Jinsi vyuo vikuu vilivyojipanga kuandaa wataalamu wa viwandani

Thursday May 16 2019
VIWANDA PIC

Kutokana na hamasa ya ujenzi wa viwanda vitakavyosaidia kuipeleka Tanzania kwenye uchumi wa kati ifikapo mwaka 2015, vyuo vikuu nchini vimejipanga vyema kuwaandaa watalaamu watakaoshindana vyema kwenye mapinduzi ya nne ya viwanda.

Akieleza mkakati uliopo wakati wa kupitisha bajeti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Naibu Waziri William Olenasha mapema wiki iliyopita, alisema mipango iliyopo ni kuhakikisha inapatikana kompyuta kubwa itakayoweza kuchakata taarifa kubwa.

Na kuonyesha ni namna gani Tanzania imejitayarisha kuingia kwenye mageuzi hayo makubwa, taasisi za elimu ya juu kwa kushirikiana na mamlaka zilizopo zinaandaa mitaala ya kufundishia kozi zitakazowapika wataalam.

Akijibu hoja zilizoibuliwa na wabunge, naibu waziri huyo alikitaja Chuo Kikuu cha Nelson Mandela kuwa kimerekebisha mtaala ili kuanza kutoa shahada ya umaahiri katika mifumo ya bebwa na jongevu (master of science in embedded and mobile systems), shahada ya umahiri katika mifumo ya habari na usalama mtandaoni (masters in information systems and network security) na shahada ya umahiri katika mawasiliano ya pasiwaya na jongevu (master of science in wireless and mobile communicatitions).

Kwa upande wa Taasisi ya teknolojia Dar es Salaam (DIT), alisema wamejipanga kutoa shahada ya umahiri wa uhandisi wa sayansi ya kompyuta (masters of computational science engineering) na Chuko Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) kikitoa shahada ya umahiri ya sayansi katika biolojia molekyuri ya afya jumuishi (master of science in one health molecular biology).

Vilevile, SUA itatoa wahitimu wa shahada ya umaahiri katika uzazi wa wanyama na bioteknolojia na shahada ya awali ya bioteknolojia na sayansi ya maabara.

Advertisement

Taasisi ya Sayansi na Teknolojia Mbeya (MIST), alisema watafundisha shahada ya awali ya sayansi katika akili bandia, shahada ya awali katika sayansi data na shahada ya awali ya uhandisi wa bayotiba.

Kwenye orodha hiyo ya mifano, alihitimisha na Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) alichosema kitaandaa wasomi wa shahada ya awali ya sayansi katika uhandisi wa akili bandia, shahada ya awali ya sayansi katika uhandisi wa sayansi data, shahada ya awali ya sayansi katika uhandisi wa intaneti vifaa na shahada ya sayansi ya awali katika uhandisi na usalama mtandaoni.

“Inawezekana haifahamiki sana huko nje, vyuo vyetu vimejikita kuingia kwenye mapinduzi ya nne ya viwanda ili nasi tuweze kushindana kidunia. Vyuo hivi pia hufanya utafiti katika maeneo mbalimbali,” alisema Olenasha.

Mambo haya hayafanywi bila kushirikisha wadau wa kimataifa. Alisema DIT kwa mfano imeingia mkataba na kampuni ya Belfrix yenyemakao makuu nchini Malaysia wa kuwajengea uwezo Watanzania katika teknolojia ya uhifadhi wa taarifa na takwimu za kidijiti katika sayansi ya kompyuta (broke chain technology) ambayo huongeza ufanisi wa Tehama.

Mkuu wa kitengo cha viwanda na taasisi wa DIT, Dk John Msumba anasema shahada ya uzamili ilishaanza kufundishwa miaka miwili iliyopita.

“Tayari tumeshatoa wahitimu wa kozi hiyo. Mtu anayetaka kujiunga anaweza kupata taarifa azitakazo kwenye tovuti ya chuo,” anasema Dk Msumba.

kuhusu ushirikiano nao na Belfrix Tanzania, anasema wanafundisha kozi za kitaaluma kwa wahitimu.

Na kupitia mradi wa kukuza ujuzi, Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) imetoa mafunzo kwa makamu wakuu wa vyuo vikuu 40 jinsi ya kusimamia mafunzo na uanzishaji mitaala inayoendana na mahitaji ya viwanda vilivyopo na vitakavyoanzishwa.

“Vyuo vitaendelea kubuni mitaala mipya na kuipitia iliyopo ili kukidhi mahitaji ya mabadiliko ya sayansi na teknolojia yaliyopo. Kupitia mradi huu, TCU wameshafanya mafunzo ya kutengeneza mitaala inayoendana na soko na tunategemea wanataaluma 132 watanufaika na mpango huu,” alisema.

Ofisa habari wa Udoma, Beatrice Baltazary anasema kuna shahada zinafundishwa chuoni hapo.

“Kozi nyingine tumepewa kibali na zitaanza kufundishwa mwaka wa masomo 2019/20. Zipo kozi kwa ajili ya watu na diploma na cheti pia,” anasema Beatrice.

Udom kilichoanzishwa mwaka 2007 kina uwezo wa kudahili wanafunzi 40,000.

Pamoja na mipango hiyo inayokusudia kuiweka Tanzania kwenye ramani ya dunia, baadhi ya wataalamu wanashauri kutumia teknolojia iliyozoeleka kwa wananchi kuimarisha uzalishaji.

Kwenye kongamano la maendeleo ya uchumi wa ndani lililoandaliwa na Repoa na kuwakutanisha zaidi ya watafiti 300 kutoka mataifa mbalimbali duniani, msisitizo mkubwa uliwekwa kwenye matumizi ya teknolojia rafiki.

Profesa Peter Knorringa wa Chuo Kikuu cha Erasmus kilichopo jijini Rotterdam, Uholanzi, alisema nchi zinazoendelea Tanzania ikiwamo zinapaswa kunyanyuka kuanzia pale zilizopo ili kuwashirikisha wananchi wote.

“Iwepo sera itakayoruhusu muungano wa teknolojia inayotumiwa na wananchi na mbinu mpya za uzalishaji mali. Ni rahisi kwa wananchi kutumia teknolojia waliyoizoea endapo itaboreshwa,” alisema Profesa Knorringa.

Hata kama dunia inakimbia, alisema Afrika imeonyesha ubunifu na uvumbuzi unaowafaa wananchi wake hivyo misingi hiyo inapaswa kuimarishwa. Alitolea mfano wa huduma za fedha kupitia simu za mkononi ambazo zimeongeza idadi ya wanaozitumia hivyo kurahisisha maisha kwa namna fulani.

Mkurugenzi mtendaji wa Repoa, Dk Donald Mmari kuendeleza teknolojia iliyopo ili kuongeza uzalisha (frugal technology) ni mfumo unaotumika maeneo mengi duniani hivyo Tanzania ipo kwenye nafasi nzuri kuuchangamkia.

“Mfumo huu ni mzuri zaidi kwa sekta isiyo rasmi ambayo huwa ngumu kwao kuendana na mabadiliko ya teknolojia ya kisasa kutokana na kutokuwa na maarifa ya kutosha kuitumia. Ni vyema kampuni zikaanza kutengeneza mashine na mitambo midogo inayoweza kutumiwa na wajasiriamali wadogo,” alisema Dk Mmari.

Kuonyesha jinsi mfumo huo unavyofanya kazi, Dk Mmari alisema powertiller ni muendelezo wa plau za kukokotwa na ng’ombe, teknolojia ambayo wakulima wengi wanaijua hivyo ni rahisi kwao kuitumia.

Advertisement