Wanandoa washikiliwa polisi kwa tuhuma za mauaji ya binti yao

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba, Sheikhan Mohamed Sheikhan

Muktasari:

  • Wakazi wawili ambao ni wanandoa, Abdallah Othman Said na Amina Juma Khatib wa shehia ya Kiungoni Wilaya ya Wete visiwani Zanzibar, wanashikiliwa na polisi kwa tuhuma za mauaji ya binti yao, Rahila Abdalla Othman aliyefariki Septemba 28, 2018

Zanzibar. Jeshi  la Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba linawashikilia baba na mama wa familia moja wakazi wa shehia ya Kiungoni wilaya ya Wete kwa tuhuma za mauaji ya mtoto wao wa kike mwenye umri wa miezi minane, Rahila Abdalla Othman.

Wazazi hao Abdalla Othman Said na Amina Juma Khatib hadi sasa wanaendelea kuhojiwa na Polisi baada ya mtoto wao kukutwa kisimani akiwa amefariki dunia katika tukio lililotokea Septemba 28, 2018 majira ya saa tatu asubuhi.

Akizungumza na MCL Digital leo Oktoba 1, 2018, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba, Sheikhan Mohamed Sheikhan amesema licha ya kuwashikilia wanandoa hao pia jeshi hilo linawashikilia vijana wengine ambao waliachiwa jukumu la ulezi kwa mtoto huyo wakati wazazi wake walipokwenda harusini.

Sheikhan amesema kwa mujibu wa maelezo waliyopokea kutoka kwa wataalamu wa afya, mtoto huyo inaonyesha alifariki dunia kabla ya kuingia kwenye kisima hicho ambapo maiti yake ilipatikana.

Amesema  kutokana na maelezo hayo wamepata mashaka juu ya kifo cha mtoto huyo ukizingatia umbali uliopo kutoka kwenye makazi ya mtoto huyo na umri wake hadi kwenye kisima alichokutwa mtoto huyo akiwa ameshafariki.

“Mtoto huyu ana umri wa miezi minane tu na maiti yake imekwenda kukutwa ndani ya kisima ikiwa inaelea ukizingatia kisima hicho pia kipo mbali, hapa bila shaka kuna jambo na lazima tufanye upelelezi wa hali ya juu kugundua taarifa zaidi kuhusu tukio hili’’ amesema Sheikhan.

Kamanda huyo amewataka wazazi au walezi kuwa makini na watoto wanapoamua kutoka nyumbani kwani wakati mwingine kuwaachia watu wasiokua waaminifu kunaweza kuibuka kwa matukio mbalimbali yakiwemo ya kihalifu.

Kwa upande wake, mama mzazi wa mtoto huyo Amina Juma Khatib amesema tukio la kufariki mtoto wake lilitokea wakati akiwa harusini, hakuwepo nyumbani kwake kwani aliwaachia watoto wengine mtoto wake kwa ajili ya kumlea kama ilivyo kawaida kwa baadhi ya familia.

“Jinsi tukio lilivyotokea mimi siwezi kujua kwani sikuwepo nyumbani, nilikuwa harusini kwa jirani, nilikuja kuitwa na kuambiwa mtoto wangu ametumbukia kisimani tu” amesema.