwa na Rais Magufuli niwape pole waandishi waliopata ajali kwenye msafara wake na kwamba jambo hilo lilimshtusha na kumsikitisha sana hivyo anaendelea kuwaombea afya zao ziimarike mapema ili waendelee kuihabarisha jamii na kuleta maendeleo,” amesema Mongella.