Wawekezaji, FastJet waonja joto la uchumi
Muktasari:
- DSE: Mauzo yameendelea kushuka kwa wiki tatu mfululizo baada ya wiki iliyopita kuporomoka kwa asilimia 87.
- VIWANDA: Wenye viwanda waitaka Serikali ipunguze kodi kwenye bidhaa za msingi zinazochangia kuinua pato la wananchi wa chini.
- USAFIRI WA ANGA: Baadhi ya mashirika ya ndege nchini yameanza kupunguza safari za ndani na nje ya nchi katika kutekeleza mpango wa kubana matumizi.
Dar es Salaam. Baadhi ya wawekezaji kutoka China wamesema kupanda kwa gharama za maisha, hali ngumu ya uchumi na makato makubwa ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kumewasababishia hasara iliyowafanya baadhi yao kukimbilia nchi za jirani na wengine kurejea kwao.
Wawekezaji hao walikuwa wakizungumza wakati wa ziara ya timu ya waandishi wa habari wa China na Tanzania yenye lengo la kufungua pazia la ushirikiano wa vyombo vya habari baina ya nchi hizo mbili katika kuandika na kutangaza taarifa za uwekezaji zinazofanywa na nchi hizo.
Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Sunshine Group, Tonny Sun alisema tozo ya asilimia 18 ya VAT ni kubwa hasa kipindi hiki ambacho biashara nyingi zimeyumba.
Sun alisema ikiwa hali ya biashara itaendelea kama ilivyo, inahatarisha uwekezaji japo kampuni yake iliyotumia zaidi ya dola 100 milioni (Sh216 bilioni) kuwekeza nchini inaendelea kujitahidi ili ifikie malengo yake ya kuwasaidia wananchi.
“Hali ya biashara imekuwa ngumu sana, wenzetu wengine kama asilimia 30 ya wawekezaji wa China wameshindwa kwa sababu hali ya biashara imekuwa ngumu, wapo waliohamia nchi za jirani na wengine wamerudi nyumbani, hali ya biashara imekuwa ngumu,” alisema.
Alisema kampuni yake yenye viwanda zaidi ya vitano vikiwamo vya kuzalisha mafuta ya alizeti na korosho, imeajiri wafanyakazi wazalendo 1,600 na kwamba wakulima wanaowauzia mazao kwa ajili ya kutengeneza bidhaa zao, wananufaika na uwepo wa soko la uhakika.
Aliiomba Serikali isaidie kupunguza kodi kwenye baadhi ya bidhaa za msingi zinazochangia kuinua pato la wananchi wa chini ili kuwawekea mazingira mazuri ya kuendelea na kazi yao.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Star Times, Leo Liao alisema kwa sasa kampuni yake haipati faida kutokana na hali ngumu ya uchumi iliyosababisha asilimia 50 ya wateja wake kushindwa kulipia gharama za ving’amuzi kwa mwezi.
Alisema hali hiyo imewafanya wapunguze bei hadi kufikia Sh6,000 kwa mwezi lakini bado hali imekuwa ngumu.
“Hakuna faida na tunajiendesha kwa hasara kwa sababu ya hali ngumu iliyopo, ninavyoona tunaelekea kufa kabisa kibiashara kwa sababu asilimia 50 ya wateja wetu hawajaweza kulipia huduma. Tunajitahidi kuendelea kutoa huduma nzuri kwa wateja wetu, tumepunguza bei na wateja wanaweza kulipia kwa siku tano hadi wiki moja,” alisema.
Aliiomba Serikali kufuta chaneli zinazoonekana bure ikiwa mteja atashindwa kulipia gharama kwa madai kuwa jambo hilo pia linachangia watu kutolipia.
“Hali ya uchumi imekuwa ngumu na kwa sababu chaneli nyingine ni bure, basi unakuta watu hawalipii kabisa,” alisema.
Alisema mkakati wake ni kuendelea kuboresha huduma kutokana na uwekezaji wake ili kuimarisha urafiki uliopo baina ya Tanzania na China.
Wakati kampuni hizo zikilia, kiwanda cha Nguo cha Tanzania Took kimesema hakijayumba kiuchumi kutokana na bidhaa zake kuuzwa Marekani kwa kampuni kubwa ikiwamo Levis.
Lakini meneja wa kampuni hiyo, Rigobent Massawe alisema imeajiri zaidi ya wafanyakazi wazalendo 1,800 na kwamba inatarajia kuendelea kujiendesha kwa hasara kutokana na gharama za uwekezaji hali itakayodumu kwa miaka mitatu au minne kabla ya kusimama.
