Bodi ya Maziwa, Benki ya Maendeleo ya Kilimo kukopesha ng’ombe bora wa maziwa

Muktasari:

  • Baada ya Serikali kuweka mikakati ya kumlinda mzalishaji wa ndani kwa kumpunguzia ushindani kutoka nje, Bodi ya Maziwa Tanzania (TDB) kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) zimeandaa utaratibu wa kuwakopesha ng’ombe wa kisasa wanaotoa maziwa mengi wafugaji wadogo ili kuwaongezea tija.

Dar es Salaam. Ili kuongeza uzalishaji wa maziwa nchini, Bodi ya Maziwa Tanzania (TDB) imeandaa mkakati wa kuwawezesha wafugaji kuongeza tija ya kazi zao.

Mkakati huo unahusisha kuwakopesha ng’ombe wanaotoa maziw amengi kwa bei na masharti nafuu pamoja na kuwajengea uwezo wa kufuga kisasa.

Kufanikisha hilo, kaimu msajili wa bodi hiyo, Dk Sophia Mlote amesema wanashirikiana na Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) na wanaanza na Mkoa wa Tanga ambako tayari mitamba 350.

“Bodi ya maziwa iliingia makubaliano na TADB kuviwezesha vyama vya ushirika mafunzo ya ufugaji bora wa ng’ombe wa maziwa na mikopo nafuu. Mikopo hiyo itahusisha ununuzi wa ng’ombe bora wa maziwa, ujenzi wa mabanda, ununuzi wa pembejeo, vyakula na dawa za mifugo,” amesema Dk Sophia.

Akizungumza na wafugaji aliokutana nao jijini Tanga, Dk Sophia amewataka kuanzisha mashamba ya malisho kwa ajili ya mifugo aliyonayo.

Wajumbe wa kikao hicho kilichohudhuriwa na vyama vya wafugaji wa ng’ombe wa maziwa mkoani Tanga chini ya mwamvuli wa Tanga Dairy Cooperative Union (TDCU) waliomba wapewe maeneo yaliyofutiwa hati kama Amboni Estate, Marungu na Kibaranga ili wayafanye mashamba ya malisho.

Licha ya kuwa zaidi ya ng’ombe milioni 36 hivyo kuifanya nchi ya pili kwa idadi kubwa ya mifugo Afrika ikiwa nyuma ya Ethiopia, Tanzania inazalisha lita bilioni 2.4 pekee kwa mwaka.

Kwa uzalishaji huo, inakadiriwa kila Mtanzania anakunywa lita 47 kwa mwaka badala ya 200 zinazopendekezwa na Shirika la Afya Duniani (WHO).

Miongoni mwa changamoto kubwa zinazowakabili wafugaji ni malisho duni, magonjwa na elimu ndogo ya ufugaji na isiyozingatia kanuni bora wa ufugaji hali inayoshusha uzalishaji wa maziwa.

Kudhihirisha ukubwa wa changamoto iliyopo, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina amesema tanzania inatumia zaidi ya Sh30 bilioni kuagiza maziwa kutoka nje ili kuziba pengo la uzalishaji lililopo.

Kuhakikisha tatizo hilo linashughulikiwa kwa pamoja, maneja biashara wa TADB, Dickson Pangamawe anasema mradi wakuwakopesha wafugaji ni wa nchi nzima ingawa utaanzia Tanga ilii kujifunza na kuona changamoto zilizopo.

“Changamoto iliyopo kwenye sekta ya maziwa ni upatikanaji wa ng’ombe bora wenye uwezo wa kutoa maziwa mengi yatakayomnufaisha mfugaji,” anasema Pangamawe.

Kwa kuanzia, amesema TADB itakopesha ng’ombe 150 wa maziwa kwa vikundi viwili kisha kusambaa nchi nzima.