Wilaya ya Mbinga yapokea msaada wa vitabu toka Marekani

Wednesday September 11 2019

Mwakilishi ya taasisi ya The second wind

Mwakilishi ya taasisi ya The second wind Foundation of Seabrook TX ya USA, Clement Kilembe kushoto akikabidhi funguo za kontana lililojaa vitabu kwa Mkuu wa Wilaya ya Mbinga Juma Mnwele wiki iliyopita mjini Mbinga (Picha Kwa hisani ya The second wind Foundation of Seabrook TX). 

Wilaya ya Mbinga wiki hii imepokea msaada wa vitabu mbalimbali kutoka Marekani kwa ajili ya matumizi ya shule za misingi pamoja na sekondari.
Akikabidhi msaada huo, mwakilishi ya taasisi ya The second wind Foundation of Seabrook TX ya USA, Clement Kilembe alisema msaada huo umetolewa na taasisi yao ambayo ni washirika na kampuni ya Seabrook TX Rotary Club’s ya nchini humo.
Kilembe alisema wametoa kontena moja lenye ukubwa wa futi 40 ambamo ndani yake kuna vitabu vya masomo mbalimbali kwa elimu ya sekondari na shule ya msingi.
Alisema kampuni ya Seabrook TX Rotary Club’s imeanzisha mradi ujulikanao kama 'Books for the World Project' na wana mpango wa kutoa makontena 350 nchi mbalimbali duniani.
Alisema Tanzania imenufaika na mradi huo, imepata kontena mbili moja wilaya ya Kibiti lilitolewa mwaka 2017 na mwaka huu wilaya ya Mbinga.Aliongeza kuwa ataongeza jitihada ili kuhakikisha wilaya nyingi zaidi zinanufaika hapa nchini.
Akipokea msaada huo, Mkuu wa wilaya ya Mbinga, Juma Mnwele alisema wilaya yake imefurahi kubahatika na mradi huo na kuahidi kuwa vitabu hivyo atavigawa katika shule mbalimbali pamoja na maktaba ya wilaya ili wanafunzi na wananchi wengine waweze kunufaika na vitabu hivyo.
Mnwele pia alishukuru jitihada zilizofanywa na taasisi ya Maguu Community Based Information Centre Association (MACOBICA) pamoja na kampuni ya Sakyambo Ltd kwa kuhakikisha kontena hilo linafika wilayani Mbinga sababu wahisani ufadhili wao ulikomea Bandarini tu.

Advertisement