Wanawake wa kipato cha chini wakombolewa kupitia Vicoba

Muktasari:

  • Mfumo huu ulianza Tanzania miaka 10 iliyopita na umeonyesha mafanikio makubwa kwa wanachama kukopeshana na kusaidiana katika matatizo mbalimbali na pia kuanzisha miradi ya kiuchumi.

Vicoba (Village Community Bank) ni mfumo wa kuweka na kukopa kwa wanachama waliojiunga kwa pamoja na kuunda kikundi kwa malengo ya kujikwamua kutoka kwenye umaskini.

Mfumo huu ulianza Tanzania miaka 10 iliyopita na umeonyesha mafanikio makubwa kwa wanachama kukopeshana na kusaidiana katika matatizo mbalimbali na pia kuanzisha miradi ya kiuchumi.

Vicoba vimesaidia asilimia kubwa ya wananchi kujikwamua na umaskini ambao umetawala. Kupitia Vicoba, jamii imepanua maendeleo yake na Taifa kwa ujumla.

Wapo wanawake mbalimbali ambao leo hii wamekuwa mfano kwa jinsi walivyopata mafanikio kupitia Vicoba.

Rukia Mtopwa ni mmoja wao,  anasema Vicoba imeinua maisha yake, amefanikiwa kujenga, kusomesha watoto lakini pia sasa anaweza kutatua masuala ya kifamilia bila msaada wowote tofauti na ilivyokuwa hapo awali.

“Vicoba imenisaidia kuepukana na aibu ya kuwakopa watu binafsi, watoto nawalipia ada kwa wakati na pia nimeweza kufungua miradi ya ujasiriamali ikiwamo duka la dawa, biashara ya mitungi ya Gas na huduma za kutoa na kuweka fedha kupitia mitandao ya kijami,” anasisitiza Rukia.

“Kwa kifupi Vicoba imekuwa mkombozi wangu nimeweza kununua hata gari ya kutembelea na inanifanya niwe mwanamke ninayejitimizia matatizo yangu bila kutegemea mkono wa pili,”anaongeza. Si hivyo tu Rukia anasema kupitia Vicoba amepata ujasiri wa kuwa mwanamke anayemudu kuwalea watoto wake bila kusumbuana na baba yao ambaye alimtelekeza miaka saba iliyopita.

Kupitia kikundi chao walichokianzisha miaka mitano iliyopita kinachoitwa Wanawake Kiparang’anda (Viwaki) wilayani Mkuranga, Pwani, Rukia anasema kikundi hicho kimekuwa mkombozi kwake.

“Nimefanikiwa kununua shamba na sasa nina mpango wa kujenga mabanda nianze ufugaji au kulima mbogamboga, inategemea na ushauri nitakaopata kwa wataalamu,” anasema Rukia mama wa watoto watatu.

Si Rukia pekee aliyenufaika na Vicoba, Fatuma Omary mkazi wa Mkuranga, Pwani yeye imemsaidia kupata pesa nyingi kwa pamoja.

“Katika Vicoba tunakopeshana kwa riba nafuu, hakuna masharti makubwa. Awali tulishindwa kupata mikopo katika mabenki kutokana na masharti ya kuweka dhamana, kama unavyojua wanawake hatumiliki ardhi kirahisi mali zote zinaandikwa jina la mume lakini pia katika familia zetu mila nyingi hazimmilikishi mwanamke ardhi lakini sasa hali ni tofauti tunakutana kila wiki na kukopeshana kwa urahisi tunadhaminiana wenyewe,” anasisitiza.

Fatuma anasema Vicoba imemsaidia kuungana na wanawake wengine na kubadilishana mawazo jinsi gani wanaweza kujikwamua kiuchumi na kujiongezea kipato.

“Awali nilikuwa nakaa mwenyewe sina mtu wa kunisaidia lakini kupitia Vicoba tunazungumza na wakati mwingine tunawakaribisha walimu wa ujasiriamali, masuala ya fedha na masoko kutupatia elimu.”

