Wapinzani wamkumbuka Tundu Lissu bungeni

Muktasari:

Leo Septemba 7 umetimia mwaka mmoja tangu mwanasiasa huyo na mwanasheria Mkuu wa Chadema kushambuliwa kwa risasi Mjini Dodoma.

Dodoma. Wabunge wa Kambi ya Rasmi ya Upinzani wameanza kuzungumza bungeni kwa kumkumbuka Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema) Tundu Lissu ambaye leo ametimiza mwaka mmoja tangu apigwe risasi mjini Dodoma katika makazi yake Area D.

Wabunge hao ni Naibu Msemaji wa Kambi hiyo Ally Salehe, Abdallah Mtolea (Temeke-CUF) na Salome Makamba (Viti Maalum-Chadema) wakati wakichangia maoni yao katika Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali wa mwaka 2018 ambao ndani yake kuna marekebisho ya Sheria ya Chama cha Mawakili (TLS).

Mtolea ameanza kuchangia kwa kumtakia afya njema Lissu ambaye bado yupo katika matibabu nchini Ubelgiji

“Leo ni mwaka mmoja tangu mbunge mwenzetu Tundu Lissu apigwe risasi katika makazi yake Area D mjini hapa.”amesema Mtolea.

Hata alipofika wakati wa kuchangia Salome ameanza kwa kumkumbuka Lissu na kusema kuwa Lissu ni sababu kubwa ya mabadiliko ya Sheria ya TLS.