Kicheko kwa baadhi ya benki kutokana na faida ya 2018

Thursday April 18 2019

 

By Julius Mnganga, Mwananchi [email protected]

Mwaka 2018 umeanza kurudisha furaha kwa baadhi ya watendaji wa benki baada ya kupata faida baada ya kupunguza uwiano wa mikopo chechefu na ile ghafi.

Sababu kadhaa zimechangia kuongeza ufanisi wa menejimenti hivyo kumaanisha furaha kwao na wanahisa pamoja na wadau wengine kutokana na utendaji mzuri mwaka jana tofauti na iliyokuwa miaka miwili iliyopita.

Miongoni mwa sababu hizo ni kupungua kwa uwiano wa mikopo chechefu, kuimarika kwa mapato ya riba, kuongezeka kwa mikopo iliyotolewa kwa wateja na matumizi ya teknolojia kufikisha huduma kwa wananchi.

Miongoni mwa benki zilizoongeza faida yake mwaka jana ni CRDB ambayo ufanisi wake uliongezeka kwa asilimia 78 kutoka Sh36.2 bilioni ya mwaka 2017 hadi Sh64.1 bilioni.

Kutokana na matokeo hayo, mkurugenzi mtendaji wa benki hiyo, Abdulmajid Nsekela anasema wanatarajia kufanya vizuri mwaka huu pia.

“Mwaka 2018 ulikuwa wa mafanikio. Mapato na faida yetu iliongezeka kutokana na kuimarika kwa mapato. Tunao mpango wa kuendelea kujitanua nje ya nchi kwani tuna mtaji wa kutosha na ukwasi unaokidhi mahitaji,” anasema Nsekela.

Nsekela atakuwa miongoni mwa wakurugenzi watakaowasilisha ripoti zao kwa bashasha ikiwa ni mara yake ya kwanza tangu ateuliwe kuiongoza benki hiyo tangu alipoteuliwa kushika wadhifa huo mwaka jana akipokea kijiti kutoka kwa Dk Charles Kimei.

Kwa miaka miwili iliyopita, faida ya CRDB haikuongezeka. Mwaka 2016 kwa mfano, ilipungua kwa takriani Sh50 bilioni ilipopata faida ya Sh74 bilioni na ikashuka tena mpaka Sh36.2 bilioni mwaka 2017 kabla mambo hayajakaa sawa mwaka jana.

Uwiano wa mikopo chechefu ulipungua kutoka asilimia 13.6 mwaka 2017 hadi asilimia 8.5 huku mapato ya riba yakifika Sh586.28 bilioni Sh560.34 bilioni mwaka uliotangulia.

Kutokana na jitihada za kuhamasisha huduma kwa kupitia simu za mkononi mfano kuanzishwa kwa mkopo wa mshahara ambao mtumishi wa umma anaweza kuuomba bila kwenda tawi lolote la benki, Nsekela amefanikiwa kupunguza gharama za riba kutoka Sh150.62 bilioni hadi Sh143.44 bilioni ya ndani ya kipindi hicho.

Operesheni za Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kukagua na kuyafungia maduka ya kubadilisha fedha kuanzia Novemba mwaka jana haikuwa na mchango mkubwa kwa CRDB kwani faida kutokana na miamala ya fedha za kigeni ilipungua mpaka Sh31.32 bilioni kutoka Sh37.35 bilioni zilizopatokana mwaka 2017. Taarifa za benki hiyo zinaonyesha ilipunguza matawi 21 kutoka 255 hadi 234 ambayo, meneja masoko na mawasiliano wake, Godwin Semunyu anasema yalikuwa miongoni mwa taasisi ndogo za fedha na vituo vya huduma.

Idadi ya waajiriwa pia imepungua kutoka 3,164 mwaka 2017 hadi 3,101. Semunyu anasema: “Hiyo imetokana na utaratibu wa kawaida wa idara ya rasilimaliwatu. Kuna waliostaafu, kuacha kazi au kufukuzwa.”

Licha ya CRDB, Benki ya NMB nayo ilikuza faida yake baada ya kodi kutoka Sh95.6 bilioni mwaka 2017 hadi Sh100.96 bilioni mwaka jana ikichangiwa na kuimarika kwa mapato ya riba yaliyofika Sh600.55 bilioni kutoka Sh585.51 bilioni huku gharama zake zikipungua kutoka Sh120.29 bilioni hadi Sh109.61 bilioni.

