Mambo muhimu ya kufahamu kuhusu ukuaji wa uchumi

Suala la ukuaji uchumi ni muhimu katika nchi zote ikiwemo Tanzania. Taarifa mbalimbali kuhusu uchumi wa Tanzania zinagusia dhana ya ukuaji inayojumuisha taarifa za kisera, mikakati na bajeti.

Kati ya sehemu muhimu ambapo ukuaji uchumi unatajwa ni dira ya maendeleo 2015, mpango wa miaka mitano ya maendeleo, mpango wa maendeleo wa mwaka mmoja na bajeti. Ukuaji uchumi huzungumzwa sehemu mbalimbali ikiwamo katika kampeni, hotuba na taarifa nyinginezo. Hata hivyo kuna mambo muhimu na ya kimsingi yanayopaswa kufahamika kuhusu dhana hii.

Kwa lugha nyepesi, ukuaji wa uchumi ni kuongezeka kwa thamani ya fedha ya bidhaa na huduma zinazozalishwa katika nchi kwa kipindi fulani. Huduma na bidhaa hizi huzalishwa katika sekta mbalimbali za uchumi kama vile kilimo, viwanda, utalii, usafirishaji, benki, elimu, afya, madini na utalii.

Ukuaji hupimwa kwa kipindi cha mwaka mmoja mmoja. Kunapokuwa na ongezeko, ukuaji huwa chanya na ukipungua huwa hasi. Ukuaji chanya ni neema kwa nchi. Uchumi unapokua, ustawi wa nchi husika huongezeka. Kusudi haya yatokee, lazima masharti kadhaa yatimizwe.

Vichocheo vya uchumi

Ukuaji wa uchumi wa nchi hutegemea hali ilivyo duniani kwa ujumla hasa katika mataifa makubwa kama Marekani na Uingereza. Hutegemea hali ya biashara mjfano bei za bidhaa kama mafuta, madini na nafaka. Ukuaji uchumi hutegemea upatikanaji wa mikopo, hali ya kisiasa, kuibuka kwa magonjwa ya mlipuko kama ebola.

Kwa uchumi kukua uwekezaji ni muhimu sana. Mazingira mazuri, rafiki na ya kuvutia yanahitajika pia. Mazingira haya ni ya kisera, sheria na udhibiti. Uimara na kutabirika kwa sera na sheria ni muhimu kwa uwekezaji hasa wa muda mrefu.

Mambo mengine muhimu kuzingatiwa ni wingi na ubora wa miundombinu, mazingira ya kikodi, nguvukazi, ukiritimba, rushwa na kadhalika. Tukitaka uchumi ukue ni lazima kuzingatia mambo haya na mengineyo.

Ukuaji wa uchumi

Zipo nchi ambazo zina tarakimu kubwa za ukuaji na nyingine tarakimu ndogo. Tarakimu kubwa huwa mbili yaani kuanzia asilimia kumi na kuendelea. Tarakimu ndogo ni ukuaji wa kati ya asilimia moja na tano. Hii ni kwa sababu nchi ambazo zimekuwa na ukuaji wa asilimia sita hadi saba zimehesabika kuwa na ukuaji mkubwa.

Ukuaji mkubwa au mdogo si hoja sana bali ukubwa wa uchumi unaokua. Uchumi mkubwa sana kama wa Marekani kwa mfano ukikua kwa asilimia moja hadi mbili matokeo yake ni makubwa kuliko ukuaji wa asilimia saba wa uchumi mdogo.

Ukuaji wa uchumi unapaswa kuongeza ajira. Ni bahati mbaya ukuaji wa baadhi ya uchumi ukiwamo wa Tanzania hauongezi ajira kwa sababu mbalimbali ikiwamo ukweli kuwa sekta zinazokua ni zinazotumia mitambo na machine badala ya watu wengi.

Kazi ya kufanywa na watu wengi hufanywa na wachache wakisaidiwa na au wakizisaidia mashine na mitambo. Matokeo yake ni ukuaji mkubwa wa sekta husika bila kuajiri watu wengi mfano ni katika viwanda vya kisasa, migodi ya kisasa, bandari, sehemu za ujenzi hata mashamba yenye mitambo.

Kuongezeka umasikini

Kati ya malalamiko na maswali yanayoibuka kila inapokuwapo taarifa ya kukua kwa uchumi Tanzania ni kutogusa mifuko ya wengi hasa watu wa kipato cha chini. Sababu za hali hii ni nyingi.

Huenda ni sekta zinazokua kwa kasi kutumia zaidi mitambo hivyo wananchi hawafaidi ukuaji wake kwa kutoimarisha kipato ambavyo vingepunguza umasikini walionao. Pia sekta zinazokua hazina mwingiliano mkubwa na mzuri na sekta zisizokua kwa kasi.

Pia sekta zinazokua zinaweza kua kwa kiasi kikubwa chini ya umiliki wa kampuni za nje zinazoruhusiwa kuhamisha faida, mapato, mtaji kwenda kwao. Hivyo kama sehemu iliyokua haitawekezwa nchini ukuaji huo hautafika mifukoni mwa wasiomiliki kampuni hizo na kupata gawio.