Hata hivyo, Fatuma anasema changamoto kubwa wanayokutana nayo ni uaminifu: “Ni nadra kupata wote waaminifu inapotokea mmoja asirudishe mkopo mnarudi nyuma na kukwamisha malengo ya wengine,”anasisitiza Fatuma.

Katika kikundi cha Vicoba cha Upendo, Mary Sengelema ambaye ni katibu wa kikundi hicho anasema kikundi chao kina wanachama 109.

Anasema mwaka jana pekee wametengeneza faida ya zaidi ya Sh12 milioni ambazo wanagawana.

“Kwa mujibu wa katiba yetu, fedha zinazopatikana kutokana na faida tunagawana hivyo kutusaidia katika mahitaji yetu ya msingi,” anasisitiza na kuongeza kuwa lengo la kikundi chao ni kupambana na hali ngumu ya maisha ili kujiongezea kipato.

Naye Sophia Nyambilo ambaye ni mwanachama wa kikundi hicho anasema changamoto iliyopo ni ile ya marejesho hafifu kwa baadhi ya wanachama na kusababisha wengine kukosa mkopo kwa wakati.

 

Vibubu vimepitwa na wakati

Akizungumzia nafasi ya Vicoba, mbunge wa Kibaha Vijijini, Hamoud Jumaa anasema utaratibu wa kuhifadhi fedha kwenye vibubu nyumbani umepitwa na wakati kwa kuwa si salama.

Jumaa pia anasema nyakati za kubweteka zimepitwa na wakati na kwamba hata wanaume hawataki wanawake wasio na kipato.

“Ukijishughulisha na kuhifadhi fedha zako katika vikundi hivi na kukawa na usimamizi imara familia yako haiwezi kukosa mahitaji muhimu kama chakula na fedha za kupeleka watoto shule,”anasisitiza.

Mbunge huyo anabainisha kuwa hata Serikali imekua ikisisitiza watu kujiunga na vikundi ili iwe rahisi kwa halmasahuri na wadau wengine kuwakopesha maana wanaamini zitakua na usimamizi mzuri.

“Nimefurahi kuona wanawake sasa wanajikusanya na kuunda vikundi, kujisimamia na kuweka fedha kisha kupeana mikopo ili kila mmoja anufaike,”anasema.

Jumaa pia anawashauri wanawake hao kuendelea  kushikamana, kufanya marejesho kwa wakati na kutoruhusu mambo ya kinafiki ili kila mmoja anufaike kwa wakati.

 

Mtaalamu azungumza

Mwanasheria na mchambuzi wa shughuli za ujasiriamali Justine Kaleb anasema faida za Vicoba ni pamoja na kutoa mafunzo ya kuongeza ujuzi wa biashara kwa wanachama kupewa fursa au kipaumbele cha kupata mafunzo na ujuzi wa biashara ili kuleta ongezeko na faida kwenye biashara wanazofanya.

Anasema pia, hutoa mafunzo juu ya ujasiriamali na biashara mbalimbali. Hufundisha jinsi ya kuwa mjasiriamali na kubainisha anatakiwa aweje, nini maana yake na faida zake.

“Mara nyingi huwafundisha kutengeneza bidhaa mbalimbali, kuwasaidia kutafuta masoko ya uhakika kwa ajili ya kusambaza na kuuza bidhaa zao kwa bei yenye faida bila wao kunyonywa,”anasisitiza.

Anaongeza kuwa wanachama wanaweza kupata mitaji ya biashara kutoka kwenye kikundi ambayo itawawezesha kuanzisha au kuendeleza biashara zao.

“Biashara za wanachama zitaweza kukua kutoka kiwango cha chini au kutoka kwenye biashara ya mtaji mdogo hadi kuwa mkubwa.”

“Ndiyo kusema si ajabu mjasiriamali aliyeanzia kwenye Vicoba akajikuta anakuwa mfanyabiashara mkubwa anayetegemewa na Taifa katika kuongeza mapato yake kupitia kodi mbalimbali,” anasisitiza.

