Kikosi cha jeshi Mgulani kuanza kusambaza mkaa endelevu Dar

Ili kuhamasisha matumizi ya nishati mbadala ya kupikia, Jeshi la Wananchi (JWTZ) limesaini mkataba na kampuni ya Tractors kwa lengo la kusambaza mkaa endelevu jijini Dar es Salaam.

Mkataba huo utakaodumu kwa miaka mitatu, umesainiwa kati ya kampuni hiyo yenye makao makuu yake mjini Iringa na kikosi cha jeshi 312 ambacho ni cha huduma.

Mkurugenzi mtandani wa Tractors, Benjamin Lane amesema katika utekelezaji wa mkataba huo, kwa miezi sita ya kwanza kikosi hicho kitapewa tani 100 kila mwezi kuona mwitikio wa soko.

“Kwa sasa tunazalisha kati ya tani 300 hadi 450 kwa mwezi. Tunao mpango wa kuongeza mpaka tani 1,000 kwa siku kadri mahitaji yatakavyokuwa yanaongezeka,” amesema Lane.

Akieleza mkakati wa mabadiliko hayo, mkuu wa kikosi 312, Meja Tumain Kimathi amesema mkataba huo ni sehemu ya utekelezaji wa agizo la Serikali inayozitaka taasisi zote zinazolisha zaidi ya watu 300 kutumia nishati mbadala ya kupikia.

“Tulifanya majaribio ya kuutumia mkaa huu hapa kambini na baadhi ya vibanda vya chakula vya wajasiriamali. Tumepata mrejesho mzuri sasa tunataka vikosi vingine navyo pamoja na askari wetu waanze kuutumia. Utakuwa unauzwa hapa kambini na tutakuwa tunausambaza pia,” amesema Meja Kimathi.

Kwenye Bunge la bajeti linaloendelea jijini Dodoma, waziri wa Mazingira, January Makamba ameaziagiza taasisi zote za umma na binafsi kutumia nishati mbadala ili kuokoa mazingira kutokana na ukataji miti kwa ajili ya kuni na mkaa.

Waziri amesema taasisi yoyote yenye watu wanaozidi 300 ianze kutumia nishati mbadala vinginevyo ivune kuni au mkaa kutoka kwenye shamba lake la miti. Waziri amezitaka kambi za jeshi, hospitali, vyuo vikuu na taasisi nyingine kuzingatia agizo hilo.

Akizungumza kwenye hafla ya utilianaji sahihi mkataba huo, mkuu wa brigedi ya chui, Brigedia jenerali Victor Kisiri amesema kambi nyingi za jeshi zimeachana na matumizi ya kuni na mkaa na kuhamia kwenye gesi hivyo mkaa endelevu unaongeza fursa.

“Uvunaji wa miti una madhara mengi kwetu. Miti ni chakula cha wanyamapori, bila wanyama hao utalii wetu utakufa hivyo kulikosesha Taifa fedha za kigeni,” amesema Kisiri.