Baada ya wiki ya mlipakodi, tathmini ifanyike kupima mchango wake

Pamoja na mambo mengine, Mamlaka ya Kodi Tanzania (TRA), hutoa elimu ya mlipakodi kwa njia mbalimbali ikiwamo vitabu vidogo, vipeperushi na kupitia vipindi vya vyombo vya habari kama luninga, magazeti na redio.

Kwa siku za karibuni, idara ya elimu kwa mlipakodi imejitahidi kutoa elimu kupitia mitandao ya kijamii. Pia imekuwa ikifanya hivyo katika juma la elimu kwa mlipakodi.

Hili ni jambo zuri lakini, ipo haja ya kufanya tathmini ya juhudi za kuwaelimisha walipakodi na kupima matokeo ya juhudi zinazofanywa katka juma hili.

Utafiti unaonyesha Serikali zote duniani huhitaji fedha kwa ajili ya kugharamia bidhaa na huduma za umma kama vile elimu, afya, maji, miundombinu ya kiuchumi kama barabara, bandari, reli na viwanja vya ndege.

Pia serikali zina wajibu wa kutoa ulinzi na usalama kwa raia na mali zao. Ili kufanya yote haya fedha zinahitajika. Fedha hizi hutoka katika vyanzo mbalimbali vikiwamo vya kodi na visivyo vya kodi.

Kodi ni kati ya vyanzo vikuu na vya uhakika vya mapato ya Serikali. Nchi inayokusanya kodi ya kutosha huepuka kukopa hivyo kuzuia ongezeko la deni la Taifa na athari zake.

Pia huepuka kutegemea misaada ya wafadhili ambayo huweza kuwa na masharti magumu, kutotoka kwa wakati na kiasi kilichokubaliwa na kuhitajika. Kwa upande wa wananchi, ulipaji kodi huifanya Serikali kuwajibika kwao zaidi kuliko kuwajibika zaidi kwa wafadhili na wakopeshaji.

Wiki ya mlipakodi

TRA huadhimisha juma la mlipakodi kwa miaka kadhaa sasa. Katka juma hili mambo mbalimbali hufanyika kwa lengo la kuelimisha wananchi mambo mbalimbali ya msingi kuhusu kodi mfano maana ya kodi, aina za kodi, umuhimu wa kulipa kodi, namna ya kulipa kodi na kadhalika.

Juhudi hizi zinapaswa kuleta mabadiliko katika ulipaji kodi. Mabadiliko haya ni pamoja na kupanua wigo wa kodi, kuongeza ukusanyaji wa kodi, kuongeza ulipaji kodi kwa hiyari, kupunguza ukwepaji kodi na kadhalika.

Ni muhimu kufanya tathmini ya kina kuhusu matokeo ya juhudi na rasilimali zinazowekezwa katika juma la mlipa kodi.

Dhana ya tathmini hutumiwa sana katika taaluma ya usimamizi wa miradi pamoja na ya ufuatiliaji. Katika siku za karibuni huunganishwa na dhana ya kujifunza.

Tathmini ni kitendo cha kutizama nyuma baada ya utekelezaji wa jambo fulani ili kupima mambo kwa lengo la kujifunza. Tathmini huweza kuangalia utekelezaji wa kilichopangwa kufanywa, matokeo ya kilichofanywa, ufanisi wa mchakato wa utekelezaji wa kilichofanywa, uendelevu wa kilichofanywa na kadhalika.

Lengo kuu ni kujifunza na kuboresha utekelezaji wa jambo hilo au jambo kama hilo katika mazingira yanayofanana kwa siku zijazo. Kwa kawaida tathmini ni taaluma inayosomewa na ina wataalamu wake. Tathmini ya juma la mlipakodi ni muhimu katika muktadha wa malengo makuu ya juma hili.

Tathmini ya wiki

Tathmini ya wiki ya mlipakodi inaweza kulenga mambo mbalimbali ya msingi kupima matokeo ya wiki hii. Katika hali ya kawaida matokeo yanayotegemewa baada ya maadhimisho ya wiki hii ni kupanuka kwa wigo wa kodi, kuongezeka kwa hiyari ya ulipaji, kupunguza ukwepaji na kuwa na ongezeko la walipakodi. Mwisho wa yote haya ni kuongeza ukusanyaji wa kodi.

Tathmini nzuri ya juma la walipa kodi inapaswa kuwa shirikishi. Wadau wakuu wanapaswa kutoa maoni kuhusu matokeo ya juhudi za kutoa elimu ya mlipakodi katika juma hili. Tathmini nzuri ni ile inayofanywa na mtu wa nje.

Hii ni muhimu ili kutokuwa na mgongano wa maslahi unaoweza kusababisha kujipendelea kama mamlaka itajitathmini yenyewe.

Ni vyema kufanya tathmini kila baada ya muda fulani kama vile mwaka ili kuwa na taarifa ya hali ilivyokuwa kabla. Hii husaidia kufanya ulinganifu wa hali ilivyokuwa kabla na baada ya elimu.

Ni muhimu kupima matokeo ya elimu inayotolewa na kujiridhisha kama kuna haja ya kufanya uchambuzi wa kina kujua iwapo yanachangiwa na elimu iliyotolewa au la.

Hii ni kwa sababu elimu ya mlipakodi ni miongoni mwa mambo yanayochangia matokeo tunayoona. Baada ya tathmini ni muhimu kujifunza.