Kwa mujibu wa mtaalamu huyo, iwapo mhusika atakuwa makini na kufuata kanuni sahihi za kibiashara zilizobuniwa vizuri atafanikiwa zaidi.

Anasema Vicoba pia husaidia kukuza uchumi wa wanachama au wanakikundi kutokana na shughuli ambazo wamekuwa wakijihusisha nazo na ambazo zimekuwa zikiwaletea maendeleo.

“Kukua huku kwa uchumi wao kumeziondolea familia mizigo mingi ambayo ilikuwa ikiwakabili ikiwamo ile ya kusomesha watoto pamoja na pesa ya matibabu pale kunapokuwa na mgonjwa katika familia,” anaeleza.

Pia, Kaleb anasema Vicoba hutoa mikopo kwa wanachama ambayo inawasaidia wanachama (jamii) katika shughuli za kimaendeleo ikiwamo biashara.

Anasema mikopo hii ni nafuu kwa sababu inakuwa na riba ndogo kuliko mikopo ya taasisi nyingine. Riba yake haizidi asilimia 10 katika marejesho yake, hii inasaidia wanachama waweze kurejesha kwa wakati na kwa wepesi.

Anasema wanachama wa Vicoba wana umoja ambao pindi panapotokea matatizo ikiwamo misiba na ugonjwa, husaidiana kwa asilimia kubwa kama inavyokuwa kwa ndugu wa familia moja.

Kwa mujibu wa Kaleb, vikundi hivi vinatoa ajira kwa wanachama. Vimekuwa vikitoa ajira kwa wanachama kutokana na miradi mbalimbali ambayo wamekuwa wakianzisha.

Benki kampuni za simu zawatambua

Kampuni za mawasiliano pamoja na benki mbalimbali nchini zinashirikiana bega kwa bega na wanawake walioamua kujikwamua.

Airtel Tanzania ni miongoni mwa kampuni hizo ambako kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ilizindua huduma mpya ijulikanayo kama Timiza Vikoba yenye lengo la kuviwezesha vikundi vya Vicoba nchini kutumia njia ya kisasa na salama itakayorahisisha ukusanyaji wa michango, kutoa mikopo na marejesho ya mikopo kwa urahisi.

Huduma hii ya Timiza Vikoba inawawezesha wateja walio katika vikundi vya kuanzia watu watano hadi 50 kupata huduma za kifedha saa 24 siku saba za wiki kwa gharama nafuu.

Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Airtel, Beatrice Singano Mallya anathibitisha hilo: “Huduma hiyo italeta uwazi na kuwezesha vikundi vya Vicoba kuhakiki taarifa zao kwa kupata taarifa za miamala mbalimbali kwa wakati kupitia simu zao za mikononi.

Kwa upande wake mkurugenzi mtendaji wa Maendeleo Bank, Ibrahim Mwangalaba anasema wanajisikia fahari kushirikiana na kampuni za simu ili kusaidia wajasiriamali wadogo na wa kati kuweza kuweka akiba zao kupitia simu zao za mkononi.

Anasema kwamba kwa sasa kupanuka kwa huduma za kifedha na kuwafikia wale watumiaji wa kipato cha chini ni lengo mojawapo la benki yao na kwamba mikakati waliyojiwekea ni kuwapatia huduma nzuri na nafuu zinazoendana na utoaji wa mikopo kwa makundi ili kuwapa uwezo wao wenyewe waweze kudhaminiana kwenye makundi yao.

“Lengo letu ni kuhakikisha tunaendelea kuleta na kurahisisha zaidi huduma za kifedha kwa kuweka mikakati kama hii itakayoleta tija katika maendeleo ya jamii nchini,” anafafanua Mwangalaba

Anaeleza kuwa dhamira yao ni kuiendeleza tabia ya kujiwekea akiba katika jamii na pia kuwapa wateja uwezo wa kukopa na kupokea mkopo kupitia simu zao za mikoni kwa kuwa wanaamini hiyo ni njia bora na rahisi zaidi kuliko ile iliyozoeleka.