Maelewano kwenye ndoa hufanikisha biashara

Muktasari:

  • Kuna mstari mwembamba kati ya uhusiano mzuri wa wanandoa na kufanikiwa kibiashara.

Ni ngumu kutenganisha mafanikio ya kibiashara na uhusiano mzuri baina ya wanandoa.

Japo wapo waliopambana na kufanikiwa pamoja licha ya uhusiano mbovu na wenzi wao, bado kutegemeana kupo.

Kuna mstari mwembamba kati ya uhusiano mzuri wa wanandoa na kufanikiwa kibiashara.

Misingi mizuri katika ndoa inajengwa na ufahamu na uelewa wa Sheria ya Ndoa kwa sababu uhusiano usio halali kisheria unaweza kuwajibishwa hatimaye kuipoteza biashara au kuvunja uhusiano huo.

Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 inatoa muongozo na sifa za wanandoa, namna na mahali ambapo ndoa inaweza kufungishwa, utaratibu wa kufunga na wenye mamlaka ya kufungisha ndoa.

Sheria inasema ndoa ni muunganiko wa hiari kati ya mwanamume na mwanamke ambao umekusudiwa kuwa wa kudumu.

Ndoa ni mkataba kama ilivyo mingine inayotambulika kisheria. Hivyo vigezo vinavyoufanya mkataba uwe halali hutumika kuhakikisha vimezingatiwa.

Kutofikisha umri, wenza kuwa na uhusiano uliokatazwa kisheria kufunga ndoa kama vile undugu au endapo mmojawapo tayari ameshafunga ndoa ya mume aumke mmoja. Mahakama au baraza la usuluhishi linaweza kuagiza kutofungwa kwa ndoa husika.

Sababu nyingine ni mmojawapo kutoridhia kufunga ndoa hiyo, mmoja kati ya wanandoa kutokuwapo wakati wa kufunga ndoa au ikifungishwa na mtu ambaye hana mamlaka kisheria.

Ndoa zinaweza kuwa halali kisheria lakini mahakama au chombo chochote cha sheria zikazibatilisha. Sababu za kubatilisha ni kutokuwa na uwezo wa kushiriki tendo la ndoa, matatizo ya akili au mke kuwa na mimba ya mtu mwingine ndoa inapofungwa.

Sheria ya Ndoa imeainisha uhusiano unaoweza kuwagharimu wafanyabiashara. Jambo la msingi kwao ni kuwa makini kabla hawajaanzisha uhusiano wa ndoa kwa kumzingatia anayetaka kufunga naye, mazingira ya uhusiano wenyewe na hatua kuihalalisha kisheria na kuwatengenezea mazingira mazuri kibiashara na kisheria.