“Hata hivyo, tuna bidhaa ambazo hatulipii kodi kwa sababu tumepitia EPZ (Maeneo Maalumu ya Uwekezaji), lakini tungekuwa tunategemea soko la ndani peke yake nasi tungekuwa kwenye hali mbaya,” alisema.
Akizindua mahojiano ya pamoja baina ya vyombo vya habari vya Tanzania na China, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye alisema Serikali itaendelea kushirikiana na China katika masuala ya uwekezaji.
Alisema Watanzania hawana budi kuunga mkono juhudi hizo na kusema wanaobeza suala la uwekezaji hawajui walitendalo.
“Kama wanabeza leo, kesho watatambua mchango wa uwekezaji wa nchi hizi maskini. Hakuna nchi iliyoendelea bila uwekezaji, hata Marekani bado wanaitegemea China katika masuala ya uwekezaji,” alisema.
Alivitaka vyombo vya habari vya China na Tanzania kuwa daraja baina ya nchi hizo mbili kwa kuandika kwa kina habari za uwekezaji zitakazosaidia kukuza maendeleo.
Naibu Waziri na Habari na Uenezi wa China, alisema ushirikiano ulipo baina ya nchi yake na Afrika hasa Tanzania hauna budi kuendelezwa ili kufikia malengo.
“Ushirikiano huu unahitaji kuenziwa, na vyombo vya habari vya nchi hizi mbili vina jukumu la kuhakikisha vinaandika kwa kina habari za uwekezaji ili mema na mazuri ya nchi hizi yaifikie dunia,” alisema.
Alisema China inashirikiana na bara la Afrika katika mambo mengi hususani uwekezaji katika nyanja za kijamii na kiuchumi.
Utata wa kampuni sita
Wakati hali ikiendelea kuwa hivyo, Shirika la Habari la Uingereza Reuters limeripoti kuwa kampuni sita kubwa nchini zinaweza kusitisha shughuli zake kutokana na ongezeko la kodi.
Kampuni hizo zimeelezwa kuwa ni zile zilizowekeza kwenye uchimbaji madini, mawasiliano ya simu na usafirishaji wa baharini.
Katika mahojiano na Reuters na maofisa watendaji wakuu baadhi ya kampuni hizo ambazo hata hivyo, hazikutajwa walisema zinaweza kuhamishia biashara zao nchi nyingine za Afrika Mashariki.
Hata hivyo, alipoulizwa kuhusu taarifa hizo, Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Edwin Ngonyani alisema Serikali haina taarifa rasmi juu ya nia hiyo wala ya kampuni ya usafirishaji mizigo bandarini kama ilivyoripotiwa.
“Ndiyo ninapata hizo taarifa, sina hakika kama Serikali ina taarifa kwa kuwa imetolewa na kampuni zenyewe ambazo hata hivyo, hazijatajwa,” alisema na kuongeza:
“Taarifa imetolewa lakini ni ngumu kupima ukweli kwa sababu mtu aliyetoa hana mamlaka ndiyo maana hawajataja majina halisi ya kampuni hizo. Inaweza kuwa ni uzushi kama mitandao ya kijamii inavyotoa taarifa zisizothibitishwa.”
Taarifa hiyo ya Reuters ilieleza kuwapo kwa kampuni mbili za madini ambazo zipo mbioni kuondoka nchini kutokana na ongezeko la kodi na kuyumba kibiashara.
Kuhusu kampuni za madini, Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo alisema kwa kifupi, “Kodi, hili ni la TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania) na Hazina.”
Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo alisema kodi ni jambo la kawaida kwa nchi yoyote na kwa Tanzania, hupitishwa na Bunge hivyo ni takwa la kisheria ambalo kubadilika kwake ni mpaka lirudishwe bungeni kujadiliwa upya.
“Kila nchi ina utaratibu wake wa kulipa kodi, na kodi hiyohiyo inayolalamikiwa kuna kampuni za Kitanzania zinalipa, ukisema uwaondolee au uwapunguzie wawekezaji wa kigeni utakuwa ni ubaguzi kwa wengine ambao ni wazawa,” alisema Kayombo.
Alisema VAT hulipwa na mlaji na si kampuni ndiyo maana mwisho wa mwezi kama kampuni ililipa, inadai.
Mauzo DSE yaporomoka
Katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), mauzo yameendelea kushuka kwa wiki ya tatu mfululizo baada ya wiki iliyopita kuporomoka kwa asilimia 87.
