Anawaza kumiliki kiwanda cha vipodozi vya mawese

Wataalamu wanashauri kutumia mafuta ya mawese kwa kuwa hayana lehemu ambayo huleta athri katika mwili wa binadamu inayosababidha magonjwa mbalimbali.

Lakini, licha ya uwepo wa malighafi nyingi kama mawese inayoweza kuzalisha mafuta yanayoweza kukidhi mahitaji ya mafuta nchini lakini bado utumiaji wake ni hafifu kutokana na wengi kudai upatikanaji wake siyo wa uhakika.

Jambo hilo lilimfanya Isack Shaban (25) kuitumia kama fursa baada ya kuona katika eneo lililoisha bidhaa hiyo haipo.

Akiwa na mtaji wa Sh400,000 alienda mkoani Kigoma kununua mafuta ya mawese kasha kuyasafirisha na kuwauzia wakazi wa Mabatini jijini Mwanza.

“Kwa wakati huo dumu moja la lita 20 lilikuwa linauzwa Sh25,000 hivyo nilinunua madumu 16 ambayo baadaye kila moja lilitoa madumu manne ya lita 5 niliyoyauza kwa Sh15,000 kila moja,” anasema.

Katika awamu hiyo ya kwanza, anasema alipata faida ya zaidi ya Sh500,000 jambo lilimfanya aongeze bidii katika anachokifanya na kuwahudumia wateja wengi zaidi.

Anasema mpaka sasa mtaji wake umefikia Sh1.5 milioni na badala ya kuuza kwa lita tano pekee, amekuwa muuzaji wa jumla kwa wengine wanaopenda kuuza bidhaa hiyo.

“Biashara hii inaniendeshea maisha bila shida yoyote na wateja wangu nawapata kwa kuzunguka mitaani na kwenye mitandao ya kijamii hivyo kuifanya kutokuwa ngumu sana,” anasema Shaban

Anasema licha ya mara moja moja kukutana na changamoto ya kuletewa mafuta yaliyokaa kwa muda mrefu, lengo lake ni kuwa mfanyabiashara mkubwa wa bidhaa hiyo na kuwatengenezea soko la uhakika wakulima wa chikichi.

“Hapa namaanisha kuanza kutengeneza bidhaa za vipodozi vinavyotokana na mawese ikiwamo sabuni, mafuta, scrub na vingine ili kuhakilisha watu wanaweza kutumia mafuta haya kwa njia mbalimbali,” anasema Shaban