Bima ya kilimo kuanza kuwanufaisha wakulima nchini

Muktasari:

  • Kutokana na mchango wa kilimo kwenye pato la Taifa na uhakika wa chakula nchini, Serikali inaandaa sera itakayohakikisha wakulima wafidia na kampuni za bima pindi shughuli zao zinapoenda kombo. Mpaka Juni, Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga amesema kila kitu kitakuwa tayari hivyo wakulima wataanza kunufaika kuanzia msimu ujao wa kilimo.

Kutokana na mavuno mazuri ya msimu wa mwaka 2018/19, Tanzania ilikuwa na tani 95,534 za akiba ya chakula huku ikipunguza uagizaji kutoka nje.

Akiba hiyo, taarifa ya kila mwezi ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inaonyesha iliongezeka kutoka tani 92,402 zilizokuwapo Novemba au tani 92,074 za Desemba 2017.

Mwezi huo, Desemba 2018, ripoti hiyo inaonyesha Mamlaka ya Taifa ya Uhifadhi wa Chakula (NFRA) iliuza tani 1,081.9 kwa wafanyabiashara na Jeshi la Magereza huku ikinunua tani 4,213.6 kutoka kwa wakulima kufidia kiasi kilichotoka.

Licha ya umuhimu huo wa kujitosheleza kwa chakula, kilimo ni muhimu pia kwenye kuliingizia Taifa fedha za kigeni. Ripoti hiyo inasema Desemba hiyo thamani ya bidhaa na huduma zilizouzwa nje ya nchi ilishuka kwa asilimia 3.2 na kufika Dola 8.38 bilioni za Marekani ikilinganishwa na Dola 1.02 bilioni za kipindi kama hicho mwaka 2017.

Kushuka kwa mauzo hayo, BoT inasema: “Kulitokana na kushuka kwa mauzo ya chai, korosho na karafuu. Mapato ya korosho yamepungua kutokana na kuchelewa kwa usafarishaji wa zao hilo kulikochangiwa na bei ndogo.”

Pamoja na mchango huo, sekta ya kilimo nchini inakabiliwa na changamoto nyingi zinazotokana na sababu tofauti. Changamoto hizi zinajumuisha bajeti ndogo inayotengwa na Serikali ambayo ni chini ya asilimia 10 kama ilivyopendekezwa kwenye mkataba wa Maputo.

Nyingine ni ukosefu wa masoko ya uhakika, bei zisizotabirika na athari za mabadiliko ya tabianchi zinazosababisha mafuriko au ukame. Wakati mwingine, mlipuko wa magonjwa pia.

Kutokana na changamoto hizi, wakulima wengi hawafanyi kilimo biashara hivyo kipato chao kuendelea kuwa chini.

Kwa kutambua changamoto zilizopo, Serikali imeandaa mpango wa kuhakikisha wakulima wanapata kinga ya changamoto hizo hivyo kuwa na uwezo wa kukabiliana nazo bila kuyumba kiuchumi.

Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga anasema Serikali inazitafuta suluhu ya kudumu kukabiliana na vikwazo vilivyopo ambavyo vinadhorotesha kilimo na kumpunja mkulima mapato anayostahili.

Katika utekelezajia mpango huo, anasema Serikali inaandaa kanzidata au taarifa ya mazao yote ya kipaumbele na sera ya bima ya kilimo ili kuziruhusu kampuni nyingi zaidi kuwahudumia wakulima.

“Mpaka Juni, orodha ya mazao itakuwa inapatikana ili kuzisaidia kampuni za bima kuangalia mazao yapi waanze nayo na nimemwagiza kamishna wa bima kuharakisha mchakato wa uandaaji sera ili kuiwasilisha serikalini kwa hatua nyingine,” anasema Hasunga.

INAENDELEA UK.16

Bima

Kati ya kampuni 29 za bima zilizopo, taarifa zinaonyesha ni chini ya tano zinatoa bima ya kilimo lakini baada ya muda mfupi nyingi zaidi zitajielekeza kwenye sekta hiyo.

Mkurugenzi mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Bima Tanzania (Tira), Dk Baghayo Saqware tayari wadau muhimu wamejulishwa kuhusu mkakati huo wa kufidia hasara wanayoweza kuipata wakulima.

