Wataalamu dawa za usingizi changamoto Biharamulo

Muktasari:

Mganga Mkuu wa Wilaya Dk Mashauri amesema ingawa kuna vituo viwili vya afya ya uzazi vinavyotoa huduma kamili lakini changamoto ni uhaba wa wataalamu wa dawa za usingizi.

Bihalamulo. Licha ya kujengwa vituo viwili vya huduma kamili za uzazi wa dharura Nyakanazi na Nyakahura wilayani Biharamuro, bado changamoto kuu ni kukosekana kwa watalaamu wa dawa za usingizi.

Hayo yamezungumzwa jana Septemba 11 na Mganga Mkuu wa Wilaya hiyo, Dk Gabriel Mashauri wakati akizungumzia miradi mbalimbali ya maendeleo inayofadhiliwa na Shirika la Misaada la Marekani (USAID) inayotekelezwa na Usaid Boresha Afya ikiwamo huduma kamili za uzazi wa dharura kabla, wakati na baada ya kujifungua.

Amesema uwepo wa huduma hizo zilizowezeshwa na Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kushirikiana na USAID Boresha Afya, umesaidia kupunguza vifo vya mama na mtoto, huku changamoto kubwa ikiwa ni upungufu wa wataalamu wa dawa za usingizi.

“Uwepo na vituo hivi viwili imesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza vifo baada ya Serikali kutoa Sh500 milioni na wahisani kuchangia vifaa, lakini kila kituo kina mtaalamu mmoja pekee, hivyo inakuwa vigumu kwa wao kupumzika na hata kwenda likizo.”amesema

Dk Mashauri amesema kwa kawaida katika vituo hivyo inapaswa kuwa na zamu tatu kwa madaktari na wauguzi kupokezana, lakini wataalamu hao wa dawa za usingizi wanafanya kazi usiku na mchana siku saba za wiki.

“Angalau tungekuwa na wataalamu sita ili kila kituo kiwe na wataalamu wawili na wengine wawepo katika hospitali ya wilaya,” amesema Dk Mashauri.

Mganga Mkuu Mfawidhi Msaidizi wa kituo cha afya Nyakanazi, Alfred Koikoi amesema kituo chake kinakabiliwa na upungufu wa wataalamu wa dawa za usingizi kwani aliyepo ni mmoja ambaye hata hivyo kwa sasa yupo mafunzoni.

“Tunaye mtaalamu mmoja Kija Mahembo ambaye kwa sasa yupo mafunzoni kwa ajili ya kuongeza ujuzi kuhusu upasuaji salama, tunahitaji tuwe nao angalau watatu kwa maana upasuaji wa dharura unamhitaji mtaalamu huyu wakati wote awe kituo cha kazi,” amesema Dk Koikoi.