Faida yake kutokana na miamala ya fedha za kigeni iliongezeka kwa Sh4.51 bilioni na kufika Sh21.89 bilioni ndani ya kipindi hicho huku ikishusha uwiano wa mikopo isiyolipika kutoka asilimia 6.4 hadi asilimia 5.9.

Ili kujiimarisha zaidi, iliongeza idadi ya waajiriwa kutoka 3,371 waliokuwapo mwaka 2017 hadi 3,450 mwaka 2018 sambamba na matawi 11 hivyo kufikisha 223.

Mkurugenzi wa Benki ya DCB, Godfrey Ndalahwa ni miongoni mwa waliosimamia mipango yao vyema baada ya kujihakikishia faida ya Sh995.13 milioni baada ya kodi kutoka hasara ya Sh6.04 bilioni iliyopata mwaka uliopita. Ingawa haikupunguza uwiano wa mikopo chechefu ulioendelea kubaki asilimia 19, ilikuza mapato yasiyo ya riba kutoka Sh2.96 bilioni hadi Sh3.14 bilioni na kupunguza gharama nyinginezo kutoka Sh21.16 bilioni hadi Sh17 bilioni.

Faida Iliyopungua

Ikiwa miongoni mwa benki tatu kubwa zaidi nchini, faida ya Benki ya NBC baada ya kodi ilishuka kidogo na kufika Sh10.32 milioni kutoka Sh15.46 bilioni mwaka.

Kupungua kwa faida hiyo kulitokana na kupungua kwa mapato ya riba yaliyokuwa Sh158.86 bilioni yakilinganishwa na Sh184.33 bilioni mwaka uliotangulia huku ikikata gharama za riba kutoka Sh49.27 bilioni hadi Sh29.53 bilioni.

Hata hivyo, mikakati ya benki hiyo ilisaidia kupunguza uwiano wa mikopo chechefu kutoka asilimia 12.4 hadi asilimia 7.8 na kukuza faida kutokana na miamala ya fedha za kigeni kutoka Sh13.26 bilioni hadi Sh17.17 bilioni.

NBC iliongeza tawi moja hivyo kufikisha matawi 51 na ikaongeza ajira pia. mpaka Desemba 2018 ilikuwa na wafanyakazi 226 kutoka 200 waliokuwapo mwaka 2017.

Ingawa ilijitahidi kukuza faida yake kutokana na miamala ya fedha za kigeni kutoka Sh16.39 bilioni mwaka 2017 hadi Sh26.03 bilioni mwaka 2018 na kupunguza uwiano wa mikopo chechefu kutoka asilimia 8.2 hadi asilimia 3.2, faida ya Benki ya Barclays ilipungua kidogo.

Mwaka 2018, benki hiyo ilipata faida ya Sh6.03 bilioni baada ya kodi ikilinganishwa na Sh9.21 bilioni iliyopata mwaka 2017.

Kushuka kwa faida hiyo, pamoja na mambo mengine,

hesabu za fedha zinaonyesha kulichangiwa na kuongezeka kwa gharama za riba zilizofika Sh18.75 bilioni kutoka Sh16.33 bilioni ilhali mapato ya riba yakipungua kutoka Sh67.52 bilioni hadi Sh66.88 bilioni. Hata hivyo, ndani ya mwaka huo, benki iliongeza wafanyakazi 10 na kufikisha 506 kuhudumia matawi 15 yaliyopo.

Faida baada ya kodi ya Benki ya Standard Chartered ilipungua kwa zaidi ya Sh19 bilioni kutoka Sh39.53 bilioni iliyopata mwaka 2017 hadi Sh20.5 bilioni mwaka jana.

Faida hiyo ilipungua ingawa benki ilijitahidi kupunguza uwiano wa mikopo chechefu kutoka asilimia 8.4 asilimia 0.3. Pamoja na mkakati huo, mapato ya riba yalishuka kutoka Sh125.57 bilioni mwaka 2017 hadi Sh102.22 bilioni ingawa gharama zake zilipungua mpaka Sh26.66 bilioni kutoka Sh46.47 bilioni.

Advertisement