Kila mwananchi afahamu ripoti za CAG huonyesha nini

Thursday April 11 2019

Mdhibiti na Mkakuzi Mkuu wa Hesabu za Serikali

Mdhibiti na Mkakuzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Musa Assad. 

Aprili imeanza na mjadala mkubwa baada ya Bunge kukataa kufanyakazi na Mdhibiti na Mkakuzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Musa Assad.

Jambo hili lina maana kubwa na pana katika nyanja mbalimbali ukiwamo uchumi. Yapo mambo kadhaa yanayoonyeshwa katika ripoti za kila mwaka za CAG. Yumkini wengi hawafahamu mambo haya kwa sababu mbalimbali.

Ripoti ya CAG hutolewa kila mwana na huwa inahusu taarifa za fedha za taasisi za Serikali Kuu kwa mwaka wa fedha unaoishia Juni 30. Ni ripoti kubwa.

Ukaguzi wa CAG hufanywa kwa mujinu wa Katiba chini ya Ibara ya 143 (4) pamoja na Kifungu cha 34 (1)(c) cha Sheria ya Ukaguzi wa Umma ya mwaka 2008 sambamba na kanuni zake za mwaka 2009.

Ni ripoti inayokagua mambo mbalimbali ikiwamo matumizi ya fedha, sheria, mifumo ya ndani na masuala ya utawala wa Serikali Kuu; mafaili ya pensheni, ukaguzi maalum chini ya Serikali Kuu na ukaguzi wa vyama vya siasa na masuala yaliyobainika katika ukaguzi wa miaka ya nyuma lakini hayakutolewa taarifa zake kwa kipindi husika.

Inatoa taarifa ya utekelezaji wa mapendekezo ya ukaguzi wa miaka ya nyuma na maagizo ya Bunge. Inahusu utawala bora na unaofuata sheria, uwajibikaji, uwazi, upatikanaji wa huduma na bidhaa za umma, haki na upotevu wa mali ya umma.

Kati ya taarifa 222 za fedha zilizokaguliwa mwaka 2017 ni 190 zilizopata hati inayoridhisha na 24 zikapata hati zenye mashaka. Taarifa tatu zilipata hati isiyoridhisha na tano hati mbaya. Baadhi ya taasisi zilipata hati mbaya kwa kutokuwa na mchanganuo wa matumizi ya fedha za umma.

Hesabu za taasisi 10 za miaka ya nyuma zilikaguliwa pia na mbili zilipata hati inayoridhisha, mbili hati zenye shaka, moja hati isiyoridhisha, na nne hati mbaya.

Utekelezaji

Baada ya ukaguzi, CAG hutoa mapendekezo yanayotakiwa kufanyiwa kazi. Mwaka 2017 kwa mfano, mapendekezo 3,898 ya ukaguzi yalitolewa. Kati ya haya, 1,449 yalitekelezwa kikamilifu, 1,351 yalikuwa katika hatua ya utekelezaji, 842 yalikuwa hayajatekelezwa na 256 yalipitwa na wakati.

Katika ripoti ya 2014/15 kulikuwa na mapendekezo 102 ambayo hayakutekelezwa. Majibu ya Serikali yalionyesha mapendekezo 19 yametekelezwa, 53 yalikuwa katika hatua za utekelezaji, 20 hakujatekelezwa na 10 yalipitwa na wakati.

Licha ya CAG, Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali Kuu hutoa maelekezo pia ambayo kwa mwaka huo inaonyesha ilitoa maelekezo 290 lakini ni 102 tu yalitekelezwa kikamilifu, 87 yalikuwa katika hatua za utekelezaji, 85 hayakutekelezwa na 16 yalipitwa na wakati.

Ukaguzi huo pia huwa unaangalia utekelezaji wa bajeti ya Serikali. Kulikuwapo ucheleweshaji wa kutoa fedha kutokana na kutokuwa na usawa kati ya makusanyo halisi ya mapato na matarajio ya matumizi ya Serikali. Hali hiyo ilichelewesha utekelezaji wa miradi ya maendeleo au kutotekeleza kabisa kwa miradi iliyopangwa.

Kunapokuwa na ucheleweshaji wa fedha, gharama za utekelezaji wa miradi huongezeka na riba zinatokana na kutokulipa wazabuni kwa wakati na malimbikizo ya matumizi hupanda pia.

Udhibiti wa ndani

Ripoti ilionyesha utendaji usioridhisha kwenye idara ya ukaguzi wa ndani kwenye taasisi 34 zilizokaguliwa na ufanisi usiojitosheleza katika udhibiti wa Tehama katika taasisi 31.

Taasisi tatu zilikuwa na bodi duni huku shirika moja halikuwa nayo kabisa wakati bodi moja ilikuwa imemaliza muda wake. Kulikua na taasisi 19 hazikuwa na mpango mkakati wa Tehama endapo majanga yatatokea.

Licha ya eneo hilo, ripoti ilionyesha kulikuwa na wafanyakazi hewa 260 waliolipwa mishahara zaidi ya Sh1.4 bilioni katika taasisi 19.

Taasisi saba zilikata Sh50.5 milioni kutoka mishahara ya wafanyakazi hewa 28 na taasisi nane nyingine zilikuwa na mishahara ambayo haikulipwa kiasi cha Sh1.02 bilioni ambayo ilihifadhiwa kwenye akaunti ya amana badala ya kurejeshwa hazina.

Advertisement