Katika wiki hiyo iliyoishia Novemba 25, DSE imeeleza kuwa mauzo hayo yalishuka kutoka Sh4 bilioni hadi kufikia Sh500 milioni.
Kushuka huko kulitokana na kuyumba kwa idadi ya hisa zilizouzwa na kununuliwa sokoni hapo kwa asilimia 85 kutoka hisa 671,618 hadi 101,809 wiki iliyopita.
Ripoti ya wiki ya mwenendo wa soko hilo iliyotolewa leo juzi inaeleza kuwa kushuka huko kwa mauzo kunaweza kuhusishwa na ongezeko la mauzo ya hati fungani zilizouzwa sokoni hapo wiki hiyo.
“Wiki hii hati fungani nne zimeuzwa na kununuliwa kwenye soko kwa thamani ya Sh22.1 bilioni sawa na ongezeko la asilimia 33 kutoka mauzo ya wiki iliyopita ambayo hati fungani sita zimeuzwa na kununuliwa kwa thamani ya Sh16.6 bilioni,” imeeleza taarifa hiyo ya DSE.
Mwenendo wa mauzo ya soko hilo yamekuwa na mchanganyiko kwa kushuka na kupanda jambo ambalo limekuwa likiwapa hofu baadhi ya wawekezaji wachanga wa soko hilo. Rekodi za mwenendo wa mauzo kutoka katika soko hilo zinaonyesha kuwa mara ya mwisho mauzo kupanda ilikuwa ni wiki iliyoishia Novemba 4.
Mauzo hayo yalipaa kutoka Sh5.3 bilioni ya wiki ya awali hadi Sh8.3 bilioni.
Licha ya sekta ya benki kukabiliwa na baadhi changamoto, Benki ya CRDB imeendelea kuwa miongoni mwa kampuni tatu zinazofanya vizuri katika soko hilo wiki ya tatu mfululizo. Hata hivyo, katika wiki iliyopita ilikuwa nafasi ya tatu kwa mauzo ya idadi ya hisa kuongezeka kwa asilimia 13.33 nyuma ya Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) yenye asilimia zaidi ya 21 na DSE iliyoongoza kwa ongezeko la asilimia takribani 38.
FastJet yafuta safari
Kadhalika, kampuni ye ndege ya FastJet Tanzania itasitisha safari zake za Dar es Salaam kwenda Nairobi, Kenya na Entebbe, Uganda kuanzia Oktoba 5, ikiwa ni katika kutekeleza mpango wa kubana matumizi.
Hivi karibuni, Mkurugenzi wa FastJet, Nico Bezuidenhout karibuni alitoa maelezo ya kusitisha safari hizo akisema ipo katika mipango ya muda mrefu kujiimarisha kiuchumi, “...Tunafanya hivi kupunguza gharama za uendeshaji...”
Alitaja sababu ya kufikia hatua hiyo kuwa ni upungufu wa abiria na kupungua kwa ufanisi wa uzalishaji katika safari hizo.
“Abiria wote watarudishiwa fedha zao kwa safari ambazo walishazipanga na kununua tiketi kwa hizo safari zilizoahirishwa,” alisema Bezuidenhout.
Ripoti ya fedha ya mwaka 2015 ya Fastjet inaeleza kuwepo mazingira magumu ya kibiashara yaliyosababisha kushuka kwa idadi ya abiria ambayo inabainisha yalitokana na hali ya kisiasa na kiuchumi hususani kuporomoka kwa thamani ya shilingi katika nusu ya pili ya mwaka.Katika mwaka ulioishia Disemba mwaka jana, Fastjet inayoendesha biashara zake kwa mfumo wa nauli nafuu barani Afrika, ilipata hasara ya Dola 21. 9 milioni (Sh47.7 bilioni) ikiwa ni ahueni kutoka hasara ya Dola 72.1 milioni sawa na zaidi ya Sh157 bilioni mwaka 2014.
Miezi ya karibuni kampuni hiyo ilianza kupunguza wafanyakazi wake wakiwamo marubani kisha ilifuatiwa na kuziondoa nchini ndege zake kubwa aina ya Air Bus na kuleta Embrear E 190 iliyokodishwa kutoka Bulgaria ikiwa katika mpango huo wa kubana matumizi.
Safari ambazo zitaendelea kuwepo ni za Dar es Salaam kwenda Mwanza, Kilimanjaro, Mbeya, Zanzibar, Johannesburg, Lusaka na Harare.