Waziri Makamba: Hoja ya muda kwa wazalishaji wa mifuko ya plastiki haina mashiko

Monday April 15 2019

 

By Bakari Kiango,Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais ( Muungano na Mazingira), January Makamba amewataka wafanyabiashara na wazalishaji wa mifuko ya plastiki kuacha  kwenda kwenye vyombo vya habari kuiomba Serikali iwaongezee muda wa matumizi ya mifuko hiyo.

Makamba ametoa kauli hiyo leo, Jumatatu Aprili 15, 2019 wakati wa kikao cha wadau cha wazalishaji na wauzaji wa mifuko mbadala kuhusu fursa za mifuko hiyo baada ya Serikali kupiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki ifikapo Juni Mosi mwaka huu.

"Waache visingizio vya kwenda katika vyombo vya habari. Muda waliopewa umeshaisha na tulitakiwa tupige marufuku tangu mwaka 2017 lakini sakata la virobo likaingilia kati."

"Hakuna mjadala tena kuhusu mifuko ya plastiki atakayezungumza anatuchelewesha kwa sababu athari zake zinajulikana," amesema Makamba

Machi Mosi 2017, Serikali ilipiga  marufuku matumizi ya mifuko ya pakiti ya plastiki ya kufungushia pombe kali maarufu 'viroba'.

Makamba amesema mchakato wa kupiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki ulianza mwaka 2017 kwa Ofisi ya Makamu wa Rais kutuma timu ya wataalamu katika nchi mbalimbali kuangalia namna zilivyofanikiwa kwenye mchakato huo.

"Tulianza tangu mwaka 2016,  lakini ilipofika mwaka 2017 suala la viroba likaja na kwa vile lilikuwa mahsusi na ilibidi tusimame katika mifuko ya plastiki. Ofisi yetu ndio ilipewa jukumu la kupiga marufuku viroba kwa kutumia Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004,"amesema

Makamba ambaye ni mbunge wa Bumbuli, amesema  hoja kubwa ya wazalishaji na wauzaji wa mifuko ya plastiki ni muda mchache lakini ukwel ni kwamba hoja hiyo haina mantiki kwa sasa.

Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi Makamu wa  Rais (Muungano na Mazingira), Balozi Joseph Sokoine amesema lengo la kikao ni kuhamasisha wadau kuhusu fursa ya mifuko ya mbadala baada ya Serikali kupiga marufuku matumizi ya plastiki ifikapo Juni Mosi mwaka huu.

Advertisement