Wabunge Kenya wataka kusogeza tarehe ya uchaguzi

Tuesday October 9 2018

Nairobi, Kenya. Wabunge wanatarajiwa wiki hii kupigia kura pendekezo la kubadili tarehe ya Uchaguzi Mkuu kutoka Agosti hadi Desemba huku ushawishi ukiongezeka katika hatua ambayo itauongezea utawala wa sasa kukaa ofisini kwa miezi mine zaidi.
Muswada wa Katiba ya Kenya (Marekebisho) mwaka 2017 unadhaminiwa na Mbunge wa Kiminini Chris Wamalwa.
Pendekezo hilo linataka tarehe ya uchaguzi mkuu wa rais, magavana, wabunge na wajumbe wa mabaraza ya kaunti isogezwe kutoka Jumanne ya pili ya Agosti hadi Jumatatu ya tatu Desemba katika kila mwaka wa uchaguzi.
Wajumbe wengi kati ya wabunge 349 wa Bunge la Taifa wanaunga mkono muswada huo Jumatatu, Dk Wamalwa alisema takriban wabunge 250 wameahidi kuunga mkono ukifika wakati wa kupiga kura.
Muswada huo unahitaji kuungwa mkono na theluthi mbili ya wabunge au wabunge 233 kati ya 349 ili uweze kupitishwa.
“Sina shaka yoyote kwamba muswada utapita kwa sababu ninaungwa mkono na wabunge wengi,” alisema Dk Wamalwa alipokuwa akitoa wito wa kuungwa mkono na wenzake.

Advertisement