AWF yataka Serikali iongeze bajeti utunzaji wa mazingira ya hifadhi

Wakati sekta ya utalii ikiongoza kwa kuliingizia Taifa fedha za kigeni, Serikali imetakiwa kuwekeza kwenye uhifadhi wa mazingira ili wanyamapori waendelee kuwapo na kuvutia watalii duniani.

Hifadhi za Taifa pamoja na vivutio vingine vya utalii vimekuwa vikiliingizia Taifa wastani wa Dola 2 bilioni za Marekani (sawa na trilioni 5) kwa mwaka kutoka kwa watalii milioni 1.1 wanaotembelea Tanzania. Fedha hizo zinasaidia katika miradi mbalimbali ya maendeleo.

Hata hivyo, uhifadhi wa mazingira unakabiliwa na changamoto ikiwamo Serikali kutenga fedha kidogo kwa ajili ya uhifadhi hasa kwa shughuli za ulinzi, upatikanaji wa vitendea kazi na rasilimali watu wa kutosha.

Katika bajeti ya mwaka 2018/19, Wizara ya Maliasili na Utalii ilipanga kutumia Sh29.9 bilioni kwa ajili ya kutekeleza miradi 11 ya maendeleo.

Kati ya fedha hizo, Sh3 bilioni zikiwa ni fedha za ndani na Sh26.9 bilioni zikiwa ni fedha za nje.

Miradi iliyokusudiwa katika bajeti hiyo ni pamoja na mradi wa kusimamia maliasili na kuendeleza utalii kanda ya kusini, mradi wa usimamizi endelevu wa ikolojia ya ardhioevu ya Bonde la Mto Kilombero na Mto Rufiji na mradi wa kujenga uwezo wa mapori ya akiba na kikosi dhidi ya ujangili.

Miradi mingine ni mradi wa misitu asilia, mradi wa kujengea uwezo jamii katika kusimamia rasilimali za misitu, mradi wa kujenga uwezo wa taasisi za mafunzo ya misitu na ufugaji nyuki na mradi wa panda miti kibiashara.

Licha ya kuwa na miradi mingi muhimu, bado bajeti ya fedha za ndani ni ndogo kuwezesha uhifadhi wa rasilimali za Taifa. Utegemezi wa fedha za wahisani unakwamisha jitihada za Serikali katika kutunza mazingira ya hifadhi.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Wanyamapori Afrika (AWF), Kaddu Sebunya anasema huu ni wakati wa Serikali kuongeza bajeti yake kwenye uhifadhi wa mazingira ili kukabiliana na changamoto zinazotishia kutoweka kwa wanyamapori.

“Rasilimali zetu kwa sasa zinakabiliwa na tishio la ongezeko la watu, mabadiliko ya tabianchi na ujenzi wa miundombinu ambayo hatuwezi kuiepuka. Tunachotakiwa kufanya ni kuwekeza zaidi kwenye misitu, mapori na vyanzo vya maji ili kuhakikisha kwamba vinatunzwa kwa manufaa ya sasa na vizazi vijavyo,” anasema Sebunya ambaye anaongoza taasisi hiyo ya Afrika.

Anasema maendeleo ya Afrika yanategemea rasilimali zake na kwamba mazingira asilia ni kitu muhimu katika uzalishaji wa chakula na uendelezaji wa maisha ya kila siku ya binadamu hapa duniani.

Mashirika ya kimataifa hasa la Umoja wa Mataifa (UN) yametoa tahadhari kuhusu mabadiliko ya tabianchi, zikihusisha shughuli za kibinadamu ambazo zimesababisha uharibifu wa mazingira na kuzalisha gesi hatarishi.

Wiki iliyopita, UN iliazimia kwamba mwaka 2021 – 2030 kuwa wa kurudisha mazingira yaliyoharibika (ecosystem restoration), ikisisitiza kwamba itaharakisha uboreshaji wa mazingira yaliyoharibiwa.

Sebunya anasema zaidi ya hekta bilioni 2 za ardhi ulimwenguni zimekusudiwa kurudishwa katika uasili wake kwa sababu zimeharibiwa. Anasema shughuli hiyo inahitaji utashi wa viongozi na bajeti ya Serikali katika uhifadhi wa mazingira.

Sebunya anasema theluthi moja ya ardhi ya Tanzania imehifadhiwa na inatoa makazi ya aina mbalimbali za viumbe kwenye hifadhi za Taifa.

Hata hivyo, anasema nchi hii inakabiliwa na changamoto ya matumizi mabaya ya ardhi, matokeo yake mmomonyoko wa udongo unatokea.

“Tanzania inafanya vizuri zaidi katika uhifadhi kuliko nchi nyingi Afrika na kwa sasa ndiyo inaongoza kwa kuwa na simba wengi duniani.

Mipango ya matumizi bora ya ardhi lazima iwe kipaumbele cha Tanzania ili kuhakikisha inakuwa na ardhi kubwa kwa shughuli za maendeleo za kijamii na kiuchumi,” anasema Sebunya.

Wakati shughuli za maendeleo zikinyooshewa kidole katika uharibifu wa mazingira hususani ujenzi wa mradi wa umeme katika Mto Rufiji (Stigler’s Gorge), Serikali inasema itahakikisha inahifadhi mazingira kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mussa Sima anasema Serikali itahakikisha ujenzi wa mradi wa uzalishaji wa umeme katika bonde la Mto Rufiji unakwenda sambamba na utunzaji wa mazingira. Anasema utunzaji na ulinzi wa vyanzo vya maji yanayotiririka kuelekea Mto Rufiji ni muhimu kwa ustawi na uendelevu wa ujenzi wa mradi mkubwa wa kuzalisha umeme wa ‘Stigler’s Gorge’ kwenye bonde la Mto Rufiji.

“Ofisi yangu itashirikiana kikamilifu na Nemc (Baraza la Taifa la Mazingira) na itahakikisha ujenzi wa mradi wa uzalishaji wa umeme katika bonde la Mto Rufiji unakwenda sambamba na utunzaji wa mazingira,” alisema.