Anasema utaratibu ukikamilika, wakulima nchini watafidiwa kwa mfumo unaotumika kwingineko duniani. “Kuna namna mbili ambayo ni weather index (bima ya majanga ya hali ya hewa) au yield index (bima ya mavuno),” amesema.

Amefafanua kuwa kampuni za bima hulipa fidia kwenye majanga ya asili kama vile mafuriko, ukame au magonjwa kulingana na kiwango cha uharibifu. Mengine ni ya kibinadamu mfano moto au uvamizi wa mifugo shambani. Bila kujali sababu, mkulima bima italipa kulingana na uharibufi uliotokea.

“Kwa mkulima aliyetumia mbegu bora, akapanda vizuri na kwa wakati na kufuata viwango vyote vinavyoshauriwa akiwa na matarajio ya kuvuna maguni 20 kwa mfano lakini kwenye mavuno akapata magunia pungufu, hapo bima itamlipa kiasi kilichopotea,” amebainisha Dk Saqware.

Kampuni

Kampuni za bima zinasema kikwazo kilichopo kwao kushindwa kutoa bima ya kilimo ni ukosefu wa taarifa na wakulima kutojiunga kwenye vikundi ambavyo ni rahisi kuvihudumia.

Kampuni hizo zinasema wakulima waliopo kwenye vikundi na wanaolima maeneo makubwa ni rahisi kuwapa bima na kuwafidia pindi tatizo likitokea.

Kampuni za bima

Mkuu wa kitengo cha biachara wa kampuni ya MGen Tanzania, Lugano Mkisi anasema wao wameanza kutoa bima za kilimo miaka mitano iliyopita wakijikita kwenye mazao ya chakula.

Anasema wanatoa bima kwa wakulima wanaoshiriki kilimo cha mkataba na huwalipa fidia kunapotokea mvua kubwa inayoharibu mazao, wadudu au magonjwa yatakayoathiri mazao kulingana na kiasi cha uharibifu.

“Tunatao bima ya mazao kama vile mahindi, mpunga na maharage pamoja na mlolongo wake mzima wa thamani kutoka shambani hadi sokoni,” anasema.

Kwa upande wake, mkurugenzi mkuu wa Shirika la Bima ya Taifa (NIC), Sam Kamanga anasema wanajiandaa kuanza kutoa bima hiyo hivyo kwa sasa wanajitahidi kutambua mahitaji ya soko.

“Tumepeleka mapendekezo yetu ili tuanze kutoa bima ya kilimo miezi mitatu iliyopita, tunasubiri baraka zao. Tutakapoanza tutaangalia wenye mahitaji makubwa,” anasema.

Kampuni ya First Assurence imesema itaanza kutoa bima ya pamba na tumbaku. Mkurugenzi mtendaji wa kampuni hiyo, Bosco Bugali anasema wamechagua tumbaku na pamba kwa sababu hupandwa katika maeneo makubwa.

“Sekta ya kilimo ni muhimu kufanikisha mipango ya Serikali. Inahitaji kuwekewa mikakati ya uhakika,” amesema.

Wadau

Mkurugenzi mtendaji wa Repoa, Dk Donald Mmari anasema kampuni zikitoa bima ya kilimo itahamasisha vijana kuingia kwenye eneo hilo maana wengi wanaogopa kupata hasara.

Bima hiyo anasema itasaidia kuondoa wasiwasi wa kupoteza mtaji walionao jambo litakalokuwa kichocheo cha idadi kubwa zaidi ya watu kuingia kwenye fursa zilizopo kwenye sekta hiyo.

“Bima ya kilimo ina umuhimu sana maana itasaidia kuinua sekta na kuifanya iwe na mchango mkubwa kwenye pato la Taifa,” amesema Dk Kiondo.

Aidha, amesema bima ya kilimo itafungua milango kwa benki na taaisisi za fedha kutoa mikopo huku kukiwa na uhakika wa kurejeshwa.

Mkulima wa mbogamboga mjini Kibaha, Halima Shemdoe anasema bima hiyo ni muhimu kwani sasa itamuondolea mkulima mawazo yasiyo na majibu.

“Ni ngumu sana kufanya kazi bila uhakika. Kuanza kutolewa kwa bima hii naamini kutaenda sambamba na kupata ushauri wa kitaalamu utakaosaidia kupunguza hasara. Kilimo kitakuwa cha kisasa,” anasema Halima.