Wanasiasa wetu wanaogopa watu wasiojulikana?

Makala hii ni matokeo ya maongezi yangu na Mzee mmoja wa Bukoba, Oktoba 10, 2018 tukiwa tunasubiri msafara wa waziri mkuu upite. Sikuwa na lengo la kuongea na mzee huyu ambaye anaelekea umri wa miaka 90, tulikutanishwa na msafara huo.

Barabara ilifungwa kwa muda mrefu, hatukurusiwa kutembea, lakini hatukuzuiliwa kuongea. Kila aliyekuwa mjini Bukoba siku hiyo ni shahidi kwamba barabara zilifungwa kwa saa mbili ili kupisha msafara wa waziri mkuu, ulikokuwa ukitokea Biharamulo.

Kufunga barabara kwa saa mbili ni muda mrefu sana na ni kusimamisha shughuli za wananchi wanaohitaji kila dakika ipitayo ili wajiletee maendeleo.

Maongezi yetu yalianzia hapo, tukihoji ni kwa nini kwenye dunia hii ya sayansi na teknolojia, dunia ambayo mawasiliano yamepiga hatua kubwa, ufunge barabara saa mbili? Tukakubaliana kwamba kumbe kutembelewa na viongozi wa ngazi ya juu kitaifa ni mzigo mkubwa? Badala ya furaha inakuwa kero na usumbufu?

Tulihoji ulinzi mkubwa na wa kutisha wa viongozi wetu. Huko nyuma, tuliamini kwamba viongozi wanaokuwa na ulinzi mkubwa na wa kutisha ni wale ambao nchi zao hazina amani.

Mfano, tulizoea kuona ulinzi mkubwa na wa kutisha wa Rais Yoweri Museveni wa Uganda na viongozi wengine wa Afrika ambao nchi zao hazina amani. Tanzania, viongozi wetu walilindwa, lakini si kwa ulinzi wa wazi tunaoushuhudia hii leo.

Mzee wangu, ambaye tulijenga urafiki kwa kukutanishwa na msafara wa waziri mkuu aliniuliza swali la “uchochezi” baada ya kushuhudia ulinzi wa waziri mkuu, hivi ulinzi huu, wanaogopa nini?

Wanaogopa “mashetani”, ni woga wa kutunga au wanaogopa watu wasiojulikana? Msafara wa waziri mkuu una ulinzi mkali. Lakini pia kwamba kasi ya magari ya msafara ni hatari kwa usalama wake na watu wengine kuliko adui mwingine awaye. Ukisikia msafara ya waziri mkuu au wa Rais umesimamishwa na wananchi, ujue hilo limepangwa, maana kasi ile huwezi kujaribu kuusimamisha msafara.

Ndiyo viongozi wetu wanapendwa, lakini huwezi kujua labda kuna vitu tusivyoviona. Siku hizi kuna dini nyingi zinafukuza “mashetani”, hivyo ni muhimu kuhakikisha viongozi wetu tunawalinda na maadui hawa? Lakini pia kuna watu wasiojulikana ambao wanatushambulia kulia na kushoto, nyuma na mbele.

Mjadala mkubwa ulikuwa juu ya “mashetani” na hasa “mashetani wa kisiasa”. Swali kubwa likiwa je, shetani ni nini? Yawezekana swali likaonekana jepesi na jibu lake tunalijua sote. Lakini si jepesi hivyo!