Atumia ngozi ya samaki kutengeneza bidhaa

Baada ya wiki mbili za majadiliano na kutafuta suluhu kwa changamoto zilizopo, mawaziri wa mazingira kutoka nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa (UN) wakubaliana kutumia fursa zilizopo kukabiliana na umasikini uliopo.

Licha ya kupambana na umasikini, mawaziri hao wamekubaliana kubadili namna ya uzalishaji na matumizi ya rasilimali kwa ajili ya maendeleo ya wananchi. Katika kufanikisha hilo, matumizi ya teknolojia yatapewa kipaumbele zaidi.

Wakati mawaziri hao wakitoa kipaumbele kwa ubunifu unaoonyeshwa na wajasiriamali wadogo, takriban watu 5,000 waliohudhuria mkutano wa nne wa Baraza la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) jijini Nairobi walivutika kutembelea banda la Newton Owino, mjasiriamali anayezalisha bidhaa kwa kutumia ngozi ya samaki.

Owino anatambulika na UNEP kutokana na bidhaa zake zinazotokana na uchafu ulioachwa baada ya kuondoa minofu ya sangara wanaovuliwa Ziwa Viktoria.

“Nilianzia biashara hii Tanzania kabla sijahamishia shughuli zangu nyumbani Kisumu. Tanzania kulikuwa na mazingira mazuri sana kwa biashara yangu wakati huo,” anasema Owino katika mahojiano jijini Nairobi.

Kutokana na ngozi hizo za samaki, Owino hutengeneza mikoba, mikanda, ngoma na hata nguo.

Akiwa mhitimu wa Chuo Kikuu cha Pantnagar nchini India ambako alihitimu akiwa na miaka 16 tu, Owino hakusoma kwa kufuata mfumo wa kawaida wa elimu kutokana na mapenzi yake kwenye sayansi.

Anasema, akiwa darasa la sita nchini kwao Kenya, alishiriki mashindano ya Science Congress in Schools yanayotambua ubunifu wa kisayansi unaofanywa na wanafunzi wa shule za msingi na sekondari na akawavutia wasomi waliokuwa wanayafuatilia.

Kwenye mashindano aliyoshiriki, anasema, alikuwepo Profesa Thomas Odhiambo, mwanzilishi wa Kituo cha Kimataifa cha Utafiti wa Saokolojia na Mazingira ya Wadudu (ICIPE).

“Mimi ni mtaalamu wa wadudu. Nayajua maisha yao vizuri sana. Nimejikita zaidi kwenye commercial insects (wadudu waliwao),” anasema.

Kutokana na ubunifu aliouonyesha kwenye mashindano hayo, si Profesa Odhiambo pekee aliyevutiwa na uwezo wa Owino. Alikuwepo pia Profesa Ramesh Chandaria ambaye alimsaidia kwenda nchini India kusoma. Ilikuwa mwaka 1987.

Kwa uwezo wake, anasema alirushwa madarasa ndiyo maana akaweza kuhitimu akiwa na miaka 16 ilhali watu wa kizazi chake walikuwa wanahitimu wakiwa na miaka 24. Anasema baada ya kuhitimu, aliajiriwa na kituo cha utafiti wa malaria India ambako alikaa kwa miaka mitatu tangu mwaka 1991 kabla hajarudi nyumbani alikoajiriwa na ICIPE mwaka 1994.

Akiwa ICIPE, mwaka 1994, alianzisha mradi wake wa kutengeneza bidhaa kwa kutumia ngozi za samaki aina ya sangara wanaopatikana Ziwa Viktoria. Mpaka mwishoni mwa mwaka 2007 anasema aliona ajira inambana kusimamia mradi wake hivyo akaacha kazi na mwaka uliofuata akahamia Dar es Salaam.

“Nilikuwa nafanyia shughuli zangu viwanja vya Sabasaba. Nilikuwa na vijana sita waliokuwa wananisaidia majukumu ya kila siku,” anasema Owino.

Arudi Kenya

Baada ya kuendesha mradi huo kwa miaka mitatu, alipata shauku ya kurudi kwao Kisumu nchini Kenya ambako alienda kuanza upya kwa kuwa hakukuwa na miundombinu ya kutosha.

