Mpango wa maendeleo na utekelezaji wa bajeti mpya

Thursday March 21 2019

By Honest Ngowi

Kila mwaka Serikali hupanga na kutekeleza bajeti ambayo utayarishaji wake ni mchakato mrefu. Pamoja na mambo mengine, huanzia pale waziri wa fedha na mipango anapotoa mapendekezo ya mpango wa maendeleo wa Taifa kwa mwaka husika.

Kwa mwaka wa fedha 2019/20, waziri alifanya hivi mwezi Oktoba mwaka 2018. Mapendekezo aliyotoa ndiyo msingi wa bajeti ya mwaka 2019/20. Hii ni kwa sababu bajeti inalenga kutekeleza mpango wa maendeleo kwa kukusanya na kutumia fedha kwa mpango inayoainishwa.

Taasisi na watu binafsi huwa na mipango ya maendeleo. Taasisi hizi ni pamoja na mashirika ya umma na kampuni binafsi. Nchi pia huwa na mipango ya maendeleo ambayo husaidia kutoa mwongozo wa wapi inataka kwenda ndani ya muda fulani.

Mipango hii hubainishwa na malengo mapana ya kimkakati. Kwa Tanzania, mipango ya maendeleo huhabarishwa na mambo kadhaa ya kitaifa, kikanda, bara na kimataifa.

Mambo ya kitaifa kwa mwaka wa fedha 2019/20 ni pamoja na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025, ilani ya ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 ya CCM, Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa miaka mitano (2016/17 - 2020/21) na sera na mikakati ya kisekta.

Mambo ya kikanda ni yanayohusu Jumuiya ya Afrika Mashariki na ushirikiano wa maendeleo kusini mwa Afrika. Kwa Afrika, Umoja wa Afrika na agenda ya maendeleo 2063 huhabarisha mipango itakayotekelezwa.

Advertisement

Kidunia, mipango inahabarishwa na agenda 2030 ya Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs). Ni muhimu kuelewa mambo haya ili kujua kwa nini mipango na bajeti inapangwa kama inavyokuwa.

Kwa mwaka wa fedha 2019/20 kuna mambo mahususi yaliyopangwa kutekelezwa. Haya ndiyo yatakayoipa sura bajeti ya mwaka ujao wa fedha iliyotolewa na Wizara ya Fedha na Mipango.

Miradi ya kipaumbele

Mpango wa 2019/20 una mambo mengi. Baadhi ni hali ya uchumi kwa mwaka huu wa fedha na mapitio ya utekelezaji wake. Leo nitagusia baadhi ya mambo yaliyopo kwenye bajeti ya mwaka 2019/20. Haya ni pamoja na maeneo ya kipaumbele kwa mwaka husika.

Ni muhimu kwa mpango kuweka maeneo ya kipaumbele kwa sababu bajeti haiwezi kutosha kwa kila jambo. Hii si kwa Tanzania tu, bali nchi nyingine zikiwamo zilizoendelea.

Kwa mujibu wa wizara, vipo vipaumbele ambavyo ni pamoja na miradi mikubwa ya kielelezo itakayopewa msukumo wa kipekee. Miradi hii inajumuisha mradi wa umeme wa Rufiji utakaotoa megawati 2,100, kuendeleza ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (SGR) na kuboresha Shirika la Ndege Tanzania.

Mingine ni ujenzi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Uganda hadi Tanga, mradi wa kusindika gesi asilia na kiwanda cha kufua chuma cha Liganga.

Ili miradi hii ilete chachu ya maendeleo inayotarajiwa, ni muhimu ikatekelezwa vizuri sana. Kati ya mambo yatakayosaidia kuifanya iwe na faida ni kutumia rasilimali za ndani kwa kiasi kikubwa.

Hii husaidia kuongeza na kuimarisha ajira, mapato ya nchi na watu binafsi, kukuza ujuzi, kusisimua sekta mbalimbali za uchumi na fedha kiasi kikubwa kubaki ndani ya nchi.

Hata hivyo, Watanzania kushindana kushiriki katika miradi hii. Watakapokosa uwezo, wajengewe.

Vipaumbele vingine

Pamoja na miradi tajwa, mpango wa maendeleo 2019/20 una vipaumbele vingine. Hivi ni pamoja na uanzishaji wa kanda maalum za kiuchumi na kusomesha kwa wingi wataalam kwenye fani na ujuzi adimu.

Kusudio jingine ni kuwa na viwanda vya kukuza uchumi na ujenzi wa msingi wa uchumi wa viwanda. Hii itahusisha viwanda, kilimo, wanyamapori, madini, utalii, biashara na masoko. Kipaumbele kingine ni kufungamanisha uchumi na maendeleo ya watu, kuweka mazingira wezeshi ya biashara na uwekezaji.

Serikali pia imepanga kuongeza usimamizi wa utekelezaji wa mpango huu. Itapendeza iwapo mijadala ya bajeti ndani na nje ya Bunge kuhusu vipaumbele itazungumzia namna Tanzania itakavyofaidika na vipaumbele hivi.

Advertisement