Watahiniwa 427,181 kufanya mtihani kidato cha nne kuanzia kesho

Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania, Dk Charles Msonde akizungumza na waandishi wa habari jijini, Dar es Salaam leo kuhusu mtihani wa kidato cha nne unaotarajia kufanyika nchini kote kuanzia kesho hadi tarehe 25 mwezi huu. Picha na Anthony Siame

Muktasari:

  • Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) limesema kuanzia kesho Novemba 5 hadi Novemba 23, 2018 watahiniwa 427,181 watafanya mtihani wa kuhitimu kidato cha nne

Dar es Salaam. Watahiniwa 427,181 wa kidato cha nne katika shule za Sekondari 4,873 Tanzania bara na Zanzibar wanatarajiwa kufanya mitihani yao ya kumaliza kidato cha nne kuanzia kesho Novemba 5 hadi Novemba 23, 2018.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumapili Novemba 4, 2018 Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), Dk Charles Musonde amesema kumekuwa na ongezeko la asilimia 13.82 kwa watahiniwa wa shule kutoka 323,513 wa mwaka 2017 hadi 368,227 mwaka huu.

Kati ya watahiniwa hao wavulana ni 180,908 sawa na asilimia 49.13 na wasichana 187,319 sawa na asilimia 50.87

"Kati ya hao watahiniwa wenye mahitaji maalumu wapo 562 kati yao 372 ni wenye uoni hafifu, 44 wasioona, 109 wenye ulemavu wa kusikia na 37 wenye ulemavu wa viungo," amesema Dk Msonde.

Watahiniwa wa kujitegemea waliosajiliwa ni 58,954 ambapo wanaume ni 26,964 sawa na asilimia 45.74 na wanawake 31,990 sawa na asilimia 54.26.

Watahiniwa hao wa kujitegemea ni pungufu ya asilimia 5.56 ukilinganisha na wale 62,425 waliokuwepo mwaka 2017.

Kati yao walio na mahitaji maalumu wako 384 ambapo wenye uoni hafifu ni 368, wasioona 16.

"Watahiniwa wa mtihani wa maarifa (QT) waliosajiliwa ni 14,348 ambapo wanaume ni 6,358 sawa na asilimia 44.31 na wanawake ni 7,990 sawa na asilimia 55.69," amesema Dk Msonde.

"Kama Necta tumejipanga kikamilifu katika kusimamia mitihani hii na tunawaomba wasimamizi na walimu kuepuka udanganyifu ili matokeo yao yasije kufutwa," ameongeza.