Ajira ni uhusiano wenye sheria, zifuate

Mkataba wa ajira ni makubaliano ya kisheria kati ya mwajiri na mwajiriwa ambapo mwajiriwa anakubali kutoa nguvukazi yake kwa kipindi fulani kwa malipo maalumu ambayo watakuwa wamekubaliana na mwajiri.

Kama ilivyo kwa mikataba mingine, uhalali wa mkataba ni lazima ujengwe katika nguzo kuu tano ambazo ni makubaliano, hiari ya kuingia mkataba, malipo halali, uwezo wa kuingia mkataba pamoja na uhalali wa shughuli yenyewe itakayofanyika.

Kwa mujibu wa Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini ya mwaka 2004, mkataba wa ajira ni lazima uonyeshe jina na anwani ya mwajiri na mwajiriwa, tarehe mliyosaini mkataba, tarehe mkataba unapoanza na tarehe mkataba utakapomalizika.

Ni muhimu mkataba useme mwajiriwa anaajiriwa katika nafasi gani, majukumu yake na mahali atakapofanyia kazi. Itafaa pia kama kipengele cha namna ya kusitisha au kuongeza muda wa mkataba kitakuwepo endapo upande wowote utahitaji kufanya hivyo kwa mujibu wa sheria.

Lazima uweke wazi haki na wajibu wa mwajiriwa kwa mujibu wa sheria za kazi. Mambo hayo yanaweza pia kuorodheshwa kwenye sera ya kazi ya mwajiri endapo atakuwa nayo.

Haki za mwajiriwa ni pamoja na kiwango cha mshahara stahiki, likizo na siku za mapumziko, saa za kazi, mchango wa mfuko wa hifadhi ya jamii kutoka kwa mwajiri na malipo ya muda wa kazi wa ziada.

Haki ya kujiunga na chama cha wafanyakazi, kulipa kodi, kujiunga na mfuko wa hifadhi ya jamii na mengineyo kwa mujibu wa sheria. Haki na wajibu wa mwajiri ni muhimu pia ukaelezwa katika mkataba wa ajira.

Kimsingi haki za mwajiriwa kwa upande mmoja ni wajibu wa mwajiri kwa upande mwingine ni wajibu kwa mwajiriwa hivyo kila upande ukitimiza wajibu wake, kila upande utapata haki zake pasipo kikwazo chochote.

Ni kosa kisheria kumwajiri mtu pasipo mkataba wa ajira. Pia ni kosa kumwajiri mtoto wa chini ya umri wa miaka 14, mtoto wa umri wa miaka 14 hadi 17 anaweza kuajiriwa kwa kazi nyepesi na ambazo hazitamdhuru kiafya wala kuathiri mahudhurio na maendeleo yake shuleni.