Baada ya kuirasmisha, ilinde biashara yako

Kutokana na ongezeko la mahitaji ya jamii, biashara zinakua zikichangiwa na kushamiri kwa uwekezaji duniani kote.

Wawekezaji wanatafuta fursa Tanzania na Afrika kwa ujumla kama ilivyo kwa Watanzania wanaofanya hivyo pia nje ya miapaka ya Taifa lao.

Kutokana na changamoto nyingi zilizopo kwenye biashara na uwekezaji au masuala mengine ya maisha, bima ni miongoni mwa bidhaa muhimu kuitumia.

Kama kuna jambo la msingi sana kwa mteja wa bima, ni kufahamu haki na wajibu wako. Makubaliano yoyote lazima yatoe haki kwa upande mmoja na wajibu kwa upande mwingine.

Bima ni uhamishaji wa hatari za kiuchumi kutoka kwa mteja kwenda kwa mtoaji wa huduma hiyo zinazoweza kusababisha hasara kutokana na matukio yasiyotarajiwa ambayo huathiri mali, maisha au mwili.

Ni haki ya mteja kufidiwa kulingana na ukaribu wa mazingira yaliyoainishwa katika mkataba kwa kuzingatia chanzo cha ajali. Fidia hiyo haipaswi kupungua wala kuzidi thamani ya mali husika.

Bima haipo kwa ajili ya kumtajirisha ama kumzorotesha mteja kiuchumi bali kumrejesha sehemu aliyokuwapo kabla hajakumbwa na matatizo. Ni wajibu wa mteja kusema ukweli na kutoa taarifa zinazohusiana na mali husika inayokatiwa bima.

Kwa mfano, kama ni gari, basi eleza lina muda gani tangu linunuliwe, huwa unalihifadhi wapi, eleza mazingira yote hatarishi ya sehemu unapolipaki ili mtoaji bima aweze kutambua anakukatia bima ya kiwango gani au kama anaweza kukubali au kukataa kulingana na mazingira ya mali yako.

Wajibu wa kusema ukweli hudumu katika kipindi chote cha makubaliano. Hali hii inatakiwa iwepo kabla ya kuingia hata mkataba unapokamilika.

Ni wajibu wa mteja wa bima kupunguza hasara ama kwa kujitahidi kuepusha majanga yasiyotarajiwa kadri awezavyo ili kulinda mali yake kama vile katika mlipuko wa moto sio kupuuza kwa mantiki kwamba mali hiyo ameikatia bima.

Ni wajibu wa mteja kulipa kiwango cha fedha alichopangiwa kila wakati kadri ya makubaliano na kampuni husika ya bima kumpatia mkataji sera ambazo anatakiwa akubaliane nazo.

Endapo kila biashara itakatiwa bima, wafanyabiashara watakuwa na uhakika wa kuepuka hasara.