Kisumu ni upande wa pili wa Ziwa Viktoria, hivyo kuna viwanda vya minofu ya samaki kama ilivyo Mwanza lakini kwa kuwa ni shughuli inayohitaji uzalishaji endelevu, anasema aliweka mkakati wa kuwashirikisha watu wengine.

“Nililazimka kuwafundisha vijana wa kunisaidia na kutengeneza vikundi vya wanawake ili wanisaidie kukusanya malighafi muhimu,” anasema.

Ilimchukua miaka miwili kukamilisha suala hilo, kuanzia mwaka 2011 hadi 2013 na punde milango ikaanza kufunguka. Anasema mwaka 2014 Serikali ya Kaunti ya Kisumu ilimtambua hivyo ikamuunganisha na wizara ya viwanda.

Wizara hiyo ikamuweka kwenye orodha ya wabunifu 18 ambao walipewa fursa ya kuonyesha bidhaa zao mbele ya Rais Barack Obama ambaye wakati huo alitembelea Kenya, akiambatana na jumuiya ya wafanyabiashara.

Kwenye maonyesho hayo, anasema alipata oda nyingi ambazo haikuwa rahisi kukidhi mahitaji yote, hivyo akapeleka maoni ya kukuza sekta hiyo wizarani ambako alikubaliwa.

“Nilipendekeza tuanzishe Chama cha Wasindikaji Ngozi Kisumu (Kisumu Leather Dealers Association). Nilipewa jukumu la kufanikisha hilo na tukaanza kutoa mafunzo kwa watu 18 lakini sasa tupo 37 ambao kila mmoja ameajiri wafanyakazi wasiopungua watano,” anasema Owino.

Kutokana na mikataba aliyoipata kutoka kwa wafanyabiashara walioambatana na Rais Obama, anasema alianza kwa kusafirisha kilo 200 kila mwezi lakini sasa hivi anapeleka tani nne.

Baada ya fursa hiyo, anasema baraza la biashara la wizara ya viwanda nchini humo lilimuunganisha na Switch to Green, mradi wa Umoja wa Mataifa unaohamasisha matumizi ya teknolojia kulinda mazingira. Kutokana na mradi huo kutekelezwa kwenye mataifa mengi duniani yakiwa ya Umoja wa Ulaya (EU), Owino alipata fursa ya kuuza bidhaa zake kwenye nchi hizo.

Akitambua mchango wa Owino, katibu mkuu msaidizi wa Umoja wa Mataifa anayesimamia mazingira, Satya Tripathi alisema Switch to Green ni mradi unaozisaidia serikali na wajasiriamali kuzigeuza changamoto za mazingira kuwa fursa.

Alisema changamoto zilizopo zikiangaliwa kwa jicho la pili ni fursa ya kutengeneza ajira, kukabili umasikini na kutanua shughuli za kiuchumi.

Naye naibu mkurugenzi mkuu wa kamisheni ya ushirikiano wa kimataifa ua Umoja wa Ulaya, Marjeta Jager alisema Swith to Green sasa hivi unatekelezwa kwenye mataifa 39 na zaidi ya kampuni 100,000 na umeshatoa zaidi ya ajira 350,000 kutokana na uwekezaji wa dola 1.1 bilioni za Kimarekani.

Kwa Afrika, mradi huo ulizinduliwa mwaka 2014 na unatekelezwa katika nchi sita na kwa miaka minne iliyopita imezinufaisha zaidi ya kampuni 3,000 kwa mafunzo na kujengewa uwezo uzalishaji.

“Miongoni mwa walionufaika ni Newton Owino ambaye anaonyesha bidhaa zake kwenye mabanda ya maonyesho ya mkutano huu. Yeye anaongeza thamani kwenye mabaki ya samaki ambayo yangepaswa kutupwa,” inasema sehemu ya taarifa ya mradi wa Switch to Green.

Baada ya kupata nafasi hiyo, Owino anasema alianza kusafirisha kilo 10 kwenda Ulaya mwaka 2016 ambazo mpaka sasa zimeongezeka hadi tani nne kila mwezi.

Mafanikio aliyonayo sasa yalianzia Dar es Salaam. Anasema: “Wakati huo Dk John Magufuli alikuwa waziri na alipanga kuhudhuria sherehe hizo, hivyo akataka kumbebea rafiki yake zawadi. Niliona kwenye televisheni akimkabidhi zawadi ile, nilifurahi sana.”